Ni nyakati za hatari, utu umetupwa kule

KUNA kila dalili kwamba dunia kwa ujumla wake imekumbwa na hali ya kutia shaka sana, kiasi kwamba hisia za watu juu ya madhila yanayowapata watu wengine ni kama zimekufa kabisa.

Duniani leo kuna maeneo ambako kuna mizozo mikubwa na mapigano na mamilioni ya watu wameathirika. Kwa bahati mbaya wakubwa wa dunia hii ni kama hawajali kabisa wala kusumbuliwa na hali hiyo. Kwa mfano, yanayoendelea katika ukanda wa Gaza eneo ambalo dunia inajua ni makazi ya Wapalestina, ni kitisho dhidi ya utu, ubinadamu na kukosekana kabisa kwa huruma miongoni mwa jamii ya kimataifa.

Picha kwa hisani ya BBC

Picha za vyombo vya habari zikionyesha mamia ya Wapalestina wakisukumana kupata chakula cha msaada wa kusitiri uhai wao, siyo chakula cha kutosha, ni matukio ambayo hakika yanasumbua hisia za ndani kabisa za binadamu yeyote mwenye kujali utu wa binadamu.

Nchini Sudan hali ni tete pia, takribani watu 150,000 wameuawa tangu mzozo wa wenyewe kwa wenyewe uibuke miaka miwili na ushei sasa. Taarifa za mashirika mbalimbali ya misaada ya kibinadamu zinasema kwamba hadi Mei mwaka huu nchini Sudan, watu milioni 13 wameyakimbia makazi yao ili kunusuru nafsi zao dhidi ya vita. Watu hawa ambao ni raia wasiokuwa na hatia ni pamoja na watu milioni 8.8 ambao wameacha makazi yao na kutafuta hifadhi maeneo mengine ya Sudan, na watu wengine takribani milioni nne ambao wamevuka mipaka na kupata hifadhi ya ukimbizi katika nchi za jirani za Sudan Kusini, Chad, Misri, Ethiopia na Jamhuri ya Afrika ya Kati. Hali ni mbaya sana hasa kwa watoto na wanawake na janga kubwa la njaa na utapiamlo linakabili watoto wengi kwa mamilioni.

Kwa kutambua hali mbaya inayokabili Sudan iliyosababishwa na wababe wawili wanagombea madaraka, wale wa Majeshi ya Serikali ya Sudan (SAF) wakiongozwa na Jenerali Abdel Fattah al Burhan na wale wa Rapid Support Forces (RSF), wakiongozwa na Mohamed Hamdan Dagalo, Umoja wa Mataifa umeomba walau Dola za Marekani bilioni sita ili kukabiliana na hali ya hatari wanayokabiliwa nayo raia wa Sudan, lakini ni kiasi kidogo sana cha msaada huu kimepatikana mpaka sasa. Hali ya Sudan ni ya kutisha.

Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) upande wa mashariki mwa nchi hii, nako hali ni tete. Mgogoro wa DRC ambao umejidhihirisha katika sura ya raia wa nchi hiyo wakisaidiwa na majeshi ya Rwanda, kupigana kwa kile wanachodai kutafuta haki ya kutambuliwa, hadi sasa umesababisha zaidi ya watu milioni 10 kuyakimbia makazi yao. Ingawa hivi karibuni serikali ya Rwanda ilikubali kuingia katika makubaliano ya kusitishwa kwa mapigano na serikali ya DRC, bado zaidi ya watu milioni 11 wanahitaji msaada wa kibinadamu ambao hauonekani ukiwafikia.

Umoja wa Mataifa umeomba takribani Dola za Marekani bilioni 2.54 ili kusaidia janga kubwa la binadamu linalokabili watu milioni 11, lakini muitikio ni mdogo sana kwani kiasi kilichopatikana ni chini ya nusu ya hicho. Hali ya DRC Mashariki ni mbaya.

Maeneo mengine ambako kuna mapigano makubwa ni Ukraine ambako majeshi ya Urusi yalivamia nchini hiyo. Miaka miwili na ushei sasa imepita tangu vita hivyo vianze, na maafa yanazidi kuendelea. Takribani watu 120,000 wakiwa ni wanajeshi tu wa pande zote mbili, Ukraine na Urusi wanadaiwa kuuawa katika vita hivyo. Maelfu ya raia wamekosa makazi huku malaki ya wanajeshi wakidaiwa kujeruhiwa vitani.

Migogoro hii ambayo imetanda duniani kwa sasa, ukiacha mingine ambayo imekuwako kwa kitambo sasa kama ile ya Yemen, Chad, Syria kutaja tu kwa uchache, inaelekea kusaidia kujengeka kwa hali ya ukiukaji wa haki za binadamu duniani kote. Hali hii ni kama imetoa stakabadhi ya uhalali wa mataifa mbalimbali duniani kukalia na kukanyaga haki za raia wake.

Dunia ni kama sasa imeinamia na kukumbatia uonevu, umwagaji wa damu na mauaji makubwa ya raia wasiokuwa na hatia na ambao kimsingi hawawezi kujitetea wenyewe bila msaada.

Serikali mbalimbali za mataifa hasa ya nchi za ulimwengu wa tatu, zinachukulia hali hii tete na duniani kuruhusu na kufumbia macho madhila yanayotendwa na vyombo vyake vya ulinzi na usalama dhidi ya raia wake. Matukio ya kukamatwa kwa watu na kushitakiwa kwa makosa makubwa makubwa kwa sasa imekuwa ndiyo mfumo wa maisha wa kunyamazisha kila sauti huru inayohoji vitendo vya kutofuata sheria na hata kukanyaga katiba za mataifa mbalimbali.

Waliokuwa na utamaduni walau wa kukemea au hata kulaani matendo maovu dhidi ya wanyonge, nao ni kama wamejiunga na watesi wa wananchi katika mataifa mbalimbali.

Haya yako Afrika, na maeneo mengine mengi duniani. Uonevu umekuwa fasheni. Na kuna dalili za mataifa mengine kujichimbia kwenye kichaka cha kutokutaka kuingiliwa kwa mambo yake ya ndani wanapoulizwa juu ya uovu unaotendwa na ama na vyombo vyake au na makundi ya kihalifu ambayo hayafanywi lolote na mamlaka za dola. Ni jambo la bahati mbaya sana kwamba kikubwa ambacho watu wanajali kwa sasa ni kupata fursa ya kufanya mambo yao- biashara. Kupata fursa za kiuchumi hata kama mbele yao wanateketezwa watu wasiokuwa na hatia.

Hali hii inajieleza wazi jinsi baadhi ya nchi zinazotafuta kusaidia kutokomeza migogoro duniani kwa kuhakikishiwa kwanza ni kwa jinsi gani watanufaika na rasilimali za taifa lililoko katika shinikizo kubwa la watu wake kuonewa na kuuawa tu kama wanyama porini. Watawala wameingizwa kwenye kona ngumu.

Karibu mataifa yote makubwa yamepoteza uhalali wa kimaadili (moral authority) wa kutetea haki na utu. Yamejikita zaidi katika kutafuta fursa za kujinufaisha na rasilimali za mataifa yanayoonewa, yaliyoko kwenye mgogoro na ambayo kwa kweli jumuiya ya kimataifa ingepaswa kujipanga kutafuta suluhu ya madhila yanayowakuta watu hao.

Jaribu kufikiria yanayotokea Gaza au Sudan au DRC na kwingineko, madhila wanayokumbana nayo watu wa mataifa hayo ni magumu yasiyoelezeka, lakini hata katika kadhia hii nani anajali. Na ni katika mtiririko na mserereko wa kutokujali haki za raia, serikali mbalimbali za mataifa hasa ya ulimwengu wa tatu yamepata kiburi kikubwa cha kuendesha mateso na mauaji dhidi ya raia wake wenyewe kwa kuwa sasa hivi kinachotakiwa duniani ni makubaliano ya kuachia rasilimali ziwanufaishe wakubwa. Madhila dhidi ya wananchi wa mataifa yenye migogoro siyo jambo la kuwasumbua tena wakubwa wa dunia hii. Hata kukemea wameacha. Aibu ya dunia.

spot_img

Latest articles

Baba Levo atembelea Banda la TTCL Sabasaba, apongeza Mapinduzi ya Kidijitali

Na Mwandishi Wetu MSANII na mtangazaji maarufu nchini, Clayton Chipando maarufu kama Baba Levo,...

Takwimu za Samia ni nzito, kupotezwa watu akaze zaidi

IJUMAA ya wiki iliyopita yaani Juni 27, 2025 Rais Samia Suluhu Hassan aliweka historia...

Maonesho ya Sabasaba kufunguliwa Julai 7 na Rais Mwinyi

Na Tatu Mohamed RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinzudi, Dkt. Hussein...

TTCL Yajipambanua Kama Muunganishaji Thabiti wa Mawasiliano Sabasaba 2025

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam SHIRIKA la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limeendelea kudhihirisha uwezo wake...

More like this

Baba Levo atembelea Banda la TTCL Sabasaba, apongeza Mapinduzi ya Kidijitali

Na Mwandishi Wetu MSANII na mtangazaji maarufu nchini, Clayton Chipando maarufu kama Baba Levo,...

Takwimu za Samia ni nzito, kupotezwa watu akaze zaidi

IJUMAA ya wiki iliyopita yaani Juni 27, 2025 Rais Samia Suluhu Hassan aliweka historia...

Maonesho ya Sabasaba kufunguliwa Julai 7 na Rais Mwinyi

Na Tatu Mohamed RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinzudi, Dkt. Hussein...