Na Tatu Mohamed
WAZIRI wa Nchi ofisi ya Rais Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka, ametangaza uzinduzi wa shindano la kitaifa la ubunifu lijulikanalo kama Vijana Uchumi Challenge, likilenga kuwapa vijana jukwaa la kutoa mawazo yatakayosaidia kukuza uchumi wa taifa na kukabiliana na changamoto za kiuchumi zinazoikabili dunia kwa sasa.
Pia Waziri Nanauka alitoa wito kwa vijana kote nchini kujitokeza kwa wingi kushiriki shindano hilo, akisisitiza kuwa ni fursa muhimu ya kuonesha uwezo wao wa kufikiri na kuchangia maendeleo ya taifa.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Waziri Nanauka amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuweka mbele ajenda za vijana na kuhakikisha wanashirikishwa kikamilifu katika maamuzi ya kitaifa pamoja na mipango ya maendeleo.

Amesema kupitia jukwaa la Vijana Platform lililoanzishwa mwaka 2026, serikali imefanikiwa kuwafikia vijana katika mikoa mbalimbali, ambapo zaidi ya mawazo ya ubunifu 1,367 yamekusanywa na washindi 15 tayari wamewezeshwa mitaji ya jumla ya Sh milioni 15.
Waziri Nanauka alieleza kuwa majukwaa hayo yamejikita katika kusikiliza sauti za vijana, kujifunza kutoka kwao, kushirikiana nao na kuwawezesha kutimiza ndoto zao, hatua ambayo imekuwa chachu ya kuibua ubunifu na suluhisho katika jamii.
Aidha, alisema hatua hiyo inaendana na Sera ya Maendeleo ya Vijana ya mwaka 2007 iliyoboreshwa mwaka 2014, inayotambua ubunifu na uvumbuzi kama nguzo muhimu ya maendeleo ya kiuchumi nchini.

Katika shindano hilo jipya, Waziri Nanauka alibainisha kuwa jumla ya Sh milioni 50 zitatolewa kwa washindi watakaowasilisha mawazo bora yatakayosaidia taifa kukabiliana na changamoto za kiuchumi zitokanazo na misukosuko ya kimataifa.
Alisema zaidi ya asilimia 55 ya nguvu kazi ya Tanzania ni vijana wenye umri wa kati ya miaka 15 hadi 35, hivyo ni muhimu kuwapa nafasi ya kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa uchumi imara na endelevu.
“Dunia inapitia mabadiliko makubwa ya kiuchumi, kisiasa na kiteknolojia, hivyo tunahitaji kutumia ubunifu wa vijana wetu kama nguzo ya kukabiliana na changamoto hizi,” alisema.

Kwa upande mwingine, Waziri huyo alitangaza kuundwa kwa kamati ya kitaifa ya vijana itakayoratibu na kusimamia shindano hilo, ikiwa na jukumu la kuhakikisha mchakato unakuwa wazi, jumuishi na usio na upendeleo.
Aidha alieleza kuwa kamati hiyo itahusika na kuratibu upokeaji wa mawazo, kutoa elimu kwa vijana, kuchagua majaji na kuandaa shughuli zote za shindano hadi kupatikana kwa washindi.
Aliongeza kuwa serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki yatakayowawezesha vijana kukuza vipaji vyao, kuanzisha miradi na kushiriki kikamilifu katika uchumi wa nchi.

Katika kuhitimisha, Waziri Nanauka alisisitiza dhamira ya serikali ya kuhakikisha kila kijana anapata fursa sawa bila upendeleo, huku akiwataka wanahabari kuendelea kuhamasisha ushiriki wa vijana katika programu za maendeleo.
Alisema kupitia shindano hilo, vijana wataweza si tu kuibua mawazo bunifu bali pia kuwa sehemu ya suluhisho la changamoto zinazoikabili Tanzania na dunia kwa ujumla.


