Na Mwandishi Wetu
TAMASHA la IST Festival lililofanyika jana Februari 14, 2026 kwenye viwanja vya Fukwe za Coco jijini Dar es Salaam limekuwa jukwaa mahsusi la kuwafikia vijana na wanawake kwa kuwapatia fursa za uwezeshaji kiuchumi na elimu ya afya.
Kupitia tamasha hilo lililoandaliwa na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na Jiji la Dar es Salaam, wadau mbalimbali walitumia fursa hiyo kutoa elimu na kutangaza huduma zao.
Miongoni mwa wadhamini wakuu wa tamasha hilo ni Benki ya CRDB kupitia CRDB Bank Foundation, ambao walitumia mkusanyiko huo mkubwa wa vijana kunadi Programu za Go Green na Imbeju zinazolenga kutoa mitaji nafuu kwa vijana wenye miradi bunifu inayohusiana na kilimo, nishati na uhifadhi wa mazingira.

Akizungumza katika tamasha hilo, Meneja Mwezeshaji kutoka CRDB Bank Foundation, Shamiri Kamtu, amesema dirisha la maombi ya mikopo kupitia Programu ya Imbeju na Go Green limefunguliwa rasmi, na kwamba vijana kote nchini wanapaswa kuchangamkia fursa hiyo kabla ya Machi 11, ambayo ni mwisho wa kutuma maombi.
Amesema programu hizo zimeanzishwa kimkakati kuwainua vijana wanaojihusisha na mnyororo mzima wa thamani wa kilimo, huku zikihamasisha matumizi ya teknolojia na nishati safi rafiki kwa mazingira.
Katika hatua nyingine, kampuni tanzu ya CRDB Insurance Company ilitoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa bima na kutoa huduma za bima papo kwa papo kwa washiriki wa tamasha hilo.
Akizungumza kwa niaba ya kampuni hiyo, Omary Melele amesema wameimarisha mifumo ya ulipaji madai ili kuhakikisha wateja wanalipwa kwa wakati na kwa urahisi, akiwahamasisha Watanzania kujiwekea kinga kupitia huduma za bima.
Tamasha la IST Festival limeendelea kuwa jukwaa muhimu la kuwaunganisha vijana, kuwafungulia fursa za kiuchumi na kuwapatia elimu ya afya kwa maendeleo endelevu ya taifa.


