MWAKA 2024 unaelekea ukingoni. Zimesalia siku 25 tu kuupa mgongo mwaka huu ambao hakika ulikuwa na hekaheka nyingi sana za uchaguzi. Ulikuwa ni mwaka wa historia kubwa kwani takribani nchi 70 zilifanya chaguzi. Katika bara la Afrika nchi zilizofanya uchaguzi ni pamoja na Afrika Kusini, Ghana, Rwanda, Msumbiji, Namibia na Tunisia kwa kutaja kwa uchache tu. Marekani, Uingereza, Ufaransa, Japan nako kulikuwa na mnyukano mkali.
Kunapokuwa na nchi 70 ndani ya mwaka mmoja zinafanya chaguzi, huo mwaka unakuwa maalumu sana. Kwa kawaida shughuli ya uchaguzi ni muhimu sana kwa uendeshaji wa nchi husika. Tanzania mwaka huu tulikuwa na uchaguzi wa serikali za mitaa ambao ulifanyika Novemba 27. Ni uchaguzi ambao umeibua malalamiko mengi. Mchakato wa uchaguzi huo umeacha maswali mengi juu ya mantiki ya kuendelea kufanyika kwa uchaguzi, utayari wa kufanya uchaguzi na utayari wa kukubali mabadiliko.
Matokeo ya uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2024 yanaonyesha kwamba Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeshinda uchaguzi huo kwa asilimia 99, ushindi huu unatoa picha inayoweza kudhaniwa labda ulikuwa ni uchaguzi wa chama kimoja.
Uchaguzi huu ulikuwa wa aina yake, matokeo haya yanafanana sana na ushindi wa Rais Paul Kagame wa Rwanda ambaye Julai mwaka huu alipata ushindi wa kishindo wa asilimia 99.18. Rwanda nchi ambayo ilikuwa vipande vipande mwaka 1994 kufutia mauaji mabaya kabisa ya kimbari kuwahi kutokea katika nchi hiyo, imekuwa na uwanja uliobanwa sana wa shughuli za kisiasa. Chama tawala cha RPF kinachoongoza nchini hiyo chini ya Kagame, kimekuwa na uwanja mpana wa kufanya siasa, ilhali vyama vingine vikiminywa mbavu.
Tanzania tofauti kabisa na Rwanda, tangu mwaka 1992 mfumo wa vyama vingi iliporejeshwa nchini kisheria, imepiga hatua kubwa za kukuza demokrasia ya vyama vingi. Historia inaonyesha kwamba ustawi na ustahimilivu wa kisiasa katika nchi hii ulifikia kiwango cha juu kabisa mwaka 2015 wakati wa uchaguzi mkuu. Ni uchaguzi ambao kwa mara ya kwanza kambi ya upinzani bungeni ilijikusanyia wabunge 116, miongoni mwao wa majimbo wakiwa ni 71. Ni uchaguzi ambao kwa mara ya kwanza tangu uchaguzi mkuu wa kwanza wa vyama vingi wa mwaka 1995 mgombea wa CCM alishinda uchaguzi chini ya asilimia 60. Ni uchaguzi ambao Rais John Magufuli alishinda kwa asilimia 58 mbele ya Edward Lowassa wa Chadema aliyepata asilimia 39.97.
Hatua hizi chanya za kujenga demokrasia ya vyama vingi nchini pia ilionekana wakati wa uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2014. Uwanja wa siasa ulionyesha kwa kiwango kikubwa haki kutamalaki, ni uchaguzi ambao CCM ilipata ushindi wa wenyeviti wa vijiji 9,378 sawa na asilimia 79.81, vitongoji 48,447 sawa na asilimia 79.83 na mitaa 2,583 sawa na asilimia 66.66.
Hatua hizi ambazo ziliuthibitishia ulimwengu kwamba Tanzania ilikuwa makini katika kujenga demokrasia ya vyama vingi, ndizo zilionyesha kwa mara ya kwanza vyama vya upinzani vikigawana viti vingi zaidi vya wenyeviti wa vijiji, vitongozi na mitaa. Kwa mfano, Chadema walipata vijiji 1,754 sawa na asilimia 14.93; vitongoji 9,145 sawa na asilimia 15.07 na mitaa 980 sawa na asilimia 14.93.
Hata hivyo, baada ya matokeo ya uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2014 na hasa baada ya matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 kuzidi kuonyesha hatua chanya za kuimarika kwa demokrasia ya mfumo wa vyama vingi nchini, dunia ilishuhudia kuporomoka kwa haki za kisiasa nchini kwa kigezo cha uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2019 ulivyofanyika.
Kwa mara ya kwanza mchakato wa uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2019 ukajenga picha kwamba chama tawala kina uhalali hodhi wa kufanya siasa, kama kusimamisha wagombea katika ngazi zote, lakini vyama vya upinzani watapewa fursa kwa hisani. Siyo haki. Ndiyo maana mwisho wa mchakato matokeo yaliyopatikana ni ushindi wa asilimia 99.9 kwa CCM kubeba vijiji 12,260; ikabeba asilimia 100 ya mitaa 4,263 na ikabeba vitongoji 63,970 sawa na asilimia 99.4.
Kugeuka kwa upepo huu wa kisiasa ambao umeineemesha CCM, ambao uliasisiwa mwaka 2019, ukaimarishwa mwaka 2020, wapo waliodhani kwamba kwa kuwa aliyetuhumiwa kuwa muasisi wa uharibifu huo alikuwa ni Marehemu John Magufuli, basi kifo chake kingeenda na uovu huo. Kwa bahati mbaya, yaliyotokea mwaka huu katika uchaguzi wa serikali za mitaa, yamethibitisha wazi kwamba kumbe siyo Magufuli tu, ni mfumo ambao unaakisi kwa mbali kile alichopata kusema aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Bashiru Ally Kakurwa kwamba “chama tawala kitatumia dola kubaki madarakani.”
Hakuna ubishi juu ya nguvu na uwezo wa vyama vya upinzani kwamba haviwezi kuwa na nguvu sawa na CCM kwa sababu nyingi tu. Mojawapo ni kama ambayo alisema Bashiru kwamba unatumia fursa au nafuu ya kushika dola kubakia madarakani, lakini jingine ni rasilimali fedha na miundombinu ambayo vingine vimeangulia kwa CCM kwa sababu za kihistoria, lipo la watumishi wa umma na hata vyombo vya mabavu kuelekezwa na kutumika kuibeba CCM.
Pamoja na CCM kuwa na faida hiyo ya ziada tofauti na vyama vya upinzani, tangu mwaka 2019 mwelekeo ambao chama hiki kimeonyesha unaibua hisia za kuogofya sana kuhusu amani, ustawi, uvumilivu na maelewano ya taifa hili na watu wake. Kwamba kwa kiburi cha nafuu ya kushika dola, chaguzi zinavurugwa mchana kweupe. Vurugu hizi zinabarikiwa na wanaopaswa kuwa wasimamizi huru wa uchaguzi.
Kwa mfano, uovu wa kukata majina ya wagombea wa vyama vya upinzani kwa sababu zisizo na msingi, wasio na sifa za kupiga kura kuandikishwa, kura za wizi kujazwa kwenye masanduku ya kura, mawakala wa vyama vya upinzani kubugudhiwa na vyombo vya usalama, hakika ni mambo ambayo huwezi kuamini yanaweza kufanywa na wafuasi wa chama ambacho hata kabla ya kupigwa kwa kura, tayari kilikuwa kina asilimia 61 ya maeneo ambayo walisimamisha wagombea peke yao tu.
Rais Samia Suluhu Hassan akifungua mkutano wa wadau uliojadili hali ya demokrasia ya vyama vingi vya siasa nchini Tanzania Disemba 15, 2021 alisema maneno yafuatayo: “Tuweke nguvu yetu pamoja kujenga Tanzania mpya yenye kusameheana, yenye kuheshimiana na kufungua kurasa mpya za kwenda na demokrasia yetu Tanzania.” Katika mkutano huo ambao alitangaza kufutwa kwa katazo haramu la kufanyika mikutano ya vyama vya siasa lililokuwa limewekwa na mtangulizi wake, pia alisema: “Tuzike tofauti zetu za nyuma, tufungue kurasa mpya za kuendesha siasa ndani ya nchi. Niko tayari kusikiliza wenzangu. Tushawishiane kusameheana, najua kuna mengi ya kusikiliza pia. Kuna madukuduku, kuna hasira, kuna malalamiko kuna nongwa, yanayotokana na uchanga wetu wa demokrasia. Si mengine, ni uchanga tu wa demokrasia.”
Miongoni mwa madukuduku, hasira malalamiko na nongwa ambayo yalikuwa yametamalaki katika uwanja wa siasa ni pamoja na jinsi uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2019 ulivyoendeshwa ‘kihuni’ pia uchaguzi mkuu wa mwaka 2020. Haya ni mambo ambayo Watanzania na hususan wadau wakuu wa siasa waliamini yalitokea kwa bahati mbaya nchini mwaka 2019 na mwaka 2020, lakini sasa yanapoonekana yametamalaki tena mwaka huu, kile kilicholengwa kuzikwa na kufungua ukurasa mpya, kingali kinasubiriwa.
Wakristo wanatambua kauli aliyotoa Bwana Yesu wakati wa mateso yake kama ilivyoandikwa katika Luka 23:31 “Kwa maana, kama watu wanautendea mti mbichi namna hiyo, itakuwaje kwa mti mkavu?”
Mtu anaweza kujiuliza kwamba maslahi ya kiuongozi na binafsi kwa nafasi za serikali za mitaa ni madogo sana, hivi mwakani katika uchaguzi mkuu wa madiwani, wabunge na urais, hali itakuwaje kwa kuwa huko yapo maslahi makubwa zaidi ya kiuongozi na binafsi. Tuna haja gani sasa ya kufanya uchaguzi kama huu ndiyo mwendo wetu?