TOSCI: Mbegu bora ni msingi wa kuongeza tija na kukuza uchumi

Na Mwandishi Wetu

TAASISI ya Kudhibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI) imewahimiza wakulima kutumia mbegu bora zilizoidhinishwa, ikisema ndizo msingi wa kuongeza uzalishaji wa mazao, kuimarisha usalama wa chakula na kufanikisha azma ya Serikali ya kukuza mchango wa sekta ya kilimo katika uchumi wa taifa.

Akizungumza katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), Mkaguzi wa Mbegu wa TOSCI, Fatuma Nasoro, alisema matumizi ya mbegu bora ni nyenzo muhimu ya kuifanya sekta ya kilimo kuwa ya kisasa, yenye tija na inayochangia ukuaji wa uchumi.

Alisema Serikali kupitia Ajenda ya 10/30 imelenga kuongeza mchango wa sekta ya kilimo hadi kufikia asilimia 10 ya ukuaji wa uchumi, na kwamba matumizi ya mbegu bora ni miongoni mwa nguzo muhimu za kufikia lengo hilo.

“Kilimo ni biashara, na biashara hiyo haiwezi kuwa na tija bila matumizi ya mbegu bora. Mbegu bora humwezesha mkulima kupata mavuno mengi, yenye ubora na kuongeza kipato chake,” alisema Fatuma.

Alieleza kuwa TOSCI, ambayo ipo chini ya Wizara ya Kilimo, ina jukumu la kuhakikisha mbegu zote zinazowafikia wakulima zinakidhi viwango vya ubora kwa kuzifuatilia kuanzia hatua ya ugunduzi, uzalishaji, usambazaji hadi zinapofikishwa kwa mkulima.

Alisema taasisi hiyo pia hufanya ukaguzi wa mbegu zinazouzwa sokoni ili kuhakikisha zinaendelea kukidhi viwango vilivyowekwa na kulinda maslahi ya wakulima.

Kwa mujibu wa Fatuma, matumizi ya mbegu bora hayasaidii tu kuongeza mavuno bali pia yanaimarisha usalama wa chakula na kutoa fursa kwa wakulima kuuza ziada ya mazao katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

“Kadiri wakulima wanavyoongeza uzalishaji kwa kutumia mbegu bora, ndivyo wanavyoongeza kipato chao na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa kupitia sekta ya kilimo,” alisema.

Aidha, aliwahimiza wakulima na wananchi kutembelea banda la TOSCI katika Maonesho ya Sabasaba ili kupata elimu kuhusu tasnia ya mbegu, namna ya kutambua mbegu bora na huduma mbalimbali zinazotolewa na taasisi hiyo.

Alisisitiza kuwa TOSCI itaendelea kutoa elimu kwa wadau wa kilimo kuhusu umuhimu wa kutumia mbegu zilizoidhinishwa, akibainisha kuwa matumizi ya mbegu bora ni uwekezaji wenye faida kwa mkulima.

“Mbegu bora haigharimu, inalipa. Tunawahimiza wakulima wote kutumia mbegu bora ili kuongeza tija, kukuza kipato na kuchangia maendeleo ya sekta ya kilimo na uchumi wa nchi,” alisema.

spot_img

Latest articles

RAIS SAMIA KUZINDUA RASMI MRADI WA JNHPP AGOSTI 22, 2026

📌Waziri Ndejembi asema ni tukio la kihistoria litakaloshuhudiwa na watanzania pamoja na wageni 📌Asema...

JAJI MSHIBE ASISITIZA MAANDALIZI YA KISEKTA KATIKA KUKABILIANA NA ATHARI ZA EL NIÑO

Na Mwandishi Wetu MWENYEKITI wa Bodi ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA),...

Msajili wa Hazina, Fitch Ratings watathmini mageuzi ya taasisi za umma

Na Mwandishi wa OTR OFISI ya Msajili wa Hazina (OTR) Jumanne, Agosti 11, 2026, ilifanya...

More like this

RAIS SAMIA KUZINDUA RASMI MRADI WA JNHPP AGOSTI 22, 2026

📌Waziri Ndejembi asema ni tukio la kihistoria litakaloshuhudiwa na watanzania pamoja na wageni 📌Asema...

JAJI MSHIBE ASISITIZA MAANDALIZI YA KISEKTA KATIKA KUKABILIANA NA ATHARI ZA EL NIÑO

Na Mwandishi Wetu MWENYEKITI wa Bodi ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA),...