Safari ya ‘TLP’ ya Lissu ni ipi?

MWAKA 1992 wakati nchi hii ilipoingia katika mfumo wa vyama vingi vya siasa, kulikuwa na hamasa kubwa. Hamasa hii ilitokana na jambo moja kubwa, kwamba sasa uwanja wa siasa uko wazi na huru kwa Watanzania wote. Kwamba kila mmoja sasa anaweza kujishughulisha na siasa bila kulazimika kujiunga na chama kimoja tu kilichokuwako kisheria kabla ya hapo. Aidha, hamasa hii ilikuwa juu kwa sababu sasa wananchi walikuwa na uhuru wa mawazo ya kisiasa, siyo lazima kila mmoja akubaliane na itikadi ya siasa ya ujamaa na kujitegemea ambayo ilikuwa nguzo kuu ya siasa za Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Wananchi walishangilia wakijua kwamba uhuru wao kwa hakika utaheshimiwa na kwamba hakuna atakayejiunga na chama cha siasa kwa kushurutishwa. Mawazo yaliyokuwa yanatawala ni kwamba katika uwanja wa siasa sasa kulikuwa na uchaguzi mkubwa, wa ama mtu kuchagua ajiunge na chama gani, au mtu mwenyewe atafute wale wanaokubaliana kimawazo waanzishe chama cha siasa kwa itikadi wanayoona inafaa.

Hata hivyo, kadri siku zilivyokwenda ile hamasa ya wananchi kuhusu vyama vingi ilizidi kupungua. Leo ni miaka 32 tangu kuasisiwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini. Katika kipindi hiki, taifa limefanya uchaguzi mkuu mara sita; 1995; 2000; 2005; 2010; 2015 na 2020. Katika chaguzi zote hizi kumekuwako na vyama kutoka kundi nje ya chama tawala ambavyo vilionyesha kutoa changamoto kubwa. Vingi bado vimeendelea kusuasua na kubakia vyama vya siasa jina tu.

Kwa mfano, katika uchaguzi mkuu wa mwaka 1995 chama cha NCCR-Mageuzi kilitoa ushindani mkubwa sana dhidi ya CCM; mwaka 2000 na 2005 Chama cha Wananchi (CUF) kilitoa ushindani mkubwa sana dhidi ya CCM katika chaguzi hizo; mwaka 2010 na mwaka 2015 mpira ukahamia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kutoa ushindani dhidi ya CCM. Kwa kifupi ni kwamba  vipo vyama ambavyo havijaunda dola, lakini kila uchaguzi mkuu baada mwingine vimekuwa vikitoa ushindani mkubwa dhidi ya chama tawala, bahati mbaya vinavyotoa ushindani mkubwa huwa vinabadilika kila uchaguzi.

Katika harakati za chaguzi hizi, chama ambacho hakikuunda serikali, lakini kilitoa ushindani mkubwa dhidi ya chama tawala, kila baada ya uchaguzi kumalizika ile kufanya vizuri kwao kumekuwa na gharama kubwa. Viko vyama kama NCCR-Mageuzi na CUF ambavyo kwa kweli vilijijengea heshima kubwa katika kuendesha siasa, lakini baada tu ya uchaguzi mkuu vilikumbwa na migogoro isiyoisha. Migogoro hii ilionekana katika sura ya kugombea madaraka ndani ya vyama hivyo. Kufukuzana na magomvi. Pia kumekuwa na matamanio makubwa ya kuendelea kuteuliwa kwa watu wale wale kuwania urais.  Iliposhindikana kuteuliwa kuwania urais, kushindikana huko kumekuwa fimbo.

Ni fimbo iliyowakimbiza Dk. Wilbroad Slaa na Profesa Ibrahim Lipumba, kila mmoja kwa njia yake baada ya kuona uwezekano wa kuteuliwa kuwania urais mwaka 2015 kwa kofia ya UKAWA haukuwako! Kukimbia kwa viongozi hawa katika vyama vyao kumekuwa na gharama zake.

Kwa kitambo sasa nimekuwa ninafuatilia kauli za viongozi wa Chadema hasa wanaotafuta kuchaguliwa kwenye nafasi mbili za juu, Mwenyekiti wa Taifa na Makamu Mwenyekiti Taifa upande wa Tanzania Bara. Ukisikiliza baadhi ya kauli za watia nia, unavuta pumzi na kujiuliza hivi mtu anayesimama hadharani na kuikana kamati kuu yote ya chama, na yeye akiwa sehemu ya kamati kuu hiyo tangu ichaguliwe, anataka kuuthibitishia nini ulimwengu?

Kwamba yeye ni mtu pekee na wa kipekee katika kamati kuu nzima mwenye maono, msafi, ambaye ana uwezo wa kuongoza peke yake; kwamba ni yeye tu ambaye siyo ‘chawa’ wa mtu; kwamba ni yeye tu ambaye hajawahi kuhongwa; kwamba ni yeye tu binadamu mwenye sifa ya malaika katika chama hicho. Kwa hiyo wengine wote ama ni wezi au wanatumikishwa na watesi wao katika nafasi zao.

Inasumbua akili kidogo kwa mfano kuelewa kiongozi anayetafuta nafasi ya kuongoza chama kama Chadema akishawatuhumu wenzake kwa kukosa uaminifu, akishaeleza kukosa imani na sekretarieti yote, akishaonyesha kwamba ni yeye tu anafaa kuwa kiongozi wa chama hicho kwa sasa kwa sababu wengine wote ni wachafu, hivi akishinda atakwenda kuongoza chama cha namna gani? Hao anaowatuhumu wote, atawafanya nini? Je, ataingia katika fukuzafukuza ili kuwaleta malaika chamani? Au tusema akishindwa atabaki vipi katika chama kichafu kiasi hicho kama anavyokituhumu? Hasira yote hii ni ya nini?

Katika fuatilia yangu kinachoendelea Chadema, kumbukumbu zangu zimenifikisha kwa Mwanasiasa nguli nchini Mabere Nyaucho Marando.  Akiwa Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, Marando alihusika kwa asilimia kubwa kumshawishi Augustino Lyatonga Mrema kujiunga na chama hicho kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 1995 baada ya kujiengua kutoka CCM. Mrema alikubali kujiunga NCCR-Mageuzi kwa masharti mawili; moja, awe ndiye mwenyekiti wa chama na pili, ahakikishiwe kwamba atagombea urais kupitia chama hicho. Marando na wenzake walimkubalia na Mrema akawa ni kiongozi wa kwanza wa serikali mwenye hadhi ya uwaziri kuhamia chama cha upinzani.

Mrema aligombea urais mwaka 1995 kwa tikiti ya NCCR-Mageuzi na kuonyesha upinzani mkubwa dhidi ya mgombea wa CCM, Benjamin Mkapa. Hakuna ubishi kwamba vuguvugu ya kisiasa aliyopeleka upinzani ilisaidia sana kuamsha siasa za ushindani nchini.

Baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu mwaka 1995, kati ya mwaka 1996 na 1997 hali ya hewa ndani ya NCCR-Mageuzi ikaanza kuwa ya wasiwasi mkubwa. Kukawa na mvutano mkubwa kati ya makundi mawili makubwa, moja likiwa nyuma ya Mwenyekiti Mrema na jingine likiwa nyuma ya Katibu Mkuu wakati huo, Marando. Mivutano hii ndiyo ilihitimisha nguvu za NCCR-Mageuzi.

Nakumbuka siku moja Marando akizungumzia mgogoro wa chama chake alisema kuwa chimbuko lake ni Mrema kutaka chama kimteue kuwa mgombea urais mwaka 2000 miaka minne kabla. Mrema alikuwa anaweka sharti hili mwaka 1996. Sharti hili likageuka kuwa kitanzi kwa chama hicho, mengine yaliyokuja kutokea historia inashuhudia.

Katika mfululizo wa mazungumzo yangu na Marando kuna siku alisema: “Hata ukimkata Mrema kichwa sasa hivi, ukatenganisha kichwa na kiwiliwili, kichwa chake kitadai kugombea urais. Anaupenda urais kwelikweli.”

Ninapotafakari vurugu iliyotokea NCCR-Mageuzi kati ya mwaka 1996 na 1999 na hatimaye Mrema kuja kujiengua na kujiunga na Tanzania Labour Party (TLP), ninawaza kugombea urais kunaweza kumfanya mtu kuwa na hisia kali za kutaka kugombea kila wakati, na akiona kuna dalili ya kukosa fursa hiyo ‘panaweza kuchimbika.’

Katika vutanikuvute ya maneno inayoendelea ndani ya Chadema kwa sasa, Makamu Mwenyekiti wake, Tundu Lissu, amesema wazi kwamba Agosti mwaka jana alimwandikia barua katibu mkuu wa chama chake akieleza nia yake ya kutaka kuwania urais mwaka huu. Pia alikuwa anataka kuwania umakamu mwenyekiti kabla ya kubadili nia na badala yake kuutaka uenyekiti. Lissu anataka kuwania urais, ameonyesha nia mapema kama vile ambavyo Mrema alitamani kuidhinishwa mapema mwaka 1996 kuwania urais mwaka 2000.

Kama kuwania urais ni kazi nzuri na yenye kuridhisha nafsi, basi naona nafsi ya Mrema na Lissu ikielea kwenye boti moja. Shida kubwa inayokwenda kutokea ni hii, Mrema hakuidhinishwa na NCCR-Mageuzi na inavyoelekea Lissu hana ukakika wa uteuzi huo, je, katika mazingira kama haya ninaona iko safari inamsubiri kama ile ya Mrema ya kwenda TLP. Je, TLP ya Lissu ni ipi?

spot_img

Latest articles

Wajiteka na kudai pesa kutoka kwa wazazi wao

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam JESHI la Polisi Kanda Maalum Dar es salaam limefanikiwa...

Machifu watano watekwa Nyara Kenya na Al-Shabaab

MACHIFU watano wametekwa nyara siku ya Jumatatu na watu wanaoshukiwa kuwa wanamgambo wa al-Shabaab...

RAIS SAMIA APEWA TUZO

Na Mwandishi Wetu Rais Samia Suluhu Hassan amepokea Tuzo Maalum ya Kimataifa ya The Global...

KENGOLD POINT TATU MBELE YA YANGA

Na Mwandishi Wetu Kocha Msaidizi wa timu ya KenGold, Omary Kapilima amesema wamejipanga vizuri kuikabili...

More like this

Wajiteka na kudai pesa kutoka kwa wazazi wao

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam JESHI la Polisi Kanda Maalum Dar es salaam limefanikiwa...

Machifu watano watekwa Nyara Kenya na Al-Shabaab

MACHIFU watano wametekwa nyara siku ya Jumatatu na watu wanaoshukiwa kuwa wanamgambo wa al-Shabaab...

RAIS SAMIA APEWA TUZO

Na Mwandishi Wetu Rais Samia Suluhu Hassan amepokea Tuzo Maalum ya Kimataifa ya The Global...