Rais Samia avaa viatu vya Mwalimu G20

Rio de Janeiro, Brazil

RAIS Samia Suluhu Hassan ameyataka mataifa tajiri duniani ya kundi la G20 kutafakari upya namna bora ya kukabiliana changamoto za njaa na umaskini duniani, akirejea msimamo thabiti wa Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere.

Akizungumza mbele ya wakuu wa nchi na serikali za mataifa tajiri zaidi duniani wa kundi la G20, Rais Samia aliyataka mataifa hayo, kutafakari upya juu ya sera za kifedha, mikopo, madeni kwa nchi maskini kama Tanzania.

G20 ni kundi linalojumuisha mataifa wanachama tajiri 19 wakiwamo Marekani na China na mashirika mawili ya Umoja wa Afrika (AU) na Jumuiya ya Ulaya (EU) ndizo ziliushika uchumi wa dunia katika umoja wao kwa asilimia 85.

Akizungumzia madeni, hoja ambayo Mwalimu na wenzake wa kundi la nchi kusini ambao kati ya mwaka 1987 na 1990 wakati akiwa Mwenyekiti wa Tume ya Kusini walipigania kufutwa, Rais Samia aliyataka mataifa tajiri kufikiria namna ya kuzitua mzigo mkubwa wa madeni nchi masikini duniani.

Kimantiki, hotuba ya ushawishi ya Rais Samia katika mkutano huo wa jana wa G20 ilirejesha hoja ambazo mwaka 1991, zilizaa azimio lilipopitishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lililotokana na Ripoti ya Tume ya Kusini iliyoongozwa na Mwalimu Nyerere.

Pamoja na mambo mengine, kushabihiana kwa hoja za Rais Samia na Ripoti ya ‘Tume ya Kusini’, ni kuendelea kuwapo na pengine kustawi kwa changamoto za kibiashara na kiuchumi na namna mataifa tajiri na maskini yanavyopaswa kufikia mwafaka wa kuondoa hali ya msigano iliyopo.

Mbali na changamoto ya kutua kwa mzigo mkubwa wa madeni, Rais Samia aliyataka mataifa hayo tajiri kufikiria kutoa nafuu ya misaada na mikopo ya kifedha itakayozingatia mahitaji na changamoto zinazozikabili nchi maskini.

Alisema wakati hali ya leo hii duniani ni ile ya neema, kwa upande wa Afrika mambo yako tofauti kabisa kutokana na bara hilo kukabiliwa na changamoto za umaskini usioelezeka, njaa, lishe duni na kiwango cha chini katika uzalishaji.

Akifafanua, alisema leo hii kundi kubwa la vijana wanakabiliwa na changamoto zinazotokana na migogoro na sera za kidunia zinazochochea ongezeko la ukosefu wa usalama wa chakula, mkwamo katika ushindani, tatizo la masoko na mahitaji makubwa ya teknolojia.

“Tukiacha hali hii kama ilivyo, swali tutakalouliza mwaka 2030 halitakuwa, ‘tulishindwa kwa kiwango gani kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs)?’ bali litakuwa, ‘ni watu wangapi zaidi ambao ulimwengu umewaacha nyuma?” alisema Rais Samia na kupigiwa makofi.

Tunaamini kwamba ulimwengu wa haki, usawa, na endelevu utapatikana pale nchi zinazoendelea kama yangu (Tanzania) zitapata uungwaji wa mkono, rasilimali, na uwakilishi unaohitajika katika kufanikisha dhamira ya maendeleo endelevu.

Kauli hiyo ya Rais Samia inapata nguvu zaidi kutokana na hatua kadha za kibiashara ambazo zimekuwa zikichukuliwa na nchi za kundi la G20 ambazo zimekuwa na athari katika mwenendo wa kiuchumi na kibiashara duniani.

Taarifa zinaonyesha kwamba katika kipindi cha kati ya Oktoba 2023 hadi Oktoba 2024, nchi za G20 zilichukua mpya 91 za kuweka vikwazo vya kibiashara ikiwa ni , ongezeko la asilimia 85.7 ikilinganishwa na ripoti iliyowasilishwa kwenye mkutano wa G20 nchini India mwaka uliopita.

Takwimu zinaonyesha pia kwamba, kwa mwaka huu pekee, thamani ya biashara iliyoathiriwa na vikwazo vya nchi za kundi la G20 ilifikia dola bilioni 829, ikilinganishwa na dola bilioni 246 mwaka 2023.

Mbali ya hilo, takwimu zaidi zinaonyesha kwamba, jumla ya vikwazo vilivyopo kwa sasa vinahusisha dola trilioni 2.3, sawa na asilimia 12.7 ya uagizaji wa bidhaa za G20 na asilimia 9.4 ya uagizaji wa bidhaa kimataifa.

Pamoja na mwenendo usio sawia wa kibiashara, Rais Samia pamoja na changamoto mbalimbali, Tanzania imeweza kufanya mageuzi makubwa ya kisera na kitaasisi pamoja na kufanya uwekezaji wa kimkakati iliyosaidia kuimarisha mfumo wa kilimo cha mazao ya chakula.

Akihudhuria kikao hicho katika siku ya pili jana, Rais Samia aliungana tena na waalikwa mahususi kuhudhuria mkutano mkuu wa wakuu wa nchi na serikali wa mataifa tajiri yanayounda kundi hilo la G20.

Samia, Rais pekee kutoka eneo la ukanda wa Afrika Mashariki alihudhuria mkutano huo unaoundwa na mataifa tajiri 19 na taasisi mbili za Umoja wa Afrika (AU) na Umoja wa Ulaya (EU) kwa mwaliko wa Rais wa Brazil ambaye mbali ya kuwa mwenyeji ndiye Mwenyekiti wa G20 anayemaliza muda wake, Luiz Inácio Lula da Silva.

Samia ambaye ndiye rais pekee mwanamke Afrika na mmoja wa wakuu wawili katika mkutano huo wa G20, aliingia katika mkutano huo siku ya kwanza akiwa amevaa gauni refu jeusi kuashiria kuwapo katika kipindi cha maombolezo ya kitaifa yanayotokana na ajali ya kuporomoka kwa jengo la ghorofa katika eneo na Kariakoo Dar es Salaam, tukio lililosababisha watu 13 kupoteza maisha.

Awali, akihutubia mkutano huo siku ya kwanza, Rais Samia alimshukuru kwa dhati Rais wa Brazil Lula da Silva kwa mwaliko wake na kwa ukarimu wa kipekee kwake.

Samia ambaye hotuba yake ikivuta hamasa kubwa miongoni mwa viongozi wa kundi la G20 alieleza masikitiko yake kwa namna Afrika yenye utajiri mkubwa wa raslimali lakini ikiwa ndiyo bara linalokabiliwa na umaskini, njaa, magonjwa, utapiamlo na uzalishaji mdogo.

Leo, tuko katika ulimwengu wenye rasilimali nyingi, lakini bado Afrika inakabiliwa na viwango vya juu visivyokubalika vya umaskini, njaa, magonjwa, utapiamlo, na uzalishaji mdogo.

Alisema, licha ya changamoto mbalimbali, Tanzania imeweza kufanya mageuzi makubwa ya kisera na kitaasisi pamoja na kufanya uwekezaji wa kimkakati yaliyosaidia kuimarisha mfumo wa kilimo cha mazao ya chakula.

“Kwa kuwa asilimia 61.5 ya nguvu kazi yetu iko kwenye kilimo, juhudi zetu zimeongeza kasi ya ukuaji wa sekta hiyo hadi kufikia asilimia 4.2 na hivyo kufanikisha kiwango cha kujitosheleza kwa chakula hadi asilimia 128, na kupunguza viwango vya umaskini hadi asilimia 26.4 mwaka jana (2023), alisema.

Pamoja na mafanikio hayo, Rais alikiri kwamba katika sekta ya kilimo Tanzania inakabiliwa na changamoto ya udogo wa matumizi ya zana za kisasa katika kilimo, udogo wa matumizi ya mbolea na kukosekana kwa matokeo ya kitafiti na kimaendeleo

Rais Samia alitoa wito mahususi kwa mataifa tajiri yenye uchumi mkubwa duniani ya kundi la G20 ni kuzitengea mgawo maalum wa kifedha (SDRs) taasisi za kifedha za Afrika kama vile Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB).

Sambamba hilo, Rais Samia alisisitiza kuwpao kwa hitaji la kuwapo kwa viwango vya haki zaidi katika mgao wa hisa katika mfumo wa sasa wa kifedha wa kimataifa.

Pamoja na hayo, Rais alieleza uamuzi wa Tanzania kuunga mkono aina ya mikakati ya ushirikiano wa mataifa tajiri wa kundi la G20 kama ule Muungano wa Kidunia wa Kupambana na Njaa na Umaskini (Global Alliance Against Hunger and Poverty) ambao utaongeza ubunifu na ukuaji jumuishi.

Miongoni mwa viongozi wakuu wenye ushawishi mkubwa kimataifa waliohudhuria mkutano huo uliomalizika leo ni Rais wa Marekani anayemaliza muda wake Januari mwaka huu Joe Biden na Rais wa China Xi Jinpin.

Akifungua mkutano huo jana, Rais Lula da Silva, alizindua mkakati wa ushirikiano wa kimataifa wa kupambana na umaskini na njaa, ambao umeungwa mkono na nchi 81, akiwamo Rais Samia.

Ajenda nyingine kuu muhimu katika mkutano huo wa siku ulikuwa ni kuhusu biashara, mabadiliko ya tabianchi, na usalama wa chakula.

Akizungumzia kuhusu athari za kusikitisha za mabadiliko ya tabianchi zinazoonekana duniani, Rais Lula aliwataka viongozi wenzake kuunganisha nguvu na kuchukua hatua za kukabiliana na ongezeko la joto duniani na umaskini, ajenda ambazo kwa mujibu wa Mkakati wa Maendeleo wa Milenia (MDG) wa miaka takriban 20 iliyopita iliuanzisha.

Ushirikiano aliozindua, ukilenga kuratibu juhudi za kimataifa za kutokomeza njaa na umaskini, umeungwa mkono na Umoja wa Afrika, Umoja wa Ulaya, mashirika ya kimataifa, benki za maendeleo, na mashirika ya misaada kama Rockefeller Foundation na Bill & Melinda Gates Foundation.

“Njaa na umaskini si matokeo ya uhaba au matukio ya kiasili … ni matokeo ya maamuzi ya kisiasa,” alisema Lula, ambaye alizaliwa katika umaskini kabla ya kuingia katika siasa akipigania haki za binadamu.

Katika viunga vya jiji la Rio wafuatiliaji wa mambo wana shaka kwamba msukumo huu wa Rais Lula unaoungwa mkono pia na Rais Samia, taasisi za kifedha za kimataifa unaweza m kukutana na vikwazo kutoka kwa Rais mpya wa Marekani Donald Trump.

Tangu awasili Rio, Rais Samia ambaye alikuwa ameongozana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, Waziri na Dk. Saada Mkuya ambaye ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Zanzibar Fedha na Mipango na maofisa wengine waandamizi, amefanya mikutano ya kimikakati ya pembezoni kabla ya kuanza kwa mkutano wa G20 jana.

Wakati Samia akiandika historia ya kuwa Rais wa kwanza wa Tanzania kuhudhuria mkutano wa wakuu wa kundi la G20, jiji la Rio pia linaandika historia kubwa ya kuibua mkakati mwingine mkubwa wa ushawishi wa kimataifa ikiwa ni miaka 12 imepita tangu ufanyike mkutano ulioibuka na ajenda ya maendeleo endelevu wa SDGs.

spot_img

Latest articles

Chondechonde Polisi msisababishe wananchi wakate tamaa

ALHAMISI iliyopita yaani Desemba 5, mwaka huu wa 2024 lilitokea tukio baya la kuhuzunisha...

Ufaransa yaipatia Tanzania Sh bilioni 323.4

Na Mwandishi Wetu Serikali ya Tanzania na Shirika la Maendeleo La Ufaransa (AFD) wamesaini mikataba...

TANZANIA YAWEKA REKODI MKUTANO WA WAHASIBU WAKUU AFRIKA

Na Mwandishi Wetu Tanzania imeweka rekodi ya Mkutano wa Pili wa Wahasibu Wakuu wa Serikali...

TANZANIA KUPAMBANA NA JANGWA

Na Mwandishi wetu Serikali imejipambanua katika kupambana na kuenea kwa jangwa, kurejesha ardhi iliyoharibiwa pamoja...

More like this

Chondechonde Polisi msisababishe wananchi wakate tamaa

ALHAMISI iliyopita yaani Desemba 5, mwaka huu wa 2024 lilitokea tukio baya la kuhuzunisha...

Ufaransa yaipatia Tanzania Sh bilioni 323.4

Na Mwandishi Wetu Serikali ya Tanzania na Shirika la Maendeleo La Ufaransa (AFD) wamesaini mikataba...

TANZANIA YAWEKA REKODI MKUTANO WA WAHASIBU WAKUU AFRIKA

Na Mwandishi Wetu Tanzania imeweka rekodi ya Mkutano wa Pili wa Wahasibu Wakuu wa Serikali...