Mwili wa aliyeuawa wazikwa mara ya pili

Mwili wa Beatrice Ngongolwa (32), umezikwa kwa mara ya pili nyumbani kwao katika Kijiji cha Magunga, wilayani Iringa, huku mtuhumiwa wa mauaji yake Mohamed Salanga (37) akitarajiwa kufikishwa mahakamani kesho.

Beatrice anadaiwa kuuawa kwa kipigo na Salanga, usiku wa Desemba 31 mwaka jana kisha mwili wake kuzikwa ndani ya nyumba waliyokuwa wakiishi, Kijiji cha Skutari, Wilaya ya Kilosa, Morogoro.

Tukio hilo lilibainika Machi 21, 2024 wakati Jeshi la Polisi likiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Shaka Hamud Shaka walipokwenda kuufukua mwili wa Beatrice, Machi 22 2024 na kuupeleka Hospitali ya Rufaa ya Morogoro.

Leo Jumatatu, Machi 25, 2024, baba wa marehemu, Calius Ngongolwa anayeishi mkoani Iringa alikabidhiwa mwili wa mwanaye na kuzikwa. Baba huyo amesema pamoja na binti yake kuuawa kikatili, jambo linalomuumiza ni kukaa zaidi ya miaka miwili bila ya kuwasiliana naye, ambaye ni mtoto wa pili katika familia yake.

Amesema yeye kwa asili ni mwenyeji wa Iringa lakini kwa miaka mingi amekuwa akiishi mkoani Kilimanjaro, hivyo mara ya mwisho alionana na binti yake mwaka 2022, Kilimanjaro. Ngongolwa amesema baada ya hapo hakuwahi kumuona wala kuwasiliana naye tena, hadi Machi 23, 2024 alipopigiwa simu na polisi kwamba binti yake ameuawa na kufukiwa ndani.

Baba huyo amesema mtuhumiwa wa mauaji hakuwa mume wa binti yake na wala hakuzaa naye, bali walikuwa wakiishi tu na katika kipindi chote hakuwahi kusikia madhira wala mateso aliyokuwa akiyapata binti yake na hakujua kama yupo Kilosa anaishi na mtuhumiwa huyo.

“Tangu alipomaliza shule ya msingi mwaka 2005 mkoani Kilimanjaro, Beatrice alikuwa akijishughulisha na ujasirimali na hapo ndipo alipopata kijana mmoja na akazaa naye mtoto wa kike na baadaye walishindwana na akapata mwanamume mwingine ambaye alizaa naye watoto wawili wa kiume,” amesema Ngongolwa.

Ngongolwa amedai kuwa mtuhumiwa huyo aliwahi kufungwa miaka minane jela na wakati huohuo mwanamume wa Beatrice naye alifungwa miaka miwili Gereza la Karanga lililopo mkoani Kilimanjaro na wote walimaliza kifungo chao mwaka 2022.

Alisema wakiwa magereza mtuhumiwa na mwanamume wa Beatrice walikuwa marafiki na hata baada ya kumaliza kifungo mwanamume wa Beatrice alimchukuwa mtuhumiwa Salanga na kwenda kuishi naye nyumbani kwake pamoja na Beatrice na wakiwa nyumbani hapo mtuhumiwa alianza uhusiano ya kimapenzi na Beatrice.

“Mwenzake alimkaribisha nyumbani ili aweze kujitafuta na apate pesa za kurudi kwao Singida, lakini alitumia mwanya huo akaanzisha uhusiano na Beatrice, baadaye mwanamume wa Beatrice alikwenda kijijini kwao Sanya Juu kutafuta vibarua ili akipata amwite rafiki yake (mtuhumiwa) wakafanye,” amesema Ngongolwa.

“Akiwa huko kijijini kwao huku nyuma mtuhumiwa Salanga alimtorosha Beatrice pamoja na watoto wake na kwenda kuishi naye Kilosa na tangu hapo hakupatikana kwenye simu wala hakurudi tena Moshi, mpaka juzi nilipopigiwa simu na kuelezwa kuwa ameuawa na huyo bwana ambaye Mimi wala simfahamu,”amesema.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama amesema mwili huo ulikabidhiwa kwa baba yake baada ya kufanyiwa uchunguzi wa kidaktari na taarifa ya uchunguzi huo itakuwa ni sehemu ya ushahidi mahakamani.

Amesema baada ya kugundulika kwa mauaji hayo haraka Jeshi la Polisi lilianza uchunguzi wake na baadaye lilipeleka jalada kwenye ofisi ya mwanasheria mashitaka mkoa, ambaye yeye ndio mwenye wajibu wa kuandaa hati ya mashitaka kulingana na taarifa ya uchunguzi tulioufanya.

Chanzo: Mwananchi

spot_img

Latest articles

Timu ya Taifa kriketi ya wanawake kusaka tiketi ya kucheza Kombe la Dunia

Na Mwandishi Wetu Timu ya Taifa ya wanawake ya mchezo wa kriketi ya Tanzania inatarajiwa...

Ratiba ya Ligi Kuu msimu wa 2025/26 hadharani, Dabi ya Kariakoo Des 13

Na Winfrida Mtoi Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara(TPLB) leo  Agosti 29, 2025,  imetangaza ratiba...

Gari, Pikipiki, dhahabu, simu janja zaongeza msisimko katika mnada wa Piku

Na Mwandishi Wetu JUKWAA la kidigitali la PIKU linalojulikana kwa kuendesha minada ya kipekee...

TACTIC yaimarisha huduma za usafiri na usafirishaji Manispaa ya Sumbawanga

Na Mwandishi Wetu MRADI wa Uendelezaji Miundombinu ya Miji Tanzania (TACTIC) unaelezwa kuimarisha huduma...

More like this

Timu ya Taifa kriketi ya wanawake kusaka tiketi ya kucheza Kombe la Dunia

Na Mwandishi Wetu Timu ya Taifa ya wanawake ya mchezo wa kriketi ya Tanzania inatarajiwa...

Ratiba ya Ligi Kuu msimu wa 2025/26 hadharani, Dabi ya Kariakoo Des 13

Na Winfrida Mtoi Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara(TPLB) leo  Agosti 29, 2025,  imetangaza ratiba...

Gari, Pikipiki, dhahabu, simu janja zaongeza msisimko katika mnada wa Piku

Na Mwandishi Wetu JUKWAA la kidigitali la PIKU linalojulikana kwa kuendesha minada ya kipekee...