Ni hofu ya maandamano au ni kutotambua mzizi wa tatizo?

BADO tupo katika mtanziko. Ukisikiliza kwa makini yanayoendelea kwenye mitandao ya kijamii, kwenye vijiwe vya kahawa, kwenye baa na mikusanyiko mingine kuhusu hali ya kisiasa nchini Tanzania, yapo maswali magumu ambayo bado hayana majibu.

Maswali haya yanazunguka mduara mmoja, kwamba ni kwa nini neno maandamano limekuwa chanzo cha taharuki kubwa hivyo? Mpaka kufikia Jumatatu wiki hii, yaani Julai 6, 2026 vuguvugu la kuwapo kwa maandamano Julai 7, 2026, lilikuwa limeibua hadharani vyombo vikuu vinavyohusiana na ulinzi na usalama wa nchi hii. Katika hali ambayo ni nadra sana kutokea katika utendaji wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) lilitoa tamko kupitia msemaji wake kuhusu maandamano.

Katika taarifa yake ya Julai 4, 2026, JWTZ ilisema kwamba: Tanzania inaendelea kuwa nchi yenye amani na utulivu; kwamba kuna watu wanaodaiwa kusambaza taarifa za upotoshaji na uchochezi kupitia mitandao ya kijamii ili kuwashawishi wananchi kushiriki vitendo vinavyoweza kuvuruga amani; kwamba halihusiki na madai yanayolihusisha na maandamano; na limewataka wananchi kupuuza wito wowote wa kuvunja amani na kutoa taarifa kwa mamlaka kuhusu viashiria vya vurugu. Limesisitiza kuwa litatekeleza wajibu wake wa kikatiba wa kulinda nchi, wananchi na usalama ikiwa kutatokea vitendo vya kuvunja amani.

Jeshi la Polisi nalo limetoa tamko lake, Msemaji wa Polisi amesema kuwa Jeshi hilo lina taarifa za kiintelijensia kwamba baadhi ya wanaopanga maandamano wanadaiwa kuwa na nia ya kufanya vitendo vya uhalifu kama kuvuruga amani na kuharibu mali; kwamba haki ya kufanya maandamano hailindi vitendo vya vurugu au uvunjifu wa sheria; limeonya kuwa litachukuwa hatua za kisheria dhidi ya yeyote atakayekiuka sheria na kwamba limejiandaa kuhakikisha usalama wa raia na mali zao unakuwako.

Hizi ni kauli za vyombo vya ulinzi na usalama mbali ya kauli za wanasiasa wenye dhamana kubwa katika serikali iliyoko madarakani ambao wamesema kuwa wana ushahidi wa watu kulipwa fedha ili kuandaa maandamano, watu kutengeneza mabomu na tuhuma nyingine nzito kuhusu wapangaji wa maandamano.

Inaeleweka wazi kwamba vyombo vya ulinzi na usalama vina dhima ya kulinda amani nchini. Vina wajibu wa kikatiba na kisheria kutekeleza majukumu hayo. Wajibu huu haujawahi kuwa suala la mjadala. Mjadala unatokea pale utekelezaji wake unapokuwa umekwenda kinyume cha matarajio ya umma. Kwamba badala ya kuulinda umma, yanatokeo kama yale ya Oktoba 29, 2025.

Sasa tujiulize ni kwa nini maandamano yamekuwa yakiibua taharuki, hofu na sintofahamu kubwa nchini kiasi cha kuibua matamko makubwa makubwa kama ambayo yamekwisha kusikika hadi sasa? Hofu chimbuko lake ni nini hasa?

Nizungumzie maandamano kidogo. Maandamano ni suala la haki, pia ni jambo la kisiasa na kijamii. Maandamano yanaakisi muktadha tofauti kulingana na mazingira ya nchi husika, aina ya utawala, na malengo ya kuitishwa kwake. Kwa ujumla, malengo ya maandamano aghalabu huogopesha watawala. Hii ni kwa sababu nyingi. Kubwa ya hizo ni hofu ya kuyumba kwa utulivu wa kisiasa kwani yanaweza kuathiri utulivu wa nchi, hasa yakigeuka kuwa vurugu au kusababisha mgawanyiko mkubwa wa kisiasa. Aidha, maandamano yanaweza kuonyesha hadharani kuwa sehemu ya wananchi hawaridhiki na serikali. Hilo linaweza kuathiri taswira ya serikali ndani na nje ya nchi. Maandamano pia yanaweza kuvuruga biashara, usafiri, utalii na uwekezaji, hasa kama yatadumu kwa muda mrefu, hivyo kuathiri uchumi kwa ujumla wake.

Mara nyingi watawala huhofia kwamba maandamano yanaweza kuchochea madai makubwa zaidi, kama vile mabadiliko ya sera, uchaguzi mpya au hata mabadiliko ya uongozi. Ili kuepuka haya kutokea, kumekuwa na mbinu na juhudi za kuyazuia maandamano yasitokee. Marufuku!

Itakumbukwa kwamba baada ya matukio ya Oktoba 29, 2025 ambayo yaliacha maafa makubwa nchini kwa zaidi ya watu 419 kuuawa kwa risasi za moto, kiu na madai ya maandamano haijawahi kufa. Kulikuwa na vuguvugu la kufanyika kwa maandamano Desemba 9, 2026 siku ya uhuru. Pia hapa katikati kumekuwa na wito wa watu kutaka kufanya maandamano. Mara zote hizi, vyombo vya ulinzi na usalama vimetoa matamko ya kupiga marufuku maandamano hayo, ikiwa ni pamoja na kuweka askari wengi wenye silaha mitaani.

Wakati mambo haya yote yanapotokea, ipo hali inayojijenga ndani ya taifa. Kuongezeka kwa hasira na kutoridhika kwa wananchi; kuzidi kuibua ukosoaji kuhusu haki za kiraia na uhuru wa kujieleza; na kuongezeka kwa mazingira ambayo migogoro inakuwa ya muda mrefu badala ya kutatuliwa ndani ya taifa.

Historia duniani kote inashuhudia kwamba nchi nyingi, nasi Tanzania tukiwamo, huzuia maandamano bila kushughulika na sababu zinazowafanya watu watake kuandamana. Ikiwa chanzo ni malalamiko kuhusu uchumi, huduma za umma, ufisadi, haki za kisiasa au uchaguzi, malalamiko hayo yataendelea hata kama maandamano yatakuwa yamezuiwa. Na hiki ndicho kimetukaa au kutuganda kwa sasa.

Wiki iliyopita Spika wa Bunge Azzan Zungu alikutana na wahariri kuzindua maadhimisho ya miaka 100 ya Bunge. Katika kikao kile, maswali yaliulizwa. Baadhi yalijikita juu ya wajibu wa Bunge kama muhimili katika kuhakisha haya malalamiko ya wananchi – katiba mpya, haki za kidemokrasia na kisiasa, vinapatikana. Majibu ya Spika Zungu kwa maoni yangu, hayakuwa ni ya kiongozi wa muhimili wenye dhima ya kuisimamia serikali. Ni kama alikuwa anaeleza kuwa matatizo ya haya madai – katiba mpya, uwanja sawa wa kisiasa na haki za kidemokrasia nchini, matukio ya utekaji, mauaji yaliyotokea na yanayoendelea kutokea, kidole cha lawama kinapaswa kuelekezwa kwa watu fulani. Hakuwataja moja kwa moja. Ila alielekea kurusha lawama kwa upinzani.

Picha ya ujumla inayojengwa kwa nguvu na juhudi kubwa na watu wenye dhamana za uongozi katika nchi hii, ni kwamba haya madai yanayofungamanishwa na maandamano, ni vitu vya kufikirika. Ni hila za watu wasioitakia mema nchi yetu. Ni mipango ya maadui wa taifa letu. Kwa mantiki hiyo, haya siyo madai ya Watanzania.

Ijapokuwa ni haki kuruhusu kila mwenye maoni yake kwa jambo lolote azungumze, dhana inayojengwa kwamba vuguvugu na msukumo wa kutaka maandamano nchini ni vitu vya kushinikiza kutoka nje, na kwamba watu wetu wanalipwa ili kusukuma ajenda hiyo, ni msimamo wa hatari dhidi ya ustawi wa taifa. Wenye dhamana wanapaswa kujiuliza tena kwa nini kiu ya maandamano haimalizwi kwa matamko ya wanasiasa na vyombo vya usalama? Kwa nini mzizi hautafutwi, kazi kubwa imebaki ni kufinyanga utetezi usiokuwa na mashiko? Siku wenye dhamana watakapokiri kwamba kiu ya maandamano inasababishwa na hali halisi ya madai ya wananchi, labda tutapiga hatua kuondoa kiini cha kiu ya maandamano haya.

spot_img

Latest articles

Mbeya City yabaki Ligi Kuu,  kocha akiri kukumbana na changamoto

Na Mwandishi Wetu Klabu ya Mbeya City imefanikiwa kusalia Ligi kuu ya soka  Tanzania bara...

TOSCI: Mbegu bora ni msingi wa kuongeza tija na kukuza uchumi

Na Mwandishi Wetu TAASISI ya Kudhibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI) imewahimiza wakulima kutumia...

TPRB YAENDELEA KUTOA HUDUMA SABASABA, YAPOKEA MAOMBI YA USAJILI

Na Mwandishi Wetu Bodi ya Usajili wa Wataalam wa Mipangomiji (TPRB) imeendelea kutoa huduma...

EWURA CCC yatoa elimu ya matumizi sahihi ya nishati na maji Sabasaba

Na Mwandishi Wetu BARAZA la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Nishati na Maji...

More like this

Mbeya City yabaki Ligi Kuu,  kocha akiri kukumbana na changamoto

Na Mwandishi Wetu Klabu ya Mbeya City imefanikiwa kusalia Ligi kuu ya soka  Tanzania bara...

TOSCI: Mbegu bora ni msingi wa kuongeza tija na kukuza uchumi

Na Mwandishi Wetu TAASISI ya Kudhibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI) imewahimiza wakulima kutumia...

TPRB YAENDELEA KUTOA HUDUMA SABASABA, YAPOKEA MAOMBI YA USAJILI

Na Mwandishi Wetu Bodi ya Usajili wa Wataalam wa Mipangomiji (TPRB) imeendelea kutoa huduma...