Rais Samia: Kituo cha EACLC kitaimarisha uchumi wa Taifa

Na Tatu Mohamed

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema uzinduzi wa Kituo cha Biashara na Usafirishaji Afrika Mashariki (EACLC) kilichopo Ubungo, Dar es Salaam ni hatua kubwa ya mageuzi ya uchumi wa nchi, kwa kuwa kitachochea biashara ya ndani na ya nje, kuongeza mapato ya serikali, na kupanua ajira kwa vijana.

Akizungumza leo Agosti 1, 2025, katika hafla ya uzinduzi wa kituo hicho, Rais Samia amesema mradi huo utaliwezesha taifa kuongeza ushindani wa bidhaa zake katika masoko ya kikanda na kimataifa huku pia ukiimarisha nafasi ya Tanzania kama kitovu cha biashara Afrika Mashariki.

“Kituo hiki kinaunganisha huduma zote muhimu kwa biashara na usafirishaji katika eneo moja. Kuna maghala ya kisasa, ofisi za biashara, huduma za forodha, bandari kavu na mifumo ya kidijitali ambayo itapunguza gharama na muda wa usafirishaji wa mizigo,” amesema Rais Samia.

Ameongeza kuwa mradi huo unaendana na dira ya serikali ya kujenga uchumi wa kidijitali, ambapo mifumo ya kielektroniki itatumika katika kusimamia shughuli za kituo hicho ili kuongeza uwazi, ufanisi na mapato.

Rais Samia amewataka wadau wa sekta binafsi na wananchi kushirikiana na serikali kuhakikisha kituo hicho kinatumika ipasavyo kwa manufaa ya taifa, huku akisisitiza kuwa mradi huo si mpinzani wa wafanyabiashara wa Kariakoo bali ni daraja la maarifa na teknolojia.

“Tuandae mkutano baina ya wafanyabiashara wa Kariakoo na wale wa EACLC ili kujifunza namna bora za kuendesha biashara kwa kutumia teknolojia, hivyo kuongeza faida na kuepuka upotevu wa mapato,” alieleza.

Aidha, amesema kituo hicho kitakuwa kiunganishi muhimu kati ya sekta binafsi za Tanzania na China, hasa kwa kuimarisha mauzo ya bidhaa zenye thamani kubwa kama korosho, kahawa, mazao ya asali, mvinyo na ufuta kwenda masoko ya kimataifa, ikiwemo China.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi (TISEZA), Gilead Teri, amesema kituo hicho kimejengwa kwa gharama ya Shilingi bilioni 282.7 na kitaweza kutoa ajira rasmi zaidi ya 15,000 pamoja na ajira zisizo rasmi zaidi ya 50,000.

Amesema kituo hicho chenye maduka zaidi ya 2,000 na ofisi za kisasa, kinatarajiwa kuchangia takribani Dola za Marekani milioni 8.2 kwa mwaka kupitia mapato ya serikali.

“Mbali na ajira, kituo hiki kitaongeza ushindani wa Bandari ya Dar es Salaam na kupunguza kwa asilimia 30 gharama za uendeshaji wa biashara kikanda,” amesema.

Mkurugenzi wa Kituo cha Biashara na Usafirishaji Afrika Mashariki (EACLC), Dkt. Lisa Wang Xiangyun, amesema kituo hicho kitatoa fursa kwa bidhaa mbalimbali kutoka Tanzania kusafirishwa kwa wingi kwenda China na nchi nyingine, huku bidhaa kutoka China kama mitambo zikiingizwa nchini kwa urahisi zaidi.

Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, amesema bidhaa zitakazozalishwa na kusambazwa kupitia kituo hicho zitakuwa na viwango vya kimataifa, jambo litakaloongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania duniani.

Kwa upande wake, Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar, Omary Said Shaban, amesema mradi huo unapaswa kuonekana kama fursa ya kukuza ujuzi, kuongeza thamani ya bidhaa, na kufungua milango ya biashara pana kwa wafanyabiashara wa Tanzania bara na visiwani.

spot_img

Latest articles

Vyombo vya habari vyatakiwa kuripoti habari za Uchaguzi Mkuu kwa usahihi

Na Tatu Mohamed VYOMBO vya habari nchini vimetakiwa kuwa makini katika kuripoti taarifa zinazohusu...

Tamasha la Singeli Agosti 2 wasanii kutoa burudani ya Kimataifa

Na Winfrida Mtoi Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa,...

Maandalizi ya Mkutano Mkuu Maalum UVCCM yamekamilika

Pichani ni Viongozi wa sekretarieti ya Umoja wa Vijana CCM wakikabidhi vifaa mbalimbali wezeshi...

INEC: Hakuna atakayeachwa nyuma kwenye Uchaguzi Mkuu 2025

Na Tatu Mohamed TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), imesema imeweka mazingira wezeshi...

More like this

Vyombo vya habari vyatakiwa kuripoti habari za Uchaguzi Mkuu kwa usahihi

Na Tatu Mohamed VYOMBO vya habari nchini vimetakiwa kuwa makini katika kuripoti taarifa zinazohusu...

Tamasha la Singeli Agosti 2 wasanii kutoa burudani ya Kimataifa

Na Winfrida Mtoi Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa,...

Maandalizi ya Mkutano Mkuu Maalum UVCCM yamekamilika

Pichani ni Viongozi wa sekretarieti ya Umoja wa Vijana CCM wakikabidhi vifaa mbalimbali wezeshi...