Na Tatu Mohamed
ZIARA za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, nchini Uganda na Ethiopia zimefungua fursa za kiuchumi, uwekezaji, ajira na kuimarisha nafasi ya Tanzania katika sekta ya afya ya mama na mtoto barani Afrika.
Katika ziara ya kitaifa nchini Uganda iliyofanyika Novemba 18 na 19, mwaka huu, Tanzania na nchi hiyo zimekubaliana kuharakisha miradi ya kimkakati ya nishati, uchukuzi na biashara, ikiwemo kuifanya Tanga kuwa kitovu cha nishati Afrika Mashariki.
Wakati huo huo, ziara ya kikazi nchini Ethiopia iliyofanyika Novemba 22 na 23, mwaka huu, imeimarisha nafasi ya Tanzania katika ajenda ya afya ya mama na mtoto, baada ya Rais Samia kuzindua Mpango Elekezi wa Afrika wa kuboresha afya ya mama, watoto wachanga, watoto na vijana kwa kipindi cha mwaka 2026 hadi 2030 na kutambuliwa kuwa Kinara wa Umoja wa Afrika katika eneo hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu matokeo ya ziara hizo jana Ikulu jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Bakari Machumu, alisema hatua hizo zimeongeza heshima ya Tanzania kimataifa na kufungua fursa zinazoweza kunufaisha wananchi katika sekta mbalimbali.
Alisema kutambuliwa kwa Rais Samia katika eneo la afya ya mama na mtoto kumetokana na mafanikio yanayoonekana nchini, ikiwemo maboresho ya huduma za afya na juhudi za kupunguza vifo vya mama na watoto.
Alibainisha kuwa baadhi ya nchi, zikiwemo Malawi na Kenya, zimekuwa zikija Tanzania kujifunza mifumo na uzoefu wa nchi katika kuboresha huduma za afya, hatua inayoweza kuifanya Tanzania kuwa kituo cha mafunzo kwa wataalamu kutoka mataifa mengine.

Machumu alisema nafasi hiyo pia inatoa fursa kwa wataalamu wa ndani kushiriki katika majadiliano na maamuzi ya kimataifa, huku ikivutia ushirikiano na uwekezaji katika sekta za afya, teknolojia, ubunifu na viwanda vya dawa.
Alisema kuimarika kwa diplomasia ya Tanzania kunaweza kuvutia mikutano mikubwa ya kimataifa, ambayo itachochea shughuli za hoteli, usafirishaji, utalii na huduma nyingine, hivyo kuongeza mapato na fursa za ajira.
Akizungumzia manufaa ya ziara ya Uganda, Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, alisema viongozi wa Tanzania na Uganda walifanya mazungumzo yenye tija na kufikia makubaliano katika maeneo saba yanayolenga kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi.

Alisema eneo la kwanza ni kuharakisha mpango wa kuifanya Tanga kuwa kitovu cha nishati cha kikanda, utakaohusisha uendelezaji wa miundombinu ya kuhifadhi, kusafirisha na kusambaza mafuta pamoja na kuimarisha huduma za ugavi.
Alisema nchi hizo pia zimekubaliana kuendeleza ushirikiano katika uzalishaji wa mbolea, plastiki, kemikali za viwandani na bidhaa nyingine zinazotokana na mafuta.
“Tunataka Tanzania isiwe nchi ya kupitisha mafuta pekee, bali iwe pia kitovu cha shughuli za kiuchumi zinazohusiana na nishati, viwanda na biashara,” alisema.

Prof. Mbarawa alisema uwekezaji huo utafungua ajira kwa vijana katika ujenzi, uhandisi, uendeshaji wa mitambo, usafirishaji, matengenezo ya vifaa na shughuli nyingine za viwandani.
Alisema eneo jingine ni kukamilisha mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), ambao umefikia asilimia 93.9, akieleza kuwa viongozi hao walipokea taarifa ya maendeleo yake na kusisitiza kazi zilizobaki zikamilishwe haraka ili usafirishaji wa mafuta uanze.
Alisema kukamilika kwa mradi huo kutafungua fursa katika uendeshaji, matengenezo, usalama, usafirishaji na huduma za ugavi, pamoja na kuchochea uwekezaji katika maeneo yanayopitiwa na bomba hilo.
Katika eneo la uchukuzi, alisema Tanzania na Uganda zimefungua hatua za kuunganisha nchi hizo kwa reli ya kisasa kupitia njia ya Isaka, Lusahunga, Murongo, Kikagati hadi Mpondwe yenye urefu wa kilomita 620.
Alisema reli hiyo itakapokamilika itaongeza uwezo wa Bandari ya Dar es Salaam kuhudumia mizigo ya Uganda, kupunguza gharama na muda wa usafirishaji na kufungua fursa za uwekezaji katika vituo vya usafirishaji na huduma za ugavi.
Hata hivyo, alifafanua kuwa mradi huo bado unahitaji kukamilishiwa upembuzi yakinifu, usanifu wa kitaalamu na maandalizi ya kutafuta fedha.

Prof. Mbarawa alisema makubaliano mengine yanahusu kuimarisha usafiri wa majini katika Ziwa Victoria kwa kuboresha miundombinu ya Bandari ya Port Bell nchini Uganda na kuimarisha muunganiko wa reli kutoka bandari hiyo hadi Kampala.
Alisema hatua hiyo itaongeza matumizi ya miundombinu ya Tanzania, ikiwemo reli na Bandari ya Mwanza, na kutoa fursa kwa wananchi wa Kanda ya Ziwa kunufaika na ajira katika shughuli za bandari, usafirishaji wa mizigo, huduma za meli na biashara.
Aliongeza kuwa nchi hizo zimekubaliana kuondoa vikwazo vya biashara na kuanzisha kamati ya pamoja itakayoshughulikia changamoto zinazowakabili wafanyabiashara.
Alisema kuondolewa kwa vikwazo hivyo kutasaidia bidhaa zinazozalishwa Tanzania kupata masoko makubwa zaidi nchini Uganda na kutoa fursa kwa wakulima, vijana wajasiriamali na wazalishaji wa bidhaa.
Katika eneo la nishati, alisema viongozi hao wamekubaliana kuharakisha mradi wa kuunganisha mifumo ya umeme ya kilovolti 400 kupitia Wobulenzi, Masaka, Ibadakuli hadi Shinyanga, hatua itakayosaidia kuimarisha usalama wa nishati na uhakika wa upatikanaji wa umeme.
Kwa upande wa ziara ya Ethiopia, Waziri wa Afya, Mohammed Mchengerwa, alisema kutambuliwa kwa Rais Samia kuwa Kinara wa Umoja wa Afrika katika afya ya mama na mtoto ni hatua muhimu katika kuimarisha ushirikiano wa nchi za Afrika na kutafsiri dhamira ya kisiasa ya viongozi kuwa matokeo yanayookoa maisha.

Alisema mpango elekezi uliozinduliwa unalenga kuimarisha uongozi, kuongeza uwekezaji katika huduma za afya na kuhakikisha huduma bora zinapatikana kwa mama, watoto wachanga, watoto na vijana.
Alisema Tanzania imepiga hatua katika kuboresha huduma za afya ya msingi kwa kujenga na kuboresha zahanati, vituo vya afya na hospitali, hatua iliyosaidia kupunguza umbali wa wananchi kufuata huduma.
Mchengerwa alisema utekelezaji wa mpango huo utajikita katika maeneo makuu ya kuimarisha uongozi na uwajibikaji, kuongeza uwekezaji na kuboresha mifumo ya utoaji huduma kwa kutumia ushahidi unaolenga kuokoa maisha.
Alisema nafasi ya kinara itatumika kuhamasisha nchi wanachama kuweka afya ya mama na mtoto kuwa kipaumbele katika mipango yao, kuongeza uwekezaji wa ndani na kuhakikisha utekelezaji unafuatiliwa katika ngazi za juu za uongozi.
Aliongeza kuwa mpango huo unatoa nafasi ya kuimarisha mafunzo kwa wataalamu wa afya, wakiwemo wakunga, wauguzi na watumishi wengine wanaohusika na huduma za mama na mtoto.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, James Mallya, alisema nafasi hiyo ya uongozi imeanza kuvutia mataifa mengine yanayotaka kujifunza uzoefu wa Tanzania katika kuboresha huduma za afya ya mama na mtoto.

Alisema nchi zilizokwishaonesha nia au kufika Tanzania kujifunza ni pamoja na Lesotho, Malawi, Kenya na Uganda, huku Ghana nayo ikiwa imeiomba Tanzania kuwa sehemu ya kujifunza mafanikio yaliyopatikana nchini.
“Naomba nitaje moja, nchi ya Ghana imeshatuomba kama sehemu ya kujifunza mazuri yaliyofanyika Tanzania,” alisema.
Mallya alisema wakati wa mkutano wa Addis Ababa, Ethiopia, baadhi ya wadau pia walionesha utayari wa kusaidia juhudi za kuboresha afya ya mama na mtoto barani Afrika, akieleza kuwa mmoja wao alitaja uwezekano wa kuchangia takribani dola za Marekani milioni 665.
Alisema Wizara ya Mambo ya Nje inaendelea kuweka mazingira ya kuwaunganisha Watanzania na fursa zilizopo katika nchi mbalimbali kupitia balozi za Tanzania, akizitaka taasisi, wataalamu na wafanyabiashara kutumia fursa hizo.
Naye Mganga Mkuu wa Serikali, Prof. Bruno Sanguya, alisema nafasi hiyo ya kinara inatoa fursa kwa taasisi za serikali, vyuo, hospitali, vyama vya kitaaluma na sekta binafsi kushirikiana na mataifa mengine katika kubadilishana uzoefu na kuimarisha huduma za afya.

Alisema wataalamu wa Tanzania watapata nafasi za kujifunza na kufundisha katika nchi nyingine za Afrika, huku taasisi za ndani zikitarajiwa kupanua uwezo wa kutoa mafunzo yanayotambulika kimataifa.
Alisema fursa hizo zitahusisha pia mafunzo 60 yaliyotajwa katika mpango huo, ambayo yatasaidia kuongeza ujuzi wa wataalamu wa afya na kuimarisha uwezo wa taasisi za ndani.
Prof. Sanguya aliongeza kuwa sekta binafsi inaweza kunufaika kupitia uwekezaji katika uzalishaji wa dawa, vifaa tiba, bidhaa za afya, teknolojia na ubunifu, hatua itakayosaidia kuongeza ajira kwa vijana.
Alisema taasisi za utafiti na vyuo vikuu pia zitapata wigo mpana wa kufanya tafiti na kubadilishana utaalamu na taasisi za mataifa mengine, huku matokeo ya tafiti hizo yakitumika kuboresha huduma kwa wananchi.
Alisisitiza kuwa fursa hizo hazihusu fedha au mafunzo pekee, bali pia kujifunza uzoefu wa Tanzania katika maeneo ambayo imepiga hatua na kuutumia kuboresha huduma katika nchi nyingine za Afrika.
Alisema mafanikio hayo yanapaswa kwenda sambamba na kuimarisha mifumo ya afya nchini na kuhakikisha uzoefu unaopatikana unatumika kutatua changamoto zilizopo katika utoaji wa huduma.
Kwa ujumla, viongozi hao walisema mafanikio ya ziara hizo yatategemea utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa na namna fursa zilizofunguliwa zitakavyotumiwa na taasisi, wafanyabiashara, wataalamu na wananchi, hususan vijana, katika kuongeza uzalishaji, ajira na kipato.


