Na Mwandishi Wetu
Kocha Msaidizi wa timu ya KenGold, Omary Kapilima amesema wamejipanga vizuri kuikabili Yanga, akiamini mchezo utakuwa mzuri na wanategemea kupata alama tatu katika mchezo huo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaochezwa kesho KMC Complex, Dar es Salaam.
Katika msimamo wa ligi hiyo, KenGold inashika nafasi ya 16, ikiwa na pointi 6 baada ya kucheza michezo 16, ikishinda mmoja, sare tatu na kufungwa 12.
Aidha Kocha huyo amesema kati ya wachezaji wapya waliowasajili, Bernard Morrison atakosekana kwa kuwa anamalizia matibabu ili aanze mazoezi.
Naye Kocha Mkuu wa Yanga, Sead Ramovic amesema mchezo dhidi ya KenGold ni mgumu kutokana na aina ya timu wanayokutana nayo lakini ametamba kuwa Wanajangwani hao ni timu bora, imeshinda mataji matatu na inahitaji kushinda tena.
“Tunahitaji kujaribu kucheza kati ya mistari. Tunapaswa kucheza katika nafasi ndogo nyuma ya safu ya ulinzi. Tunahitaji kuwasambaza ili tuweze kupata nafasi kati ya mistari.Kwa ujumla, itakuwa mechi ngumu tena, lakini kama ninavyosema kila wakati, sisi ni timu bora zaidi nchini Tanzania. Tumeshinda taji mara tatu, na tunataka kushinda tena,” amesema.