Sasa itoshe kuvumilia uzembe huu

WIKI iliyopita zilisambaa habari za soko jipya la kisasa la Chuini lililojengwa kwa gharama ya zaidi ya Sh. bilioni 40 huko Zanzibar kuwa linaua mitaji ya wafanyabiashara. Malalamiko yaliyotolewa na wafanyabishara wa soko hilo yanaeleza kuwa wamepoteza mitaji yao kwani wateja hawaendi kufuata mahitaji yao katika soko hilo. Huku wakilipa ushuru wa Sh. 2,000 kila siku. Soko hili lilifunguliwa na Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi Septemba 20, 2025.

Yaliyotokea Zanzibar yamekuwa ni matokeo ya kawaida mno katika miradi mingi inayojengwa kwa gharama kubwa, lakini walengwa ama hususia miradi hiyo kwa visingizio mbalimbali, kikubwa wakidai ni gharama kubwa kuendesha biashara humo ndani. Hapa jijini Dar es Salaam yapo masoko ya Bwawani na Makumbusho ambayo nayo yalijengwa kwa gharama kubwa, lakini hayana wateja. Simulizi ni hiyo, hakuna biashara. Hakuna wafanyabishara hakuna wateja!

Itakumbukwa kwamba serikali kati ya mwaka 2008 na 2010 ilijenga jengo la Machinga Complex jijini Dar es Salaam. Lilibuniwa kama suluhisho la tatizo la kuongezeka kwa wafanyabiashara wa mitaani (machinga) katika Jiji la Dar es Salaam. Malengo yake yalikuwa ni kuwahamisha maelfu ya machinga kutoka pembezoni mwa barabara na njia za waenda kwa miguu; Kupunguza msongamano katikati ya jiji; Kuwapatia wafanyabiashara maeneo rasmi na salama ya kufanyia biashara; Kuongeza mapato ya halmashauri kupitia kodi za pango na ada mbalimbali; na kuboresha mandhari, usafi na utaratibu wa kufanya biashara katika Jiji la Dar es Salaam. Mradi huu ulifadhiliwa kupitia mkopo kutoka Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), kwa gharama iliyokadiriwa kuwa kati ya Sh. bilioni 12.7 na 13.5.

Ingawa jengo lilikamilika, wengi wa walengwa waliokusudiwa kuhamia humo walichagua kubaki walikokuwa. Miaka kadhaa mpaka leo baada ya kufunguliwa, maelfu ya machinga wameendelea kufanya biashara barabarani huku sehemu kubwa ya jengo ikibaki bila kutumika ipasavyo. Baadaye likatumika kwa malengo mengine.

Mradi huo kama yalivyokuwa masoko ya Bwawani na Makumbusho katika manispaa ya Kinondoni, ulikwama. Malengo hayakutimia. Kumekuwa na maelezo mengi ya mkwamo huo. Mosi kwamba eneo halikuwa pazuri kwa biashara ya umachinga ambayo hutegemea wingi wa watu wanaopita kwa miguu. Kwa wamachinga kuhamia katika jengo la ghorofa nyingi kulimaanisha kupoteza wateja wa bahati nasibu wanaonunua bidhaa wanapopita.

Pili, kulikuwa na madai kuwa jengo halikuwa na baadhi ya huduma ambazo wafanyabiashara waliziona kuwa muhimu, kama vile maegesho ya kutosha na njia rahisi za kuwafikisha wateja na kusafirisha bidhaa kati ya ghorofa mbalimbali. Pia, baadhi ya wachambuzi walieleza kuwa wafanyabiashara hawakushirikishwa ipasavyo wakati wa kubuni mradi huo.

Tatu, kuna suala la tabia ya wateja wanaonunua kwa wamachinga ambao wanadaiwa kupendelea kununua bidhaa kutoka kwa machinga waliokuwa barabarani kwa sababu ilikuwa rahisi, haraka na yenye urahisi zaidi kuliko kuingia ndani ya jengo la ghorofa nyingi. Na nne, uhalisia wa kiuchumi wa wamachinga. Wengi hupata faida ndogo sana kwa siku. Hata gharama ndogo za pango na uendeshaji wa biashara viliwakatisha tamaa, licha ya kwamba baadaye viwango vya upangishaji vilipunguzwa.

Taarifa za kuanzishwa kwa miradi mikubwa kwa gharama kubwa ya kodi za wananchi, ikakamilika, lakini ikashindwa kutimiza lengo la kuanzishwa kwake, ni za kawaida kabisa nchini. Ndiyo maana mifano hii michache ya mwanzo mwa miaka ya 2000 na hadi hapa juzi tu, inathibitisha udhaifu mkubwa wa mchakato wa uanzishwaji wa miradi ya maendeleo. Na bado tiba haijapatikana.

Wakati miradi hii ililenga kurahisisha maisha ya wananchi katika kuzifikia huduma mahususi, pia ikilenga kusaidia kuondoa kero ya uholela wa kuendesha mambo katika miji yetu, malengo haya yamekuwa hayatimii. Imekuwa ni hasara kubwa. Imekuwa ni fadhaa kwa ujumla wake kwani wakati kuna miradi hii bado miji yetu inaendelea kushuhudia uhuria usioelezeka. Kero ya uchuuzi kila kona.

Hivi karibuni Meya wa Manispaa ya Kinondoni Songoro Mnyonge alisikika akieleza kuchoshwa kwake na uhuria usiozingatia sheria wala kanuni katika uendeshaji wa shughuli za kiuchumi katika jiji la Dar es Salaam. Kwa mfano, alihoji ni kwa nini mpaka leo eneo la Biafra Kinondoni Dar es Salaam- Manispaa ya Kinondoni, gulio linaendeshwa siku ya Jumamosi wakati mita chache tu kutoka hapo lipo soko la kisasa la Bwawani lenye huduma zote muhimu. Kibaya zaidi, wakati watu wanang’ang’ania kuendesha gulio Biafra, manispaa haipati mapato yoyote.

Kwamba ni kitu gani kinawavutia wafanyabiashara kutandaza bidhaa zao chini ambako hawana uwezo wa kudhibiti uchafu; kuzuia barabara kwa kupanga biadhaa zao kila mahali katika uholela wa kupitiliza, huku mamlaka kama Halmashauri zote za Jiji la Dar es Salaam zikinyoosha mikono? Je, ni kielelezo kwamba kwa mamlaka zimekwama kutimiza wajibu wake?

Miradi ya namna hii ipo mingi nchini. Zipo shule zimejengwa maeneo ambayo hayana wanafunzi huku mabilioni ya walipa kodi yakitumika. Ingawa kila mradi unaweza kuwa unapata changamoto zake kwa sababu mahususi, hoja kubwa ambayo imekuwa ikijirudia ni kutokushirikishwa walengwa katika hatua za awali za kubuni mradi. Ushirikishaji utaamua mradi ujengwe wapi, na mahitaji hasa ya wahusika yatabainishwa katika mchakato wa awali wa ubunifu. Utaratibu huo ungesaidia kuufanya mradi kupokewa na walengwa kwa shauku kubwa. Hali ingesaidia kutatua kero za wananchi, wakati huo huo serikali ingeongeza mapato yake.

Kukosekana kwa mikakati endelevu, shirikishi katika kuanzishwa kwa miradi ya maendeleo kwa miongo sasa imetupa majibu, lakini kwa sababu tu ya kutokujali makosa yanaendelea kujirudia.

Jaribu kufikiri aliyebuni na kujenga ile karakana ya mabasi ya mwendo kazi pale Jangwani, eneo linalojulikana wazi kabisa kwamba kila masika hujaa maji, alifanywa nini licha ya kuisababishia serikali hasara kubwa ya kuharibika kwa mabasi. Kuna madai ambayo hayajawahi kukanushwa kwamba maji yalipojaa kwenye ile karakana takribani mabasi 70 yalikufa. Hakuna yeyote aliyewajibika au kuwajibishwa kwa uzembe ule.

Ni jambo la bahati mbaya sana, miradi inajengwa, lakini malengo yake yasipotimia hakuna anayeulizwa hata kama tathmini inaonyesha wazi kulikuwa na uzembe wa dhahiri katika hatua ya kubuni mradi. Inawezekana tuna watu wasiojali katika nafasi za maamuzi, kibaya zaidi hata kama wakifanya uzembe kiasi gani hatuna cha kuwafanya. Sote tumebaki walalamikaji. Wamachinga wanalalamika, wafanyabiashara wanalalamika, wateja wanalalamika, viongozi kama meya nao wanalalamika. Anatakiwa wa kuvunja mnyororo huu wa uzembe. 

spot_img

Latest articles

CRDB yazindua msimu wa nne wa Zogo Mchongo, yasisitiza elimu ya fedha na matumizi ya teknolojia kukuza uchumi

Na Tatu Mohamed BENKI ya CRDB imezindua rasmi msimu wa nne wa kipindi cha Zogo...

WAZIRI NDEJEMBI ATOA ONYO KWA MKANDARASI ANAYETEKELEZA MRADI WA SONGEA–TUNDURU–MASASI

📌 Asema ucheleweshaji wa mradi hauendani na matarajio ya Serikali na wananchi. 📌 Amuagiza mkandarasi...

Taasisi za umma zatakiwa kuachana na utendaji wa mazoea ili kufanikisha Dira 2050

Na Mwandishi Wetu SERIKALI imezitaka Taasisi, Mashirika ya Umma na Wakala za Serikali kuachana...

NEWALA KUNUFAIKA NA UMEME WA UHAKIKA

📌*Ni baada ya kukamilika kwa njia ya kusafirisha umeme ya kilovoti 33 Masasi -...

More like this

CRDB yazindua msimu wa nne wa Zogo Mchongo, yasisitiza elimu ya fedha na matumizi ya teknolojia kukuza uchumi

Na Tatu Mohamed BENKI ya CRDB imezindua rasmi msimu wa nne wa kipindi cha Zogo...

WAZIRI NDEJEMBI ATOA ONYO KWA MKANDARASI ANAYETEKELEZA MRADI WA SONGEA–TUNDURU–MASASI

📌 Asema ucheleweshaji wa mradi hauendani na matarajio ya Serikali na wananchi. 📌 Amuagiza mkandarasi...

Taasisi za umma zatakiwa kuachana na utendaji wa mazoea ili kufanikisha Dira 2050

Na Mwandishi Wetu SERIKALI imezitaka Taasisi, Mashirika ya Umma na Wakala za Serikali kuachana...