Na Mwandishi Wetu
MSAJILI wa Hazina, Nehemiah Mchechu, amekutana na ujumbe wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) ukiongozwa na Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Afrika ya shirika hilo, Nicolas Blancher, na kujadili mageuzi yanayotekelezwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina (OTR) katika kuimarisha utendaji wa kifedha, uwajibikaji na uendelevu wa taasisi za umma.
Katika kikao hicho kilichofanyika Jumatano, Bw. Mchechu aliueleza ujumbe huo kuhusu maendeleo ya utendaji wa taasisi na kampuni zilizo chini ya usimamizi wa OTR, hatua za kupunguza utegemezi wa fedha za Serikali na mikakati ya kuongeza mchango wa uwekezaji wa umma katika uchumi wa taifa.
Ziara hiyo ilikuwa sehemu ya utaratibu wa kawaida wa IMF wa kufanya tathmini ya mwenendo wa uchumi na sera za nchi wanachama, kufuatia kukamilika kwa Programu ya Upanuzi wa Mikopo (ECF) na Programu ya Ustahimilivu na Uendelevu (RSF) Agosti 17, 2026.
Akiwasilisha mwenendo wa utendaji wa taasisi na kampuni zilizo chini ya usimamizi wa OTR, Bw. Mchechu alisema matokeo halisi ya kifedha ya taasisi za umma kwa pamoja yaliongezeka hadi Sh1.222 trilioni katika mwaka wa fedha 2024/25, kutoka Sh552 bilioni mwaka 2023/24.

Kuimarika kwa matokeo hayo kuliambatana na kupungua kwa idadi ya kampuni za kibiashara zilizopata hasara kutoka 12 hadi saba kati ya miaka ya fedha 2023/24 na 2024/25.
Aidha, makusanyo ya mapato yasiyo ya kodi ya OTR kutoka katika taasisi za umma na kampuni ambazo Serikali ina hisa chache yaliongezeka hadi Sh1.327 trilioni mwaka 2025/26, kutoka Sh1.0286 trilioni mwaka 2024/25.
Akizungumzia ufadhili wa Serikali kwa taasisi na kampuni za umma, Bw. Mchechu alisema taasisi 13 muhimu zilipokea ruzuku ya jumla ya Sh3 trilioni mwaka 2024/25, ikilinganishwa na Sh3.68 trilioni mwaka 2023/24.

Alieleza kuwa OTR inaendelea kusimamia mkakati wa kupunguza utegemezi wa fedha za Serikali katika matumizi ya kawaida, huku ikiendeleza uwekezaji katika miradi ya kimkakati, hususan miundombinu mikubwa.
Lengo ni kuimarisha uwezo wa kibiashara wa taasisi hizo ili ziweze kugharamia sehemu kubwa zaidi ya shughuli zake kwa kutumia mapato yao ya ndani.Katika kuimarisha uwazi, alibainisha kuwa OTR inaendelea kukusanya na kuunganisha taarifa za hesabu zilizokaguliwa za taasisi na kampuni zilizo katika usimamizi wake na kuzichapisha kwenye tovuti ya Ofisi hiyo, ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa za kifedha kwa umma na wadau wengine.
Kwa sasa, OTR inasimamia taasisi na kampuni 308, ambapo 252 Serikali ina hisa nyingi na 56 ina hisa chache.
Kwa upande wake, Bw. Blancher alitaka kufahamu hatua iliyofikiwa katika pendekezo la kuanzisha Mfuko wa Uwekezaji wa Umma.

Akifafanua kuhusu pendekezo hilo, Bw. Mchechu alisema bado linazingatiwa na Serikali na linalenga kuweka utaratibu maalumu wa kusaidia taasisi na kampuni za umma zenye uwezo wa kujiendesha kibiashara pamoja na uwekezaji wa kimkakati.
Alisisitiza kuwa mfuko huo haukusudii kutoa fedha moja kwa moja kwa kila taasisi ya umma, bali kuwezesha Serikali kutathmini na kupanga vipaumbele vya mahitaji ya mitaji kwa kuzingatia matokeo ya utendaji, umuhimu wa kimkakati na mahitaji ya uwekezaji ya kila taasisi.
Kikao hicho pia kilijadili fursa za kuongeza ushiriki wa sekta binafsi katika kampuni za umma kupitia uuzaji wa hisa katika masoko ya mitaji, ubia wa kimkakati na mifumo mingine ya uwekezaji.
Mchechu alisema OTR inafanya tathmini ya taasisi zilizo katika usimamizi wake ili kubaini zile zilizo tayari kuvutia wawekezaji kwa sasa, zinazohitaji maandalizi ya muda wa kati na zile zenye fursa za uwekezaji katika muda mrefu.


