MIRADI YA KUIMARISHA UPATIKANAJI WA UMEME DAR ES SALAAM YAFIKIA HATUA ZA MWISHO KUKAMILIKA – MD TWANGE

📌Serikali yawekeza zaidi ya bilioni 193 kuimarisha upatikanaji wa umeme Dar kukidhi ongezeko la mahitaji ya kiuchumi na kijamii

📌 Miradi inayotekelezwa inalenga kuongeza uwezo wa kusafirisha umeme kutoka vituo vya uzalishaji hadi kwa watumiaji

Na Mwandishi Wetu

MKURUGENZI Mtendaji wa TANESCO, Lazaro Twange, amesema wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam na mikoa jirani wanatarajiwa kunufaika na upatikanaji wa umeme wa uhakika kufuatia miradi mbalimbali ya usafirishaji na usambazaji umeme inayotekelezwa katika maeneo hayo kufikia hatua za mwisho za utekelezaji.

Amesema kukamilika kwa miradi hiyo kutaimarisha uwezo wa miundombinu ya umeme na kuhakikisha umeme unaozalishwa nchini unasafirishwa na kuwafikia watumiaji kwa uhakika ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya kijamii na kiuchumi.

Akizungumza Novemba 20, 2026, wakati akikagua maendeleo ya miradi mbalimbali ya umeme, ikiwemo njia ya kusafirisha umeme ya Kimara – Mabibo – Ilala, njia ya kusafirisha umeme chini ya ardhi kutoka Kinyerezi hadi Gongo la Mboto, upanuzi wa Kituo cha Kupokea na Kupoza Umeme cha Dege, Kigamboni, pamoja na ujenzi wa Kituo cha Kisasa cha Kupoza Umeme cha Mabibo, Bw. Twange amesema miradi hiyo ipo katika hatua za mwisho za utekelezaji.

Ameeleza kuwa miradi hiyo inalenga kuongeza uwezo wa kusafirisha umeme kutoka vituo vya uzalishaji hadi kwa watumiaji, akibainisha kuwa Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani kwa pamoja unatumia takribani megawati 800 kwa sasa, huku mahitaji yakitarajiwa kuongezeka na kufikia megawati 900 kutokana na ukuaji wa shughuli za kiuchumi, viwanda na uwekezaji.

Aidha amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, imewekeza zaidi ya shilingi bilioni 193 katika miradi ya kuimarisha miundombinu ya usafirishaji wa umeme jijini Dar es Salaam na Mkoa wa Pwani, ikiwa ni hatua ya kuongeza uwezo wa miundombinu hiyo kukidhi mahitaji ya sasa na ya baadaye.

“Miradi hii inatekelezwa kwa fedha za ndani kupitia Serikali ya Awamu ya Sita, na kwa sasa ipo katika hatua za mwisho za utekelezaji. Baadhi inatarajiwa kukamilika Disemba mwaka huu na mingine mwishoni mwa Januari 2027. Kukamilika kwa miradi hii kutaiwezesha TANESCO kuwa na uwezo mkubwa zaidi wa kupeleka umeme kwa wateja wa majumbani, biashara na viwanda, pamoja na kutoa nafasi ya kuhudumia wawekezaji wanaohitaji umeme mkubwa kwa ajili ya uzalishaji.,” amefafanua Bw. Twange.

Pamoja na hayo, amesisitiza kuwa uwekezaji katika miundombinu ya umeme ni endelevu ili kuendana na ongezeko la watu na mahitaji ya nishati nchini. Ameeleza kuwa Serikali inalenga kuongeza uwezo wa uzalishaji wa umeme nchini hadi kufikia megawati 8,000 ifikapo mwaka 2030, kutoka takribani megawati 4,600 hadi 4,700 zilizopo sasa.

Baadhi ya miradi inayotekelezwa ni pamoja na upanuzi wa Kituo cha kupoza umeme cha Dege Kigamboni ambao umefikia asilimia 90.4, Mradi wa Kituo cha kisasa cha kupokea na kupoza cha mabibo ukiwa umefikia asilimia 94 huku Mradi wa njia ya kusafirisha umeme ardhini ya msongo wa kilovoti 132 kutoka Kinyerezi hadi Gongola mboto ukiwa umefikia asilimia 86.

spot_img

Latest articles

RAIS SAMIA KUFUNGUA MKUTANO MKUU WA TUME ZA UCHAGUZI ECF-SADC

Na Mwandishi Wetu RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan...

NESCH MINTEC YAPUNGUZA GHARAMA ZA VIPIMO VYA MADINI KUPITIA MAABARA YA MWANZA

Na Mwandishi Wetu WACHIMBAJI na wafanyabiashara wa madini nchini sasa wana fursa ya kupata...

OTR na IMF zajadili utendaji wa taasisi za umma

Na Mwandishi Wetu MSAJILI wa Hazina, Nehemiah Mchechu, amekutana na ujumbe wa Shirika la Fedha...

MAAMBUKIZI MAPYA YA VVU YAPUNGUA KUTOKA 98,754 HADI 33,511

Na Tatu Mohamed MAAMBUKIZI mapya ya Virusi vya Ukimwi (VVU) nchini yamepungua kutoka watu 98,754...

More like this

RAIS SAMIA KUFUNGUA MKUTANO MKUU WA TUME ZA UCHAGUZI ECF-SADC

Na Mwandishi Wetu RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan...

NESCH MINTEC YAPUNGUZA GHARAMA ZA VIPIMO VYA MADINI KUPITIA MAABARA YA MWANZA

Na Mwandishi Wetu WACHIMBAJI na wafanyabiashara wa madini nchini sasa wana fursa ya kupata...

OTR na IMF zajadili utendaji wa taasisi za umma

Na Mwandishi Wetu MSAJILI wa Hazina, Nehemiah Mchechu, amekutana na ujumbe wa Shirika la Fedha...