Na Mwandishi Wetu
CHUO Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kimebuni mfumo wa kidijitali unaotumia simu janja (smartphone) kumwezesha mkulima kufahamu kiwango sahihi cha maji kinachohitajika na mazao yake, hatua inayolenga kuongeza uzalishaji huku ikipunguza matumizi yasiyo ya lazima ya rasilimali maji.
Akizungumza katika Maonesho ya Kitaifa ya Wakulima ‘Nanenane’ yanayoendelea jijini Dodoma, mwanafunzi wa mwaka wa tatu katika Ndaki ya Sayansi ya Kilimo na Teknolojia ya Chakula, Damian Kabisi, amesema mfumo huo umebuniwa kusaidia wakulima kufanya maamuzi sahihi kuhusu umwagiliaji kwa kuzingatia hali ya udongo na hatua ya ukuaji wa mmea.
“Mfumo huu unasoma taarifa za udongo pamoja na hatua ya ukuaji wa mmea na kumwelekeza mkulima kiasi halisi cha maji kinachohitajika. Lengo ni kuhakikisha kila tone la maji linatumika kwa ufanisi, hasa katika kipindi hiki cha mabadiliko ya tabianchi,” amesema Kabisi.

Ameongeza kuwa, wakulima wengi bado hutumia maji kwa mazoea bila kujua kiwango kinachohitajika kwa mazao yao, hali inayosababisha upotevu wa maji na kupunguza tija ya uzalishaji.
Kwa mujibu wa Kabisi, matumizi ya teknolojia hiyo yatasaidia kuongeza mavuno kwa kutumia maji kwa ufanisi zaidi, sambamba na kupunguza gharama za uzalishaji zinazotokana na matumizi makubwa ya maji.
“Wakulima wengi hupata mavuno madogo kwa sababu hawana taarifa sahihi kuhusu mahitaji ya maji ya mazao yao. Teknolojia hii inalenga kutatua changamoto hiyo kwa kuwapa taarifa sahihi kwa wakati,” amesema.

Ameeleza kuwa katika hatua za awali, mfumo huo unatarajiwa kuwafikia wakulima wakubwa na taasisi zinazojishughulisha na kilimo cha umwagiliaji, huku mpango ukiwa ni kuusambaza pia kwa wakulima wadogo kupitia mashamba darasa na programu za mafunzo.
Kabisi amesema ubunifu huo ni sehemu ya juhudi za kutumia teknolojia katika kuimarisha kilimo kinachostahimili athari za mabadiliko ya tabianchi na kuongeza tija ya uzalishaji wa mazao nchini.
Amewahimiza wananchi wanaotembelea Maonesho ya Nanenane kufika katika banda la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ili kujionea bunifu mbalimbali zinazotengenezwa na wanafunzi na watafiti wa chuo hicho kwa lengo la kutoa suluhisho kwa changamoto zinazoikabili sekta ya kilimo.


