Naamini ‘wagonjwa’ wa PhD wamesikia somo la Malawi

Malawi ni miongoni mwa nchi ndogo za barani Afrika. Kati ya nchi 54 za Afrika, Malawi inayokadiriwa kuwa na watu 21,949,625 ni ya 36 kwa ukubwa ikiwa na eneo la kilometa za mrada 118,484. Mwezi uliopita nchi hii jirani ya Tanzania kwa upande kwa kusini magharibi ilitoa somo kubwa katika kuheshimu elimu. Baraza la Ithibati la Elimu ya Juu la Malawi lilitoa maelekezo ya matumizi ya shahada za uzamivu za heshima (Honorary PhD) kwamba hazistahili kutumika kana kwamba waliotunukiwa wamepitia mchakato wa kitaaluma. Kwa maana hiyo, siyo sawa kutumia cheo cha Daktari wa Falsafa kana kwamba muhusika amesomea hadhi hiyo.

Hapa nchini wakati wa utawala wa awamu ya nne, kuna Mtanzania mmoja aliandika kitabu alichokipa jina la ‘Mafisadi wa Elimu’. Mle ndani aliorodhesha majina ya watu, wengi wakiwa ni viongozi wa kisiasa ambao walikuwa wanatumia nyadhifa za Daktari wa Falsafa kana kwamba wana sifa za kitaaluma za hadhi hizo za kielimu.

Ingawa kumekuwa na mijadala mbalimbali juu ya matumizi ya vyeo hivi kwa wale waliotunukiwa shahada za falsafa za heshima kama ni sawa au la, kiu ya watu kutumia vyeo hivyo ni kubwa sana kwa sasa na inaonekana kuongezeka kila uchao.

Waliotunukiwa shahada hizi za heshima katika miaka ya hivi karibuni wameingiwa na kiu ya ajabu sana wakidhani kwamba wao ni wa kwanza kupata utambuzi huo. Wamekuwa wakizitumia kujitambulisha ili kujiongezea hadhi zao mbele ya jamii. Swali la kujiuliza ni hili, je, ni sahihi kuendelea kutumia vyeo hivyo kama utambulisho wao?

Tukumbushane kidogo, miaka ya nyuma wapo viongozi wengi sana wa kisiasa walitunukiwa hizo shahada za heshima. Kwa Tanzania watu kama akina John Samwel Malecela na Mwalimu Julius Nyerere ni kati ya waliopata kutunukiwa shahada hizo. Kwa mfano katika uhai wake Mwalimu Nyerere alitunukiwa walau shahada za heshima 23 kutoka vyuo vikuu mbalimbali duniani. Mbali ya kutunukiwa tuzo nyingine kwa makumi mengi, katika shahada za heshima alizotunukiwa Mwalimu Nyerere walau 11 zilikuwa ni za uzamivu (PhD). Hata hivyo, Mwalimu Nyerere hakuwahi kutamani kutambulishwa kwa kutanguliza cheo cha daktari wa falsafa. Alibaki na cheo chake cha Mwalimu ambayo ilikuwa ni kazi yake ya kwanza katika utumishi wa umma.

Benjamin Mkapa, Rais wa tatu wa Tanzania alitunukiwa shahada za heshima tisa kutoka vyuo vikuu mbalimbali duniani, kati hizo tano zilikuwa za uzamivu yaani PhD. Hakuna rekodi kokote katika uhai wa Mkapa kwamba kuna siku alirejewa kama daktari. Aliendelea kuitwa kama hapo kabla ya kutunukiwa shahada hizo.

Sasa tunapotafakari nyakati za sasa na kiu ya watu kutamani sana vyeo, hadhi na kila aina ya harakati za kujipachika vyeo hivi huwa najiuliza maswali magumu kidogo. Je, tunapenda vyeo, hadhi, heshima kuliko hata utumishi wenyewe tuliopewa?

‘Ugonjwa’ huu wa kutamani hadhi umeshamiri sana. Ni bahati mbaya sana hata taaluma ambazo zilikuwa hazihangaiki na kujitambulisha kwa vyeo vya kitaaluma nao wamejiunga katika homa hii. Siku hizi ni kawaida kabisa kusikia utambulisho ufuatao kutoka kwa watu mbalimbali katika jamii. Huyu atajitambulisha kuwa mimi ni muhandisi (Engineer) fulani; huyu CPA fulani; huyu Dk fulani; huyu wakili msomi fulani; na vinginevyo.

Watu wanaweza kujiuliza kwamba kwani mtu kujitambulisha kwa hadhi yake ya kitaaluma kuna shida gani? Kwamba kama amesomea hicho anachotajimbulisha nacho kuna shida gani? Kwa haraka haraka hakuna shida. Lakini ukizama ndani zaidi kuna shida.

Niwakumbushe kiongozi aliyepata kuvuma katika siasa za Marekani ambaye wengi hawajui kwamba alikuwa mhadhiri wa chuo kikuu. Condoleezza Rice Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani katika utawala wa George W. Bush alikuwa na shahada ya uzamivu, lakini hakuna hata siku moja ambayo tulipata kuona kokote Rice akiitwa kwa jina la Daktari. Katika watumishi wa Umoja wa Mataifa ni wale tu ambao ni madaktari kwa maana ya matabibu ndiyo huitwa kwa vyeo vya daktari. Wengine wote hata kama una shahada za uzamivu ngapi, huwezi kukuta akiandikwa eti daktari fulani.

Kimsingi hadhi za kitaaluma ni sahihi kutambuliwa katika uwanja wa taaluma tu. Sasa sababu hasa ya kujitambulisha hivyo hadharani kwenye jamii ambayo hata kuelewa nini maana ya hadhi hizo, zinaongeza nini kwa jamii husika?

Sasa kama hata wenye haki ya sifa za kitaaluma kwa elimu hizo za uzamivu hawasumbuki nazo, hivi hawa waliozawadiwa kwa heshima tu wanapata wapi ujasiri wa kujiinua mabega na kujiongeza kilemba kwenye majina yao? Ili iwe nini? Je, inaongeza kitu kwao kwa kazi wanazofanya au ni kuwakoga tu wengine?

Katika kiu hii ya kutaka kujiongezea kilemba, wapo watu tunaambiwa wanatumia hata fedha kwa taasisi za elimu za nje kuwapatia hadhi hii. Wakishapata vyeo hivyo vya kitaaluma, basi utasikia wakishupaza shingo siyo tu kujitangaza kama wenye hadhi ya udaktari wa filosofia, bali wakiitukana taaluma kwa ujumla wake.

Tumesikia maneno ya kuudhi ya kukashifu elimu kutoka kwenye vinywa vya baadhi ya wabunge ambao wanajulikana kwamba elimu yao ni ndogo sana kwa kuwa tu nchi hii sifa ya elimu ya mbunge ni kujua kusoma na kuandika tu. Katika kundi hili wapo waliofanikiwa kupewa hizo zinazoitwa PhD za heshima. Wanazitumia kujitambulisha kuliko hata wanavyotumia majina yao asilia. Hawa siyo tu wanakera, bali wanafanya bidii usiku na mchana kudhalilisha elimu.

Ni katika kusikia na kusoma walichofanya Malawi unaelewa kabisa majirani zetu hawa wametupa funzo. Wametusaidia kujitafakari kwamba kama tukiendelea kuendekeza ‘ugonjwa’ huu wa vilemba vya PhD kwa watu ambao hata kuandika majina yao ni muhali, hakika tutakuja kuizamisha nchi kwenye korongo kubwa la maangamizi ya ujinga. Ningekuwa mimi ni miongoni mwa Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) au Wizara yenye dhamana na elimu, hakika nisingesita kufuata nyayo za Malawi kuhusu matumizi ya shahada za heshima nchini kwa sasa. Tujitafakari.

spot_img

Latest articles

Luhemeja ashuhudia zoezi la usafirishaji Ziwa Victoria

KATIBU Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mha. Cyprian Luhemeja akifuatilia...

Mfalme Zumaridi ashikiliwa na Polisi

Na Mwandishi Wetu Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limesema linamshikilia na kumhoji Diana Bundala...

More like this