MAAMBUKIZI MAPYA YA VVU YAPUNGUA KUTOKA 98,754 HADI 33,511

Na Tatu Mohamed

MAAMBUKIZI mapya ya Virusi vya Ukimwi (VVU) nchini yamepungua kutoka watu 98,754 mwaka 2010 hadi 33,511 mwaka 2025, huku wasichana wenye umri wa miaka 15 hadi 24 wakichangia asilimia 77.7 ya maambukizi mapya yanayotokea katika kundi hilo la vijana.

Vijana wa umri huo wanachangia asilimia 33.3 ya maambukizi yote mapya nchini, hali inayodhihirisha umuhimu wa kuimarisha mikakati ya kinga, upimaji na utoaji wa elimu sahihi, hususan kwa wasichana.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Prof. Palamagamba Kabudi, ametoa takwimu hizo leo Novemba 19, 2026, jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani yatakayofanyika Desemba Mosi mwaka huu.

Prof. Kabudi amesema takwimu za maambukizi kwa vijana zinapaswa kuwa changamoto kwa Serikali, jamii na wadau wote kuongeza juhudi za kuwafikia kwa elimu sahihi na huduma za kinga ili kupunguza maambukizi mapya.

“Pia, ninatoa wito kwa kila mmoja wetu, hususan vijana, kuwajibika katika kujikinga na VVU, kujua hali yake ya VVU na kushiriki katika kutoa elimu sahihi kwa jamii,” amesema.

Amesema Serikali ina dhamira ya kuhakikisha hakuna mwananchi anayeachwa nyuma katika mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI, kwa lengo la kutokomeza ugonjwa huo kama tishio la afya ya umma ifikapo mwaka 2030.

Ameongeza kuwa katika kipindi cha mwaka 2010 hadi 2025, vifo vitokanavyo na UKIMWI vilipungua kutoka watu 55,833 hadi 25,995, huku maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto yakishuka kutoka asilimia 9.1 hadi asilimia 6.2.

“Kwa mujibu wa takwimu za mfumo wa taarifa za afya wa DHIS-2 hadi Desemba 2025, asilimia 92.7 ya watu wanaoishi na VVU walikuwa wamepima na kujua hali zao za maambukizi.

“Aidha, asilimia 99.5 ya waliofahamu hali zao walikuwa wakipata huduma za dawa za kupunguza makali ya VVU (ARV), huku asilimia 98.2 ya waliokuwa kwenye matibabu wakiwa wamefubaza virusi mwilini,” amesema.

Amefafanua kuwa, mafanikio hayo yanaonesha hatua iliyopigwa na Tanzania katika kufikia malengo ya kimataifa ya 95-95-95, yanayolenga kuhakikisha asilimia 95 ya watu wanaoishi na VVU wanajua hali zao, asilimia 95 ya wanaojua hali zao wanapata matibabu na asilimia 95 ya wanaotumia dawa wanafubaza virusi mwilini

.Katika hatua nyingine, amesema Serikali inaendelea kuimarisha mifumo endelevu ya kugharamia mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI kwa kuongeza uwekezaji wa rasilimali za ndani, kuhamasisha sekta binafsi kushiriki na kuendeleza ushirikiano na wadau wa maendeleo.

Amesema hatua hiyo ni muhimu kuhakikisha mabadiliko ya mazingira ya ufadhili wa kimataifa hayaathiri upatikanaji na mwendelezo wa huduma za kinga, upimaji na matibabu kwa wananchi.

Vilevile, amesisitiza umuhimu wa kuondoa unyanyapaa na ubaguzi dhidi ya watu wanaoishi na VVU, akiwataka Watanzania kuwapa nafasi ya kuishi kwa utu na kushiriki katika maendeleo ya Taifa.

“Napenda kuwasisitiza Watanzania kuwa tusimnyanyapae wala kumbagua mtu anayeishi na VVU,” amesema.

Akizungumzia maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani mwaka huu, Prof. Kabudi amesema shughuli za uhamasishaji, utoaji wa elimu na huduma za afya zitafanyika kuanzia Novemba 24 hadi Desemba Mosi katika kanda saba za Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS).

Amezitaja kanda hizo kuwa ni Mashariki, Kati, Ziwa, Kusini, Nyanda za Juu Kusini, Magharibi na Kaskazini, ambako Mawaziri na Naibu Mawaziri watashiriki katika shughuli hizo kwa utaratibu maalumu.

“Maadhimisho ya kitaifa yatafanyika kuanzia Novemba 29 katika ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Centre jijini Dodoma na kuhitimishwa Desemba Mosi, ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba,” amesema.

Maadhimisho hayo yataambatana na kumbukumbu ya miaka 25 tangu kuanzishwa kwa TACAIDS mwaka 2001, pamoja na maonesho ya wadau yatakayolenga kuonesha mafanikio yaliyopatikana katika mapambano dhidi ya UKIMWI.Kaulimbiu ya mwaka huu ni “Huduma Bora za Afya ni Msingi wa Kutokomeza UKIMWI, Tuendelee Kuimarisha Upatikanaji.”

spot_img

Latest articles

MRADI WA UPANUZI WA KITUO CHA KUPOZA UMEME DEGE KUIMARISHA HALI YA UPATIKANAJI WA UMEME KIGAMBONI

📌Wafikia Asilimia 90 katika utekelezaji wake 📌 Kukamilika Mwisho wa Mwezi Disemba 2026 Na Mwandishi Wetu...

GBT yaikaribisha BetSasa sokoni, yaitaka kuzingatia maadili

Na Mwandishi Wetu MKURUGENZI Mkuu wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha (GBT), James Mbalwe ameikaribisha...

DKT. YONAZI AHIMIZA UIMARISHWAJI WA MIFUMO YA KITAASISI YA UFUATILIAJI NA TATHMINI NCHINI

Na Mwandishi Wetu- Morogoro. KATIBU Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge Uratibu na Wenye...

OTR, Benki ya Dunia zajadili fursa za uwekezaji katika taasisi za umma

Na Mwandishi Wetu OFISI ya Msajili wa Hazina (OTR) na Benki ya Dunia zimeonesha nia...

More like this

MRADI WA UPANUZI WA KITUO CHA KUPOZA UMEME DEGE KUIMARISHA HALI YA UPATIKANAJI WA UMEME KIGAMBONI

📌Wafikia Asilimia 90 katika utekelezaji wake 📌 Kukamilika Mwisho wa Mwezi Disemba 2026 Na Mwandishi Wetu...

GBT yaikaribisha BetSasa sokoni, yaitaka kuzingatia maadili

Na Mwandishi Wetu MKURUGENZI Mkuu wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha (GBT), James Mbalwe ameikaribisha...

DKT. YONAZI AHIMIZA UIMARISHWAJI WA MIFUMO YA KITAASISI YA UFUATILIAJI NA TATHMINI NCHINI

Na Mwandishi Wetu- Morogoro. KATIBU Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge Uratibu na Wenye...