Na Winfrida Mtoi
Mwinjilisti wa Kanisa la EAGT, Mwanza, Diana Dionizi amewatoa hofu watanzania kuelekea uchaguzi mkuu mwaka huu kwa kusema tayari Mungu amemwandaa kiongozi ambaye ni faida kwa Taifa.
Ameyasema hayo leo Julai 26, 2025 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Mkutano wa Injili utakaofanyika kesho Julai 27 hadi Agosti 3, 2025 kwenye viwanja vya Mwembe Yanga, Temeke ambapo yeye ndiye mhubiri mkuu.

Ameeleza hakuna shaka Rais atapatikana na viongozi wote watakaotakiwa watasimamishwa kwa sababu tangu zamani imekuwa ikifanyika hivyo.
“Uchaguzi utakuwa wa amani na furaha, wasiogope. Kitu ambacho watanzania wanatakiwa wajue, sisi tunaweza tukachagua lakini Mungu ameshachagua mtu wake kabla ya sisi. Kwa hiyo Mungu atasimamisha yule ambaye ni faida kwa ajili ya watanzania na faida kwa ajili ya Taifa la Tanzania,” amesema.
Aidha amesema dunia inakwenda kwa kasi sana, hivyo kanisa linatakiwa kusimama kwa imani, pamoja na maombi.


“Siku hizi za mwisho unatakiwa kukaa kwa kutulia na kuchagua lililojema kutokana na kuwepo wingi wa Injili zinazohubiriwa ,” amesema.
Naye Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la EAGT Temeke, Christomoo Ngowi amewataka watu kujitokeza kwa wingi katika mkutano huo ili kupata huduma zilizoandaliwa pamoja na maombezi kwa wenye shida mbalimbali.
Kwa upande wake Mratibu wa mkutano huo, Joshua Isack amesema siku ya kesho hadi Jumapili ijayo kutakuwa kwaya na waimbaji mbalimbali mkutanoni wakiwamk John Lissu, Joel Lwaga na Boaz Dunken.