UZALISHAJI GESI ASILIA WAFIKIA FUTI ZA UJAZO BILIONI 65.4, PURA YAOKOA SH BILIONI 8.86

Na Tatu Mohamed

UZALISHAJI wa gesi asilia nchini umeongezeka na kufikia futi za ujazo bilioni 65.4 katika mwaka wa fedha 2025/2026, kutoka futi za ujazo bilioni 62.6 zilizozalishwa mwaka 2024/ 2025, huku Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) ikiokoa Dola za Marekani milioni 3.3, sawa na takribani Sh bilioni 8.86 kupitia ukaguzi wa gharama na mapato katika mikataba ya uzalishaji na ugawanaji mapato.

Mafanikio hayo yametokana na kuongezeka kwa shughuli za uzalishaji na utafutaji wa gesi asilia katika vitalu mbalimbali nchini, sambamba na kuongezeka kwa mahitaji ya nishati hiyo, hususan viwandani na kwenye magari yanayotumia Gesi Asilia Iliyoshindiliwa (CNG).

Akizungumza katika mkutano na wahariri wakuu wa vyombo vya habari ulioandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina jijini Dar es Salaam, leo Novemba 23, 2026, Mkurugenzi Mkuu wa PURA, Mhandisi Charles Sangweni, amesema ongezeko hilo linaonesha kuimarika kwa shughuli za uzalishaji wa gesi asilia nchini.

Amesema katika kitalu cha Mnazi Bay kilichopo mkoani Mtwara, PURA ilisimamia uchimbaji wa visima vitatu vya gesi asilia vilivyokamilika kwa mafanikio.Amevitaja visima viwili vya uzalishaji kuwa ni Mnazi Bay Five (MB-5) na Msimbati Two (MS-2), ambavyo tayari vimeanza uzalishaji vikiwa na uwezo wa kuzalisha wastani wa futi za ujazo milioni 40 na milioni 50 kwa siku, mtawalia.

Aidha, amesema uchimbaji wa kisima cha utafutaji cha Kasa One X (Kasa-1X) umefanikisha ugunduzi wa gesi asilia inayokadiriwa kuwa na kiasi cha futi za ujazo bilioni 223.Kuhusu kitalu cha Ruvuma, amesema maandalizi ya uchimbaji wa kisima cha Chikumbi-1 (CH-1), ukarabati wa kisima cha Ntorya-1 (NT-1) na majaribio ya uzalishaji katika kisima cha Ntorya-2 (NT-2) yanaendelea.

Katika hatua nyingine, amesema tafsiri mpya ya data za mitetemo za 3D katika kitalu cha Tanga imebaini maeneo matatu yenye viashiria vya uwepo wa mafuta, huku uchimbaji wa kisima cha utafutaji katika maeneo hayo ukitarajiwa kufanyika mwaka 2027.

Ameongeza kuwa katika eneo la Eyasi-Wembere, ukusanyaji wa data za mitetemo za 2D ulikuwa umefikia asilimia 99, sawa na kilomita 772 kati ya kilomita 779, hadi Juni 30, 2026, wakati eneo la Lindi-Mtwara ukusanyaji wa data za mitetemo za 3D ulikuwa umefikia asilimia 35.

Katika kuimarisha ushiriki wa Watanzania katika sekta hiyo, Sangweni amesema thamani ya bidhaa na huduma zilizotolewa na kampuni za ndani katika miradi ya mkondo wa juu wa petroli imeongezeka kutoka Dola za Marekani milioni 14 mwaka 2025 hadi zaidi ya Dola milioni 30 mwaka 2026.

Amesema PURA pia imesimamia utekelezaji wa miradi ya uwajibikaji kwa jamii (CSR), ikiwemo ujenzi wa Shule ya Msingi Likong’o katika Halmashauri ya Manispaa ya Lindi, ujenzi wa majiko ya kisasa yanayotumia gesi ya LPG katika shule nne za Kata ya Msimbati, mkoani Mtwara, pamoja na ufadhili wa vijana kupata mafunzo ya ufundi katika Chuo cha Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) mkoani Lindi.

Akifafanua kuhusu fedha zilizookolewa, amesema kiasi cha Dola za Marekani 3,306,678 kilipatikana kupitia ukaguzi wa gharama na mapato katika kitalu cha Songo Songo, vitalu namba 1 na 4 kwa kipindi cha mwaka 2023 hadi 2024, pamoja na kitalu cha Ruvuma, hatua iliyowezesha fedha hizo kurejeshwa katika fungu la ugawanaji wa mapato.

Kwa upande wake, mwakilishi wa Ofisi ya Msajili wa Hazina, Sabato Kusuri, amesema sekta ya mafuta na gesi ina nafasi kubwa katika kujenga uchumi wa taifa na kwamba ni muhimu kuipa kipaumbele kinachostahili kutokana na fursa za uwekezaji, ajira na mapato inayoweza kuzalisha.

Amewataka wahariri na waandishi wa habari kuongeza taarifa na uchambuzi kuhusu sekta hiyo, kuelimisha umma kuhusu fursa zilizopo na kueleza mchango wake katika uchumi wa nchi.

Amesema Ofisi ya Msajili wa Hazina itaendelea kuandaa majukwaa ya majadiliano kati ya taasisi na mashirika ya umma pamoja na vyombo vya habari ili kuimarisha mawasiliano, uelewa na ushiriki wa wananchi katika masuala ya maendeleo ya taifa.

Naye mwakilishi wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Stella Brown amesema mafunzo na mikutano ya aina hiyo ni muhimu katika kuongeza uelewa wa wahariri kuhusu sekta ya mafuta na gesi, ili waweze kupeleka elimu sahihi kwa wananchi.

Amesema jamii bado ina uelewa mdogo kuhusu shughuli za utafutaji na uzalishaji wa gesi asilia, hivyo vyombo vya habari vina wajibu wa kuongeza elimu kwa umma kuhusu rasilimali hiyo na fursa zinazotokana nayo.

spot_img

Latest articles

MIRADI YA KUIMARISHA UPATIKANAJI WA UMEME DAR ES SALAAM YAFIKIA HATUA ZA MWISHO KUKAMILIKA – MD TWANGE

📌Serikali yawekeza zaidi ya bilioni 193 kuimarisha upatikanaji wa umeme Dar kukidhi ongezeko la...

RAIS SAMIA KUFUNGUA MKUTANO MKUU WA TUME ZA UCHAGUZI ECF-SADC

Na Mwandishi Wetu RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan...

NESCH MINTEC YAPUNGUZA GHARAMA ZA VIPIMO VYA MADINI KUPITIA MAABARA YA MWANZA

Na Mwandishi Wetu WACHIMBAJI na wafanyabiashara wa madini nchini sasa wana fursa ya kupata...

OTR na IMF zajadili utendaji wa taasisi za umma

Na Mwandishi Wetu MSAJILI wa Hazina, Nehemiah Mchechu, amekutana na ujumbe wa Shirika la Fedha...

More like this

MIRADI YA KUIMARISHA UPATIKANAJI WA UMEME DAR ES SALAAM YAFIKIA HATUA ZA MWISHO KUKAMILIKA – MD TWANGE

📌Serikali yawekeza zaidi ya bilioni 193 kuimarisha upatikanaji wa umeme Dar kukidhi ongezeko la...

RAIS SAMIA KUFUNGUA MKUTANO MKUU WA TUME ZA UCHAGUZI ECF-SADC

Na Mwandishi Wetu RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan...

NESCH MINTEC YAPUNGUZA GHARAMA ZA VIPIMO VYA MADINI KUPITIA MAABARA YA MWANZA

Na Mwandishi Wetu WACHIMBAJI na wafanyabiashara wa madini nchini sasa wana fursa ya kupata...