Yajayo baada ya uchaguzi mkuu yahitaji hekima kubwa

JUMATANO ijayo, OKTOBA 29, 2025, taifa la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania linakwenda kuongeza mstari mwingine katika historia yake ya kisiasa. Ni siku ambayo Watanzania watafanya uchaguzi mkuu wa kuwachagua viongozi wao kwa nafasi ya urais, ubunge na udiwani.

Ni mstari juu ya historia ambayo ilianza kuandikwa tangu taifa hili lifanye uchaguzi wa kwanza mwaka 1960, mwaka 1965, mwaka 1970, mwaka 1975, mwaka 1980, mwaka 1985 na kisha mwaka 1990. Pia ni mfululizo wa kuongeza mstari katika siasa za ushindani nchini tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992 na kisha kufuatiwa na chaguzi nyingine sita za vyama vingi. Mwaka 1995; 2000; 2005; 2010; 2015 na 2020.

Hakuna ubishi, uchaguzi huu unakwenda kufanyika. Historia inakwenda kuandikwa, kwa sasa haijalishi ni ladha au sura gani ya uchaguzi wenyewe utakavyokuwa, ila tu kitu kimoja ni hiki: Kwamba historia inakwenda kuandikwa. Yaweza kubeba sura na ladha yoyote. Kwa hatua tuliyofikia sasa suala la uchaguzi mkuu wa 2025 siyo jambo la kujadili tena kwa sababu ni sawa na ile methali isemayo ‘maji ukiyavulia nguo, huna budi kuyaoga’. Watanzania wanakwenda kuoga.

Wanakwenda kuoga. Yawezekana maji hayo yakawa ya baridi sana, au ya moto sana au hata ya uvuguvugu. Yawezekana pia hayo maji yakawa safi sana au kinyume chake, yaani machafu. Kwa vyovyote usafi au uchafu wa maji hautaondoa ulazima wa methali ya ‘ukishayavulia maji nguo huna budi kuyaoga. Suala kuu la kujiuliza ni je, baada ya kuoga watatoka watu wa aina gani? Taifa la aina gani? Watakuwa wametakata au wamechafuka kwa kiasi gani? Ni nini kitakachofuata baada ya kuwa wameyaoga maji hayo?

Hili la ni nini kitafuata baada ya uchaguzi huu ni la msingi zaidi pengine kuliko uchaguzi wenyewe. Hili ndilo suala la kuwafikisha Watanzania, kama watu wa taifa moja. Yafaa wajiulize kwa haki ya dhamiri zao, kwamba katika kuandika historia ya taifa lao katika mchakato wa uchaguzi, je, watakuwa wamepiga hatua mbele kwa kuulinganisha uchaguzi huu na safari yao ya kisiasa kama taifa walioanza nayo baada ya kurejea kwa mfumo wa vyama vingi? Katika safari hiyo ya ushindani wa vyama katika kutafuta madaraka ya dola mwaka huu unaweza kuwapa matokeo bora zaidi ya kisiasa kuliko ilivyokuwa katika chaguzi sita zilizopita tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini?

Katika kutafakari maisha baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu, ni jambo jema pia kuangalia nyuma na kutafakari kwamba taifa limeingia katika uchaguzi huu likiwa na sura gani ya kisiasa kama taifa. Ni kweli kwa mara ya kwanza katika historia ya vyama vingi nchini, wameingia katika uchaguzi mkuu wakiwa wameparaganyika.  Mparaganyiko huu siyo mdogo. Mparaganyiko huu siyo wa kupuuzwa; na mparaganyiko huu una sababu zake.

Wapo miongoni mwa Watanzania wanaoamini kwamba kila kitu kiko sawa. Hawa wanajenga hoja kwamba kila Mtanzania anaridhika na hali ya mambo ilivyo kisiasa kwa sasa. Wajenga hoja hii wanasukumwa na mambo kadhaa kama msingi wa msimamo wao. Wanasema kwamba ni kweli mfumo wa kuendesha uchaguzi umebadilika kwa kutungwa kwa sheria mbili mpya za uchaguzi. Hizi ni sheria ya uchaguzi wa rais, wabunge na madiwani ya mwaka 2024; sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ya mwaka 2024, pia na marekebisho makubwa yamefanyika ya sheria ya vyama vya siasa ya mwaka 2024. Sheria hizi tatu, ndizo zinaweka msingi wa kisheria wa kuendesha uchaguzi mkuu kwa mwaka huu na miaka ijayo.

Kwa mantiki hiyo, wajenga hoja hii wanaamini kwamba mazingira ya kisheria na kikanuni katika kuendesha na kusimamia uchaguzi mkuu wa mwaka huu, yapo vizuri. Kwamba kuna sheria mpya za kuendesha uchaguzi, hasa hasa ikiwa imeanzishwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) ambayo ina madaraka yote ya kuendesha uchaguzi huu.

Mawazo haya ya utetezi wa kisheria na kikanuni pamoja na uimara wake, pamoja na ukweli wake, bado yamekuwa yanakumbana na ukinzani wa kifikira kutoka kwa wanaosadiki kwamba mabadiliko hayo, hayakidhi madai ya kutaka kuwapo kwa mazingira rafiki kwa shughuli za kisiasa kuendeshwa nchini bila kupendelea upande mmoja unaoshikilia madaraka. Hoja ya kundi hili, kama ilivyo ya kundi la kwanza, nayo ina mashiko yake. Mashiko yake yanapatikana katika uchambuzi wa sheria husika na jinsi ambavyo zimeshindwa kuweka uwanja sawa kwa wadau wote wa kisiasa, wanasiasa na vyama vya siasa kwa ujumla.

Ni katika hoja hiyo, baadhi ya wadau wa kisiasa wameamua kujiweka kando na uchaguzi mkuu wa mwaka huu. Kilio chao ni kimoja, hayajafanyika mabadiliko ya kimsingi ya kisheria ya kuiwezesha Tanzania kufanya uchaguzi huru na haki. Katika malalamiko hayo, yameibuka mambo mapya, makubwa na mabaya kwa sura na taathira. Kushitakiwa kwa watu katika kesi ngumu, kutekwa, kupotezwa na hata kuuawa kwa watu katika mazingira tatanishi yanayohusianishwa na siasa na uchaguzi, ni mambo yanayosumbua ndani ya jamii kwa kuwa hayapati majibu.

Matukio haya mabaya yanatamalaki katika kipindi hiki cha uchaguzi. Yanadogosha na kuchafua taswira ya uchaguzi mkuu. Mambo haya ndiyo taifa hili limeingia nayo kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu. Ni mambo ambayo yamezaa maumivu, majeraha na chuki kubwa miongoni mwa jamii.

Ukipitia mijadala mingi kwenye mitandao ya kijamii, sura hii mbaya, ya chuki, ya makasiriko, ya kukosekana upendo na mwelekeo wa kupotea kwa maelewano katika jamii, inajidhihirisha wazi. Hii siyo sura nzuri hata kidogo. Hii haiakisi hulka na desturi za Watanzania kama watu wanaozungumza bila kusagiana meno. Haionyeshi sura ya kupendeza wala kutia matumaini kwamba baada ya uchaguzi huu kupita, basi mambo yatarudi tu kuwa kawaida kama zamani bila kufanyika kwa juhudi za makusudi za kutibu haya ambayo yamepandwa na kupaliliwa ndani ya jamii kwa sasa.

Ni katika kutafakari ukweli huu tunapotafakari uchaguzi huu, ambao kwa vyovyote vile utafanyika tu, yafaa kujiuliza je, tutatoka katika uchaguzi huu tukiwa taifa moja, lenye amani, upendo, maelewano la watu wanaowahurumia wenzao? Au tunakwenda kutoka na majeraha zaidi? Ni mstari wa historia ya nanma gani unakwenda kuandikwa? Katika muktadha huu, nini majaliwa ya Watanzania katika kurejea kwenye hulka yao ya jamii isiyosagiana jino? Nani anakwenda kutibu majeraha haya? Ni katika tafakari hii kazi inayokuja baada ya uchaguzi mkuu inakwenda kuwa ngumu na nzito zaidi. Maarifa, unyenyekevu na mbinu thabiti za kiuongozi zitahitajika kuchukuliwa ili kuondoa machungu yaliyopandwa ndani ya jamii kwa kitambo sasa.

spot_img

Latest articles

Dkt. Matarajio aagiza vifaa vyote vya uhakiki wa jotoardhi Ziwa Ngozi kufika kwa wakati

Na Mwandishi Wetu NAIBU Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Dkt. James Mataragio ameliagiza Shirika...

Viongozi wa dini Kaskazini wahimiza amani kuelekea Uchaguzi Mkuu

Na Mwandishi Wetu, Moshi VIONGOZI wa dini kutoka mikoa ya kanda ya kaskazini, wamewataka Watanzania...

Zulfa Macho atinga fainali ya ngumi Zone 3 Afrika

Na Mwandishi Wetu Bondia Mtanzania Zulfa Macho amemchapa kwa pointi Bisambu Deborah wa DR Congo...

Simba kuwania tuzo ya Klabu Bora Afrika, Kapombe mchezaji bora

Na Mwandishi Wetu Klabu ya Simba imeteuliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), kuwania tuzo...

More like this

Dkt. Matarajio aagiza vifaa vyote vya uhakiki wa jotoardhi Ziwa Ngozi kufika kwa wakati

Na Mwandishi Wetu NAIBU Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Dkt. James Mataragio ameliagiza Shirika...

Viongozi wa dini Kaskazini wahimiza amani kuelekea Uchaguzi Mkuu

Na Mwandishi Wetu, Moshi VIONGOZI wa dini kutoka mikoa ya kanda ya kaskazini, wamewataka Watanzania...

Zulfa Macho atinga fainali ya ngumi Zone 3 Afrika

Na Mwandishi Wetu Bondia Mtanzania Zulfa Macho amemchapa kwa pointi Bisambu Deborah wa DR Congo...