Nani hasa mnufaika wa umwagaji wa damu nchini?

Imemwagika nyingine tena. Hii ni damu ya raia wa Tanzania. Kidogo kidogo taifa linataka kuzoeshwa kwamba kumwaga damu ya raia wasiokuwa na hatia ni jambo la kawaida.

Kwa mtindo ule ule wa matukio ya watu wanaodaiwa ‘wasiojulikana’ wameibuka upya na kuendeleza ujahili wao dhidi ya raia. Tukiwa bado na shauku iliyochanganyika na ghadhabu ya kujua waliko raia wengine wa Tanzania waliopotea na hata miili yao kutokuonekana kabisa, kishindo cha wasiojulikana wiki iliyopita kimetikisa tena.

Safari hii Makao Makuu ya Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC) usiku wa Aprili 30, 2025 yalishuhudia shambulizi baya dhidi ya Katibu wao, Padri Charles Kitima. Kiongozi huyu ambaye kwa hakika hajawahi kunyamazia uovu bila kuukemea, alishambuliwa usiku akiwa katika makazi hayo. Aliumizwa maeneo mbalimbali ya mwili, ikiwa ni pamoja na kichwani. Wasamaria wema walifanikiwa kumpeleka hospitali Padri Kitima ambako alilazwa kwa matibabu. Tukio hili lilikuwa ni la mshituko mkubwa, nia dhidi ya kuukatili uhai wake ilikuwa dhahiri kwa jinsi shambulizi lilivyofanywa. TEC wametoa tamko juu ya shambulizi hili. Wamelaani tukio hilo na kutaka wote waliohusika na ujahili huo wakamatwe na kushitakiwa.

Mei Mosi, polisi walitangaza kumkamata mtu mmoja kuhusiana na shambulizi dhidi ya Padri Kitima makao makuu ya TEC.

Wakati hata akili za watu hazijatafakari kwa kina tukio baya la kushambuliwa kwa Padri Kitima, siku mbili tu baadaye jijini Mbeya, Mei 2, 2025 watu wasiojulikana walimvamia kada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mdude Nyagali. Taarifa ambazo zilisambaa katika mitandao ya kijamii zilieleza kwamba watu hao walivunja mlango wa nyumba yake, kisha wakamjeruhi na kuondoka naye.

Picha zilizopigwa nyumbani kwake zilionyesha michirizi ya damu ikiwa imetapakaa kwenye chumba kinachoaminika ndiko ujahili huo ulifanywa dhidi yake. Hadi sasa haijulikani aliko. Polisi wamekanusha tuhuma dhidi yao kwamba waliotenda uovu huo ni askari wake. Wametangaza msako wa kuwapata wahusika wa uovu huo, pia kutafuta aliko Mdude.

Wakati polisi wakitoa taarifa kwamba wanaendelea kuwasaka wahusika wa ujahili huu, bado umma mpaka leo haujapatiwa taarifa za kina za kupatikana kwa wahusika wa matukio mengine mengi yanayofanana na hayo.

Miongoni mwa matukio ya kupotea/kupotezwa kwa watu, hasa wanasiasa, yenye utata ni pamoja na tukio la Mei 23, 2025 la Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM, Daniel Chonchorio Nyamhanga (46) anayedaiwa kutekwa na watu wasiojulikana. Taarifa kutoka kwa wanafamilia zilisema kuwa ndugu yao alifuatwa nyumbani kwake jijini Mwanza na watu wanne waliokuwa na gari na kisha kuondoka naye. Tangu siku hiyo hadi sasa haijulikani aliko. Tukio hilo lilitokea baada ya jingine la Februari 14, 2025 jijini Mwanza pia ambalo Katibu wa Baraza la Vijana wa Chadema mkoani Mwanza, Amani Manongelo, kupotea/kupotezwa.

Matukio haya ni mengi. Taifa bado linasubiri taarifa za waliko makada wengine wa Chadema ambao mwaka jana walipotea/potezwa. Makada hao, Jacob Mlay wa Chadema Katibu Temeke; Deusdedit Soko, Katibu Bavicha Temeke na mwanachama wa Chadema, Frank Mbise, wanadaiwa kupotea katika mazingira ya kutatanisha. Hata hivyo, chama hicho kimekuwa kikilituhumu Jeshi la Polisi kuwa na mikono katika kupotea kwa viongozi hao.

Hawa wanaopotea/potezwa, kushambuliwa au hata kuuawa kama Mzee Ali Kibao, ni Watanzania. Wana haki ya kuishi kwa uhuru na amani kama raia mwingine yeyote wa Tanzania. Kikubwa zaidi dola ina wajibu wa kulinda uhai wa raia wake wote. Tumeshuhudia nchi zikiingia vitani kwenda kukomboa raia wake ambao wametekwa na taifa jingine.

Ulinzi wa uhai na usalama wa raia ni wajibu mkubwa wa dola. Jeshi la Polisi ni chombo cha mabavu, lakini kina dhima adhimu ya kulinda raia na mali zao. Polisi wanapaswa kufanya kazi ya ziada ili kuhakikisha kila raia anaishi kwa usalama na amani. Huu ni wajibu wa Jeshi la Polisi. Wajibu huu hauwezi kupewa chombo kingine chochote. Kwa mantiki hii, kila damu ya raia asiye na hatia inayomwagwa ni matarajio ya umma kuona kwamba wahusika wa ujahili huo wanakamatwa na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria ili haki ipatikane.

Familia inapopotelewa na ndugu, au anapopotezwa ndugu yao, inaingia katika simanzi isiyomithilika. Je, itasubiri kwa muda gani wakiamini labda ndugu yao atarejea? Au wataanua matanga baada ya muda gani? Je, hizo familia zinazonyang’anywa mpendwa wao kikatili hivyo, zitapona vipi majeraha ya uchungu na huzuni? Watoto wanaoachwa yatima na wanawake wanaoachwa wajane, watabeba uchungu huo kwa uwezo gani na kwa kiasi gani?

Kila wakati matukio ya umwagaji damu yanapotokea huwa ninapata maswali mengi kichwani, kubwa ni hili nani huyo hasa anayefaidika na umwagaji wa damu ya raia wa nchi hii. Je, ni pepo gani limevamia nchi yetu ambalo haliishi kutamani damu ya raia wasiyo na hatia? Ni kwa nini kumwaga damu kumekuwa ni kwa kawaida sana? Ni kwa nini matendo haya yanatokea mara kwa mara kiasi kwamba uwajibikaji juu yake umekuwa ni mdogo sana?

Matukio haya yanapotokea kumekuwa na kawaida ya kelele na vilio vingi kusikika, lakini baada ya kitambo kidogo tu, kelele hizi na vilio hufifia mpaka kupotea kabisa. Hata hivyo, baadaye matendo hayo ya ujahili yanatokea tena na tena. Tunarejea kwenye mzunguko ule ule, uchunguzi wa polisi haufiki mwisho, majibu hayapatikani na familia zilizopoteza wapendwa wao zinaendelea kubeba machungu yasiyoelezeka mioyoni mwao.

Utamaduni huu mpya nchini kwetu ambao unasukumwa ili jamii ione kuwa kupotea kwa watu, kuuawa kwa watu na kumwaga damu za watu wasiokuwa na hatia ni mambo ya kawaida, ni lazima sasa jamii iukatae. Ni dhahiri kama jamii kwa ujumla wetu haitakataa matendo haya, tujue tu hakuna aliyeko salama. Kwa bahati mbaya sana, cheo ni sawa na koti la kuazima, ndiyo maana ya ‘cheo ni dhamana.’ Kama kuna wanaodhani kwamba wako salama dhidi ya madhila haya labda kwa kuwa wamekalia nafasi fulani, wanajidanganya mno. Ni vema wakakumbuka tu kwamba damu isiyokuwa na hatia ikimwagwa ina tabia ya kulia kutoka ardhini ikitafuta haki, ikitafuta malipizi. Ole wa miguu inayokimbilia kwenda kumwaga damu maana hawatakaa wawe na utulivu maishani, malipizi yatawafuata tu hata katika uzee wao na wale wa nyumbani kwao.

spot_img

Latest articles

Baba Levo atembelea Banda la TTCL Sabasaba, apongeza Mapinduzi ya Kidijitali

Na Mwandishi Wetu MSANII na mtangazaji maarufu nchini, Clayton Chipando maarufu kama Baba Levo,...

Takwimu za Samia ni nzito, kupotezwa watu akaze zaidi

IJUMAA ya wiki iliyopita yaani Juni 27, 2025 Rais Samia Suluhu Hassan aliweka historia...

Maonesho ya Sabasaba kufunguliwa Julai 7 na Rais Mwinyi

Na Tatu Mohamed RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinzudi, Dkt. Hussein...

TTCL Yajipambanua Kama Muunganishaji Thabiti wa Mawasiliano Sabasaba 2025

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam SHIRIKA la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limeendelea kudhihirisha uwezo wake...

More like this

Baba Levo atembelea Banda la TTCL Sabasaba, apongeza Mapinduzi ya Kidijitali

Na Mwandishi Wetu MSANII na mtangazaji maarufu nchini, Clayton Chipando maarufu kama Baba Levo,...

Takwimu za Samia ni nzito, kupotezwa watu akaze zaidi

IJUMAA ya wiki iliyopita yaani Juni 27, 2025 Rais Samia Suluhu Hassan aliweka historia...

Maonesho ya Sabasaba kufunguliwa Julai 7 na Rais Mwinyi

Na Tatu Mohamed RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinzudi, Dkt. Hussein...