Na Mwandishi Wetu
Serikali imesema itaendelea kuwekeza katika programu za kuwawezesha vijana kupata ujuzi unaoendana na mahitaji ya soko la ajira ili kujenga nguvu kazi yenye uwezo wa kushindana ndani na nje ya nchi.
Kauli hiyo ilitolewa na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano ya Kazi), Dkt. Eveline Munisi, alipotembelea mabanda ya taasisi zilizo chini ya ofisi hiyo katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (DITF), maarufu Sabasaba.
Dkt. Munisi alisema Serikali tayari inaendelea kutekeleza programu mbalimbali za kuongeza ujuzi kwa vijana, hatua ambayo itawezesha Tanzania kuwa na wataalamu wa kutosha katika sekta mbalimbali na kupunguza utegemezi wa wataalamu kutoka nje ya nchi.

“Kadri tunavyoendelea kuwekeza katika maendeleo ya ujuzi, ndivyo tunavyojenga nguvu kazi yenye uwezo wa kukidhi mahitaji ya maendeleo ya taifa na ushindani wa soko la ajira la kisasa,” alisema.
Alieleza kuwa ameridhishwa na namna taasisi za Ofisi ya Waziri Mkuu zinavyotumia maonesho hayo kutoa elimu kwa wananchi kuhusu sheria za kazi, afya na usalama mahali pa kazi, viwango vya mishahara, haki na wajibu wa waajiri na wafanyakazi pamoja na fursa mbalimbali za ajira na mafunzo ya kuongeza ujuzi.
Alisema maonesho hayo yamekuwa jukwaa muhimu la wananchi kupata ushauri wa moja kwa moja kutoka kwa wataalamu, sambamba na kuwasilisha changamoto na kupata ufafanuzi wa masuala yanayohusu ajira na mahusiano kazini.
Dkt. Munisi pia alipongeza matumizi ya mifumo ya kidijitali katika utoaji wa huduma kwa wananchi, akisema yamerahisisha upatikanaji wa taarifa na kupunguza muda wa kupata huduma mbalimbali zinazotolewa na taasisi za Serikali.
Katika ziara hiyo alitembelea mabanda ya taasisi mbalimbali zikiwemo NSSF, WCF, OSHA, CMA na PSSSF, ambapo alieleza kuridhishwa na ubunifu na weledi unaotumika kuwahudumia wananchi.
Aidha, alisema ushirikiano mzuri kati ya Serikali, waajiri, wafanyakazi, vyama vya wafanyakazi, taasisi za dini na asasi za kiraia unaendelea kuwa msingi muhimu wa kujenga mazingira bora ya kazi na kuharakisha maendeleo ya uchumi.
Aliwataka watumishi wa taasisi hizo kuendelea kuboresha huduma kwa kutumia teknolojia na ubunifu, huku akiwahimiza wananchi kutembelea mabanda ya Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zake ili kupata elimu na huduma mbalimbali zinazotolewa wakati wa maonesho hayo.


