Na Mwandishi Wetu
MMILIKI wa Kituo cha Soka cha Bilo Jijini Mwanza, Kocha Athuman Bilal ambaye pia amewaki kuwa kocha wa timu mbalimbali nchini, Athuman Bilali maarufu Bilo, amefariki dunia huku chanzo kikiwa bado hakijafahamika.
Bilo ambaye alikuwa na mchango mkubwa katika kukuza vipaji vya soka kwa vijana. Kipindi cha uhai wake alizinoa timu mbalimbali kama vile Toto Africans, Pamba, Gwambina FC, Alliance FC, Stand United, ambapo hadi mauti yanamkuta alikuwa akimiliki timu ya soka ya wanawake inayoitwa Bilo Queens inayoshiriki Ligi Kuu Soka Wanawake Tanzania Bara.
Meneja wa timu ya Bilo Queens, Elias Mwachula amethibitisha kufariki kwa mkurugenzi wao, akisema kuwa alipewa taarifa asubuhi.
Mwachula ameeleza kama wiki mbili zilizopita alikuwa na homa lakini hali yake iliimarika na kusema kuwa taarifa hizo kifo za bosi wake zilimpa mshtuko mkubwa kwa sababu jana walikuwa wote katika mazoezi ya timu na muda mwingi waliwasiliana kutokana na maandalizi ya safari ya timu yao waliyokuwa wakifanya.
“Tumepata pigo kubwa sana kuondokewa na mkurugenzi wetu, jana nilikuwa naye asubuhi mpaka jioni tunamaliza mazoezi. Tulikuwa na mpango wa kusafiri tarehe 19 kwenda Dar es Salaam kucheza na Ruangwa,” amesema meneja huyo.


