Tarura Kigamboni yaanza ujenzi wa Barabara za Lami KM 42 kupitia Mradi wa DMDP II

Na Mwandishi Wetu

WAKALA ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) umeanza kutekeleza ujenzi wa barabara Km 42 kwa kiwango cha lami kupitia mradi wa Uendelezaji Jiji la Dar es Salaam Awamu ya Pili (DMDP II) katika Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni jijini Dar es Salaam.

Hayo yameelezwa na Meneja wa TARURA Wilaya ya Kigamboni, Mhandisi Ismail Mafita ambapo amesema kuwa mpaka sasa wakandarasi watatu wapo “site” wanaendelea na ujenzi wa barabara Km 30 huku Km 10.2 zipo katika mchakato wa manunuzi.

“Mpaka kufikia mwisho wa mwezi Juni mwaka huu zabuni zitatangazwa kwahiyo katika kipindi cha mwezi mmoja au miwili ijayo hizo Km 10 zitaanza kutekelezwa”, amesema Mhandisi Mafita.

Amesema kuwa tayari mradi wa DMDP II umeshaanza kuleta matokeo kwani barabara ambazo zilikuwa na changamoto zimeshaanza kufanyiwa kazi na wanatarajia mwakani mwezi Februari au Machi barabara zote Km 42 zitakuwa zimekamilika na kuleta matokeo makubwa katika manispaa ya kigamboni.

“Jumla ya fedha zilizotengwa ni shilingi bilioni 100 lakini kwa Km 30 ambazo tayari wakandarasi wapo “site” zina jumla ya shilingi bilioni 78, kwakweli ni fedha nyingi lakini pindi mradi utakapokamilika wananchi watanufaika na miundombinu hii”.

Ameeleza kuwa kazi zitakazofanyika katika mradi wa DMDP II ni ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami, njia za waenda kwa miguu, vituo vya daladala, taa za barabarani na mifereji ambapo amewaomba wananchi wawe watulivu katika kipindi cha mpito cha ujenzi mara baada ya shughuli za ujenzi kukamilika mitaa yote itapendeza na itakuwa safi na salama.

Mhandisi Mafita ameongeza kwamba wanaendelea kutekeleza miradi mingine mbalimbali katika wilaya hiyo ambayo imepata bajeti ya bilioni 5 kwa ujenzi wa barabara ya Kivukoni Primary School na Rombo Bar kwa kiwango cha lami Km 0.62, pia mkandarasi yupo kazini anakamilisha mita 500 katika barabara kuu inayoelekea daraja la Mwl. Nyerere ambapo zikikamilika zitasaidia wakazi wa Kigamboni wanaoelekea maeneo ya Kivukoni au darajani kutumia barabara bila changamoto yoyote.

Naye, mkazi wa mtaa wa Salanga Kigamboni, Stephano James amesema awali walikuwa na changamoto ya barabara, mvua zikinyesha maji yakijaa pikipiki zao zilikuwa zinaharibika lakini sasa wanafanya kazi zao bila shida na wanaiomba serikali iendelee kuwaboreshea miundombinu ili kuzifikia huduma za kijamii kwa urahisi.

Ally Yusuph mkazi wa kata ya Vijibweni Kigamboni, amesema kuwa adha kubwa waliyokuwa wanaipata ni vumbi, madimbwi na matope lakini barabara ikiwekwa lami watafurahi sana na wanaomba mkandarasi asimamiwe ili kazi ikamilike kwa wakati.

Farid Yusuph mkazi wa mtaa wa feri Kigamboni ameishukuru serikali kwa kuwaboreshea miundombinu na ameomba waongezewe alama za barabarani na matuta na pia ameomba wananchi wenzake wailinde miundombinu hiyo kwa kuwa wastaarabu na kutotupa takataka kwenye mifereji.

spot_img

Latest articles

ELAF yahimiza maridhiano na amani baada ya Uchaguzi Mkuu

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam TAASISI ya Everlasting Legal Aid Foundation (ELAF) imewataka Watanzania...

Taifa Stars ya Gamondi amrejesha Kelvin John

Na Mwandishi Wetu Kaimu Kocha Mkuu wa timu ya Taifa, Taifa Stars Miguel Gamondi amemrudisha...

‘Hali ya huduma ya maji Dar, Pwani ni shwari’

Na Mwandishi Wetu WAKAZI mbalimbali wa Jiji la Dar es Salaam na Mkoa wa...

Mwanasheria Mkuu wa Serikali: Uchaguzi Mkuu wa 2025 ni halali

Na Mwandishi wetu MWANASHERIA Mkuu wa Serikali, Hamza Johari amesema kuwa, Uchaguzi Mkuu wa...

More like this

ELAF yahimiza maridhiano na amani baada ya Uchaguzi Mkuu

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam TAASISI ya Everlasting Legal Aid Foundation (ELAF) imewataka Watanzania...

Taifa Stars ya Gamondi amrejesha Kelvin John

Na Mwandishi Wetu Kaimu Kocha Mkuu wa timu ya Taifa, Taifa Stars Miguel Gamondi amemrudisha...

‘Hali ya huduma ya maji Dar, Pwani ni shwari’

Na Mwandishi Wetu WAKAZI mbalimbali wa Jiji la Dar es Salaam na Mkoa wa...