Machungu, damu yamwagwa tena

Maadhimisho ya Saba Saba nchini Kenya ni tukio muhimu katika kukumbuka mapambano ya kudai demokrasia nchini humo. Ilikuwa ni Julai 7, mwaka 1990 Wakenya kwa maelfu walipojimwaga barabarani na kisha kukutana katika uwanja wa Kamukunji kudai mabadiliko ya msingi ya kisheria ambayo yangewezesha kufanyika kwa uchaguzi huru na wa haki nchini humo. Maandamano hayo ndiyo yanatajwa kuutikisa vilivyo utawala wa mkono wa chuma wa Rais wa Pili wa taifa hilo, Daniel arap Moi, aliyepachikwa jina la Profesa wa siasa za Kenya. Pia Saba Saba yanatajwa kama chimbuko la mabadiliko ya katiba ya Kenya na kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini humo.

Mwaka huu maadhimisho hayo yalikuwa ni ya 35 na yalitarajiwa kufanyika kwa amani Jumatatu wiki hii – Julai 7, 2025. Isivyo bahati, yakageuka kuwa ni mapambano ya raia dhidi ya polisi. Miji mingi mikubwa nchini Kenya ikageuka kuwa uwanja wa mapambano ya saa kadhaa. Zikiwa ni takribani siku 10 tu baada ya kutokea kwa vurugu nyingine kubwa zilizoambatana na uporaji mkubwa wa maduka, benki na uharibifu mkubwa wa mali, raia wa Kenya wamejikuta tena kwenye simanzi kubwa- vifo, uharibifu wa mali na uporaji wa maduka. Swali kubwa linalosumbua kwa wengi ni hili, kwamba hali hii ya kuzidi kuzorota kwa usalama itakwenda mpaka wapi?

Miongoni mwa miji mikubwa iliyoshuhudia vurugu hizo ambazo pia zimesababisha vifo kadhaa, ni pamoja na Nairobi, Eldoret, Kisii, Nakuru, Machakosi kutaja kwa uchache tu. Sura ya hali ya usalama iliyoshuhudiwa ni ya kutisha. Mapambano yamebadili sura na mwelekeo kuwa baina ya polisi na wafanyabiashara wanaolinda mali zao zisiporwe kwa upande mmoja, na waandamanaji ambao kwa hakika wamegeuka kuwa magenge ya uporaji wa biashara na uharibifu wa mali za watu wengine kwa upande mwingine. Maandamano haya nchini Kenya yameweka dosari kubwa kwenye demokrasia.

Tangu Juni mwaka jana vijana wa Gen Z walipojimwaga barabarani kwa maelfu wakipinga kuwasilishwa Bungeni kwa muswada wa fedha wa mwaka 2024, mfululizo wa maandamano, mauaji, uporaji vimekuwa ni matukio ya kujirudiarudia nchini humo. Ingawa shinikizo la Gen Z mwaka jana lilionekana kuwa na matunda chanya kufuatia kufanyika kwa mabadiliko ya serikali na hata kuondolewa kwa muswada wa fedha, na hatimaye kuvunjwa kwa baraza la mawaziri la Rais William Ruto, bado bundi la maandamano linaelekea kuganda katika anga ya Kenya.

Vyombo vya habari vya nchini Kenya Juni 26, mwaka huu vilizuiwa na mamlaka ya kusimamia vyombo vya kieletroniki, kuonyesha mubashara maandamano yaliyoacha historia kubwa ya uporaji, uharibifu wa mali ambayo pia askari polisi walishambuliwa, kupigwa na kuporwa vifaa vya kazi. Sababu za zuio hilo lilielezwa kuwa ni kusaidia kupunguza ‘kumwaga petroli kwenye moto uliokuwa unawaka tayari. Yaliyotokea tena wiki hii, yanaamsha tafakari mpya juu ya kiini hasa cha kubadilika kwa mwelekeo wa maandamano haya kutoka kuwa ya amani kuwa ya vurugu na uporaji.

Kenya inatajwa kuwa miongoni mwa nchi za Afrika yenye katiba ya kidemokrasia. Inatajwa kuhakikishia mihimili ya dola – mahakama, bunge na serikali madaraka yake yasiyoingiliwa, lakini ambayo yanaruhusu kudhibitiana kwa kiwango cha kuepusha matumizi mabaya ya madaraka miongoni mwa mihimili hiyo. Wakati Kenya ikifikiriwa hivyo, yanayoendelea nchini humo kwa sasa yanageuka kuwa mtihani siyo tu kwa taifa hilo peke yake, bali hata majirani zake katika jumuiko la Afrika Mashariki.

Ukora wa uporaji wa maduka na uharibifu mkubwa wa mali ulioshuhudiwa Juni 26, 2025 kwa kiwango kikubwa umesababisha uamuzi wa Jeshi la Polisi nchini humo kuzuia kufanyika kwa maandamano ya Saba Saba. Ni kwa kuakisi matukio ya Juni 26, mwaka huu, polisi wamejikuta katika mtego mgumu wa kuhakikisha kwamba maandamano hayo yanafanyika kwa amani, wakati huo huo kuwahakikishia wananchi usalama wao na mali zao. Hali hii ni ya muhali mkubwa kwa vyombo vya ulinzi na usalama.

Mkanganyiko huu unawasilisha picha nyingine ngumu ya hali ya mambo ilivyo nchini Kenya. Ukisikiliza kauli za waandamanaji – wengi wao wakiwa ni vijana, wanalia hali mbaya ya uchumi, ukosefu wa ajira, ongezeko kubwa la gharama za maisha na kuzidi kuongezeka kwa hali ya kutokuaminiana baina ya watawala na wananchi – hasa vijana na wale wa tabaka la chini.

Kwamba mataifa mengi ya Afrika yana kundi kubwa la raia ambao ni vijana, wengine wakifikia hadi asilimia 60 ya idadi yote ya watu, ni hali inayowasilisha mfanano wa mambo yalivyo katika nchi hizo. Wengi hawana ajira, wanakabiliwa na umasikini wa kipato na kuachwa pembezoni mwa miliki ya uchumi wa mataifa yao.

Sura ya Kenya inaibua hali ya wasiwasi na mashaka makubwa kwamba ni nini hasa kinafaa kufanyika ili amani, ustawi na utulivu vishamiri katika nchi hizi? Je, uhusiano wa Jeshi la Polisi na wananchi katika nchi ambayo ilidhaniwa kwamba katiba yake ni ya kidemokrasia hivyo ingeliweza kuwa mwarobaini ya matatizo yao, unatuma ujumbe gani kwa nchi nyingine za Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla? Ni kama vile Katiba nzuri bila kuondoa umasikini ni bure.

Isivyo habati waandamanaji wamekuwa wakibeba ajenda ya kukumbuka raia wenzao waliokufa katika harakati za maandamano kama hayo miaka iliyopita na hata katika maadhimisho ya harakati za Gen Z za mwaka jana, lakini matokeo yake ni damu nyingine kumwagwa. Maandamano ya Saba Saba hadi usiku wa Jumatatu wiki hii ilithibitishwa kwamba takribani watu 10 walikuwa wameuawa. Aidha, wengine kwa makumi walikuwa wamejeruhiwa katika kurupushani kati ya polisi na waandamanaji. Kwa vyovyote, kuendelea kumwagwa kwa damu hii kunazidi kuongeza hali ya uhasama baina ya waandamanaji (wananchi) kwa upande mmoja na vyombo vya usalama na serikali kwa upande mwingine.

Ni vigumu kusadiki kwamba Kenya ambayo Mei 30, mwaka huu iliwafikisha mahakamani askari polisi kwa kuhusika na mauaji ya mwanablog Albert Ojwang, ni hiyo hiyo ya matukio ya Saba Saba Jumatatu wiki hii. Uamuzi wa kuwashitaki askari hao uliiweka nchi hiyo katika mizania nzuri ya kukuza uwajibikaji na utawala wa sheria, lakini kadhia za Saba Saba zimeiweka nchi hiyo katika sura ya utawala ambao unakabiliwa na changamoto nzito za kuhimili madai na malalamiko ya raia wake.

Hakika mfululizo wa maandamano haya nchini Kenya tangu Juni mwaka jana, yanaiacha serikali ya Rais Ruto katika mtihani mkubwa zaidi wa kuhakikisha kwamba nchi hiyo inakuwa na utengamano na raia wanaoiamini serikali waliyoichagua wenyewe kwenye sanduku la kura.

Hali hii ya serikali iliyoko madarakani kupitia sanduku la kura kukabiliwa na changamoto na shinikizo kubwa kama analopitia Rais Ruto, inaibua tafakari kubwa juu ya nafasi ya matakwa ya umma kwa upande mmoja na nafasi ya watawala na mifumo ya sheria, katiba na uwajibikaji kwa upande mwingine. Watawala wanajikuta katika mtihani mgumu wa kuridhisha umma unaoongezeka hasira kila uchao.

spot_img

Latest articles

Ndumbaro: Sheria 300 Zimetafsiriwa kwa Kiswahili Ili Kuimarisha Uelewa kwa Wananchi

Na Tatu Mohamed WAZIRI wa Katiba na Sheria, Dkt. Damas Ndumbaro, amesema kuwa hadi...

Jessica: CCM inajali uongozi wa vijana

Na Mwandishi Wetu KATIBU wa Idara ya Uhamasishaji na Chipukizi UVCCM TAIFA, Jessica Mshama...

Waziri Aweso: Tuna uhakika wa maji ya kutosha Dar na Pwani

Na Mwandishi Wetu WAZIRI wa Maji, Jumaa Aweso amewatoa hofu wakazi wa mikoa ya...

PURA yajivunia mafanikio katika Ajenda ya Nishati Safi na ushiriki wa Watanzania Sekta ya Mafuta na Gesi

Na Tatu Mohamed MAMLAKA ya Kudhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) imesema inajivunia...

More like this

Ndumbaro: Sheria 300 Zimetafsiriwa kwa Kiswahili Ili Kuimarisha Uelewa kwa Wananchi

Na Tatu Mohamed WAZIRI wa Katiba na Sheria, Dkt. Damas Ndumbaro, amesema kuwa hadi...

Jessica: CCM inajali uongozi wa vijana

Na Mwandishi Wetu KATIBU wa Idara ya Uhamasishaji na Chipukizi UVCCM TAIFA, Jessica Mshama...

Waziri Aweso: Tuna uhakika wa maji ya kutosha Dar na Pwani

Na Mwandishi Wetu WAZIRI wa Maji, Jumaa Aweso amewatoa hofu wakazi wa mikoa ya...