Na Mwandishi Wetu
WACHIMBAJI na wafanyabiashara wa madini nchini sasa wana fursa ya kupata huduma za vipimo vya madini kwa viwango vya kimataifa kupitia maabara ya Nesch Mintec iliyopo jijini Mwanza, hatua inayolenga kupunguza gharama na muda wa kusubiri matokeo ya vipimo.
Akizungumza katika maonyesho ya sekta ya madini, Mkurugenzi wa Nesch Mintec, Happiness Nesvinga, amesema awali wadau wengi walilazimika kusafirisha sampuli za madini kwenda nje ya nchi kwa ajili ya vipimo, hali iliyosababisha gharama kubwa na kuchelewesha upatikanaji wa majibu.
Amesema maabara hiyo yenye ithibati ya kimataifa (International Accreditation) inatoa fursa kwa wadau kupata huduma za upimaji ndani ya nchi bila gharama za ziada za kusafirisha sampuli nje ya Tanzania.

Nesvinga ameeleza kuwa vipimo sahihi ni msingi wa usalama wa biashara ya madini, kwani humwezesha mchimbaji au mfanyabiashara kufanya maamuzi sahihi kuhusu uzalishaji na biashara yake.
Aidha, ameishukuru Serikali kwa kuandaa maonyesho yanayowakutanisha wadau mbalimbali, akisema jukwaa hilo linaongeza uelewa kuhusu huduma zinazopatikana nchini na kujenga mazingira rafiki kwa uwekezaji katika sekta ya madini.


