Nani anayapa magenge ya utekaji jeuri?

KUANZIA leo Alhamisi Oktoba 16, 2025 taifa la Tanzania linahesabu siku 12 tu kufikia tarehe ya kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani. Uchaguzi huu unatarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025. Kwa kitambo sasa kumekuwa na hekaheka nyingi za wagombea wa nafasi hizo tatu kusaka kura kutoka kwa wananchi.

Ukipita kila kona ya nchi, mabango ya kujitambulisha na kuomba kura yametamalaki. Kila barabara kuu katika miji yote ya Tanzania imebandikwa mabango haya. Makubwa kwa madogo. Misafara, mikutano ya kampeni na matangazo ya kunadi sera na kujitangaza kwa wagombea, navyo vimekuwa ni matukio ya kila uchao tangu kuzinduliwa kwa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka huu mwishoni mwa Agosti mwaka huu.

Kwa kawaida, kipindi cha uchaguzi mkuu ni wakati wa watu kuwa na uhuru wa kusema na kutoa maoni yao juu ya masuala ya kisiasa. Mijadala na kauli hizi ni ama za kukosoa sera zinazotangazwa na wagombea na vyama vyao, au hata kukumbusha ni wapi waliopewa madaraka kwa muda unaokwisha walitekeleza wajibu wao kulingana na ilani waliyotoa. Kadhalika, ni wakati wa kuonyesha ni nini hakikutekelezwa. Kwa ujumla ni wakati wa kutafuta kuungwa mkono na wananchi ili kupata ridhaa yao ya kukalia ofisi ya umma kuanzia ngazi ya udiwani, ubunge hadi urais.

Hata hivyo, wakati taifa likiwa katika uhuru wa namna hii, katika hali ya uchaguzi, bado hofu ya wasiojulikana imeendelea kutamalaki nchini. Kwa bahati mbaya, nguvu, mashambulizi na hasira za wasiojulikana zinaonekana kuelekezwa kwa wale wenye maoni tofauti na wenye mamlaka kuhusu uchaguzi. Kuna madai ya matukio mengi ya watu kuvamiwa, kutekwa na kupotezwa. Kwa bahati mbaya, kama ambavyo sasa inaelekea kuwa kawaida au tuseme utamaduni, kila anayetekwa, kuvamiwa kupotezwa, hakuna taarifa zozote zinapatikana juu ya waliko. Kwanza, watekaji mpaka leo umma unaambiwa kuwa ni watu wasiojulikana; pili, vyombo vyenye dhima ya kuchunguza na kutoa majibu ya kueleweka kwa umma juu ya uhalifu huu, havijaweza kuwafikia siyo watekaji tu, bali hata waliotekwa pia.

Ni kwa kutambua hali hii, Askofu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam la Kanisa Katoliki, Juda Thadeus Ruwa’ichi akitoa tamko la Tume ya Haki na Amani ya Baraza Kuu la Maaskofu Tanzania wakati wa kuadhimisha Misa Takatifu ya Hija – Umoja wa Wanaume Wakatoliki (UWAKA) Kutegemeza Msista wa Shirika la Dada Wadogo iliyofanyika Visiga, Pwani, aliuliza ni kwa nini utekaji unaendelea nchini? Aliuliza ni kwa nini wenye mamlaka wameshindwa kuwa na moyo na uwezo wa kuwashinda watekaji na wauaji?

Katika misa hiyo iliyofanyika siku ya kumbukumbu ya kifo cha Baba wa taifa Mwalimu Nyerere, Askofu Ruwa’ichi aliuliza ni kwa nini waliotekwa au kupotea hawako mahabusu? Hali hii ya kutokuonekana kabisa kwa watu waliotekwa au kupotea au kupotezwa, kunaibua maswali mengi ambayo yanasumbua jamii. Haya ni je, ni kweli vyombo vya ulinzi na usalama vimeshindwa kabisa kujua watekaji ni akina nani, wako wapi na ni nani anawapa kiburi hicho?

Ni dhahiri, hivi ni vikundi vya kiuhalifu. Ni magenge ya watu. Siyo vikosi rasmi vya ulinzi na usalama vya taifa hili. Inaaminika hivyo kwa sababu, mtindo, aina na mbinu zao za kuteka watu, kuwapoteza kiasi cha kutokuonekana tena, siyo utaratibu wa kisheria wa vyombo vya ulinzi na usalama vya kushughulika na tuhuma za uhalifu nchini.

Jeshi la Polisi lenye dhima ya kupeleleza matukio yote ya uvunjaji wa sheria na uhalifu mwingine wowote, lina utaratibu ulioainishwa kisheria, kwamba mtuhumiwa atakamatwa vipi na atahifadhiwa wapi. Kiutaratibu, Jeshi la Polisi haliruhusiwi kumkamata mtuhumiwa yeyote wa uhalifu wowote kinyemela na kumshikilia bila ndugu au wakili wa mtuhumiwa kujulishwa.

Ni kwa matinki hiyo, hawa wanaofanya vitendo hivi ni magenge ya kihalifu. Ni vikundi vya watu ambavyo havina mamlaka yoyote ya kisheria kufanya hayo wanayofanya. Kwa kifupi matukio yote ya utekaji, kupotea kwa watu na hata kuuawa yanafanywa na watu ambao kisheria hawana mamlaka ya kuyafanya hivyo- nao ni  wahalifu.

Katika mazingira hayo, ni kwa nini vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vimeshindwa kuwajua? Vimeshindwa kuwapa wananchi taarifa sahihi juu ya vikundi hivi? Vinafanya uhalifu huu vikitokea wapi ambako haviwezi kujulikana? Vinapata wapi jeuri na kiburi chote hiki cha kujichukuliwa sheria mkononi? Kila taarifa inayotolewa na polisi juu ya matukio haya – utekaji upotezaji wa watu, wanakiri kwamba hawawajui na kwamba wanaendelea na uchunguzi. Uchunguzi huu umekuwa unaendelea kwa matukio mengi sana, lakini ni nadra sana kusikia umma ukijulishwa hatma ya upelelezi huo.

Ni katika kutafakari matukio haya, hasa yanapokuwa yanaendelea kutokea katika kipindi hiki cha uchaguzi hasa yanapowalenga wenye mawazo mbadala na ya watawala, tunajiuliza ni nani hasa mnufaika wa uhalifu huu? Serikali haiwezi kufurahia raia wake kutekwa na kupotezwa, kwa sababu ina taratibu za kisheria na vyombo vilivyoundwa kisheria kushughulika na uhalifu. Serikali ina Jeshi la Polisi, ina Jeshi la Magereza, ina Idara ya Usalama wa Taifa, ina Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), ina Idara ya Uhamiaji na vyombo vingine, vyote hivi vinafanya kazi zake kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu zilizo wazi kabisa. Asilani, utekaji wa raia, mauaji ya raia, upotezaji wa raia, siyo moja ya majukumu ya vyombo hivi vya ulinzi na usalama. Siyo kabisa.

Sasa hawa wanaoendesha matendo haya wanatoka wapi? Ni kwa nini kwa miaka kadhaa sasa imeshindikana kabisa kuwajua, kuwakamata na kukomesha vitendo hivi vinavyozidi kujenga hofu na chuki ndani ya jamii? Nani hasa ni mnufaika wa matendo ya magenge haya? Ni fedheha magenge ya uhalifu kuachwa tu yajifanyie uhalifu wao katika nchi ambayo miaka yote imetambuliwa kuwa ni ya amani na yenye mifumo ya wazi kabisa ya kushughulika na matendo ya kihalifu, yawe ya magenge au ya mtu mmoja mmoja. Ni kwa nini imeshindikana kuyadhibiti magenge haya? Yanapata wapi jeuri ya kufanya yote haya?

spot_img

Latest articles

Dkt. Matarajio aagiza vifaa vyote vya uhakiki wa jotoardhi Ziwa Ngozi kufika kwa wakati

Na Mwandishi Wetu NAIBU Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Dkt. James Mataragio ameliagiza Shirika...

Viongozi wa dini Kaskazini wahimiza amani kuelekea Uchaguzi Mkuu

Na Mwandishi Wetu, Moshi VIONGOZI wa dini kutoka mikoa ya kanda ya kaskazini, wamewataka Watanzania...

Zulfa Macho atinga fainali ya ngumi Zone 3 Afrika

Na Mwandishi Wetu Bondia Mtanzania Zulfa Macho amemchapa kwa pointi Bisambu Deborah wa DR Congo...

Simba kuwania tuzo ya Klabu Bora Afrika, Kapombe mchezaji bora

Na Mwandishi Wetu Klabu ya Simba imeteuliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), kuwania tuzo...

More like this

Dkt. Matarajio aagiza vifaa vyote vya uhakiki wa jotoardhi Ziwa Ngozi kufika kwa wakati

Na Mwandishi Wetu NAIBU Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Dkt. James Mataragio ameliagiza Shirika...

Viongozi wa dini Kaskazini wahimiza amani kuelekea Uchaguzi Mkuu

Na Mwandishi Wetu, Moshi VIONGOZI wa dini kutoka mikoa ya kanda ya kaskazini, wamewataka Watanzania...

Zulfa Macho atinga fainali ya ngumi Zone 3 Afrika

Na Mwandishi Wetu Bondia Mtanzania Zulfa Macho amemchapa kwa pointi Bisambu Deborah wa DR Congo...