Na Mwandishi Wetu
AHADI ya Serikali ya kufikisha umeme wa gridi ya taifa katika Wilaya zote za Mkoa wa Kagera imetekelezwa baada ya Serikali kusaini mikataba ya ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 220 kutoka Benako, Ngara hadi Kyaka wilayani Misenyi na kituo cha kupoza umeme cha Benako cha msongo wa kilovoti 220/33.
Hatua hiyo inayotoa uhakika kwa Mkoa huo kupata umeme wa gridi badala ya kutegemea umeme kutoka Uganda kwa kiasi kikubwa.

Akizungumza baada ya kushuhudia utiaji saini kwa mikataba hiyo jijini Dodoma tarehe 25 Agosti, 2025, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amesema kuwa kuanza kutekelezwa kwa mradi huo ni moja ya maelekezo ya Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye alikuwa na kiu ya kutekeleza ahadi ya Serikali kwa wananchi wa Kagera ya kupata umeme wa uhakika muda wote ili kutekeleza shughuli zao za kiuchumi na kijamii.
“Kupitia mradi huu, Mkoa wa Kagera kwa mara ya kwanza na wenyewe unaingia kwenye gridi ya Taifa hasa na hivyo kuongeza uhakika wa upatikanaji wa umeme hususan katika Wilaya za Bukoba, Muleba, Misenyi, Karagwe, Kyerwa na maeneo mengine ya jirani, nawahakikishia watu wa Kagera kuwa Serikali imeshaamua mradi huu ufanyike kwa wakati kwa miezi 24 tu,” amesema Dkt. Biteko.

Ameongeza kuwa, Kagera ambayo mahitaji yake ya umeme hayazidi megawati 47 baada ya muda itakuwa na uhakika mkubwa wa upatikanaji umeme kwani kutakuwa na njia mbalimbali za kufikisha umeme mkoani humo ikiwemo Benako- Karagwe hadi Kayaka, Nyakanazi- Biharamulo hadi Muleba na kuna mradi mwingine mkubwa unaotarajiwa kujengwa kutoka Ibadakuli hadi Mbarara Uganda wa kV 400.
#Vilevile kuna mradi wa uzalishaji umeme wa Kakono wa megawati 87 ambao upo katika hatua za mwisho za kutafuta Mkandarasi,” amesema
Amebainisha kuwa, Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan pia anaendelea kutekeleza miradi mingine ya umeme katika maeneo mengine ikiwemo mradi wa usafirishaji umeme wa kV 400 wa Tanzania- Zambia, mradi wa Usafirishaji umeme wa kV 400 Chalinze-Dodoma , mradi wa usafirishaji umeme wa Mkuranga -Pwani ambao utapeleka umeme kwa wananchi wa Kusini, pia mradi wa usafirishaji umeme wa gridi imara wa Tunduru- Masasi- Mahumbika ambao pia unaenda kutoa uhakika wa umeme katika mikoa ya Kusini.
“Utekelezaji wa miradi hii yote ya umeme ni kielelezo kuwa, Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshaonesha njia ya kuwafikishia wananchi umeme wa uhakika sasa kinachohitajika kwa watendaji ni kukimbia badala ya kutembea kwani kinachotakiwa ni matokeo na siyo kusema sana.” Amesisitiza Dkt. Biteko.
Pia amewashukuru wafadhili wa mradi ambao wametoa Dola za Kimarekani takriban milioni 105.6 ambazo ameagiza kuwa zitumike kwa usahihi ili kuwapa sababu wafadhili wengine kuendelea kusaidia miradi mbalimbali.
Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko ameagiza TANESCO kuhakikisha wananchi 1,014 wanaopisha mradi wanalipwa fidia yao mapema iwezekanavyo yaani kuanzia mwezi septemba mwaka huu.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatuma Mwassa amepongeza Serikali kwa kuona umuhimu wa kutekekeza mradi huo wenye gharama kubwa ikiwa ni kuonesha kwa vitendo jinsi inavyowajali wananchi hao.
Amesema wilaya zote mkoani Kagera zitaunganishwa na gridi kwani kwa sasa no wilaya tatu tu ndio zimeunganishwa na Gridi ya Taifa.Ameahidi kuwa, Wananchi katika mkoa huo watakuwa watumiaji wazuri wa umeme na walipaji bili wazuri iili TANESCO iendelee kupata mapato ya kutekeleza miradi mingine
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba amesema Mkoa wa Kagera ni miongoni mwa mikoa minne ambayo haijaunganishwa kwenye gridi ya Taifa ikiwemo Rukwa, Lindi na Mtwara.
Amesema kwa sasa Mkoa wa Kagera unapata umeme wa megawati 40 kutoka nchini Uganda kupitia kituo cha Kyaka na megawati 7 kutoka mwekezaji binafsi wa mradi wa Mirongo/ Kikagati.
Awali Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania ( TANZANIA), Lazaro Twange mradi huo una umuhimu mkubwa mkoani Kagera kwani wilaya za Kyerwa, Karagwe, Misenyi, Muleba, Bukoba Vijijini na Manispaa ya Bukoba kwa muda mrefu zimekuwa zikiitumia umeme kutoka nchini Uganda.