DIB yawahakikishia wananchi usalama wa amana zao

Na Mwandishi Wetu

BODI ya Bima ya Amana (DIB) imewahakikishia wananchi kuwa fedha wanazoweka kwenye benki zilizosajiliwa nchini zinalindwa kupitia mfumo wa bima ya amana, huku ikiwataka wateja wa benki zilizofilisika ambao bado hawajachukua fedha zao kujitokeza kuzifuatilia.

Akizungumza katika Maonesho ya Kitaifa ya Wakulima ‘Nanenane’ yanayoendelea jijini Dodoma, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa DIB, Lwaga Mwambande, amesema wananchi wengi bado hawana uelewa wa kutosha kuhusu kinga ya amana, hali inayowafanya kuwa na hofu pindi benki inapofungwa au kufutiwa leseni.

Amesema jukumu kuu la DIB ni kulinda amana za wateja wa benki, ambapo kwa sasa kiwango cha juu cha kinga ni Shilingi milioni 7.5 kwa kila mteja katika kila benki endapo benki hiyo itafungwa au kufutiwa leseni na Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

“Unapofungua akaunti katika benki ambayo ni mwanachama wa mfuko wa bima ya amana, tayari fedha zako zinakuwa zimekingwa. Endapo benki itafungwa, DIB hulipa fidia kwa kiwango kinachostahili kwa mujibu wa sheria,” amesema Mwambande.

Amefafanua kuwa fedha zinazotumika kulipa fidia hutokana na michango inayotolewa na benki wanachama wa mfuko huo, ambapo kila benki huchangia asilimia 0.15 ya jumla ya amana zake kwa mwaka.

Amesema fedha hizo huwekezwa katika dhamana za Serikali na vitega uchumi vingine salama ili kuhakikisha mfuko unaendelea kuwa na uwezo wa kulipa fidia wakati wowote inapohitajika.

Mbali na kulipa fidia, Mwambande amesema DIB pia ina jukumu la kuendesha ufilisi wa benki zilizofungwa na Benki Kuu pamoja na kushiriki katika hatua za kuzinusuru taasisi za fedha zinazokabiliwa na matatizo ya kifedha kabla hazijafikia hatua ya kufilisika.

Amesema kuokoa benki inayopitia changamoto mapema ni nafuu zaidi kuliko kusubiri ifilisike, kwani hatua hiyo hulinda fedha za wateja na kupunguza gharama za ulipaji wa fidia.

Kwa mujibu wa Mwambande, kwa sasa DIB inaendesha ufilisi wa benki tisa zilizofungwa katika vipindi tofauti, zikiwemo Greenland Bank, Delphis Bank, FBME Bank, Efatha Community Bank, Mbinga Community Bank, Njombe Community Bank, Meru Community Bank, Covenant Bank for Women na Kagera Farmers Cooperative Bank.

Naye Meneja wa Fedha na Uhasibu wa DIB, Romuli Mtui, amewataka wateja wa benki hizo ambao bado hawajachukua fedha zao kuwasiliana na DIB au kufika katika ofisi zake zilizopo ndani ya majengo ya Benki Kuu ya Tanzania jijini Dar es Salaam na Dodoma ili kufuatilia malipo yao.

Mtui amesema DIB imeanza awamu ya mwisho ya malipo kwa baadhi ya wadai wa benki zilizoko chini ya ufilisi, ikiwemo wateja wa tawi la Tanzania la FBME Bank waliokuwa na fedha zilizozidi kiwango cha fidia ya bima ya amana.

Ameeleza kuwa wateja waliokuwa na amana zinazozidi kiwango kilichokuwa kinakingwa wakati benki zilipofungwa wanapaswa kuendelea kufuatilia mgawanyo wa fedha zinazopatikana kupitia ufilisi wa mali za benki husika.

“Ufilisi ni mchakato wa kisheria unaohusisha ukusanyaji na uuzaji wa mali za benki pamoja na urejeshaji wa mikopo iliyokuwa imetolewa. Kutokana na taratibu za kisheria, ikiwemo mashauri yanayofikishwa mahakamani, mchakato huu unaweza kuchukua muda kukamilika,” amesema.

Ameongeza kuwa bado kuna zaidi ya Shilingi bilioni 2.9 za fidia ambazo hazijachukuliwa na baadhi ya wateja wa benki zilizofungwa, akiwahimiza wahusika kujitokeza kuzidai ili wasipoteze haki zao.

DIB imeyatumia Maonesho ya Nanenane kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kuweka fedha katika benki zilizosajiliwa, namna mfumo wa bima ya amana unavyofanya kazi, pamoja na taratibu za kufuata endapo benki itafungwa au kuingia katika ufilisi.

spot_img

Latest articles

MAKAMU MWENYEKITI UVCCM REHEMA SOMBI (MNEC) APOKELEWA NKASI, AHIMIZA VIJANA KUUNGANISHA SIASA NA UCHUMI

Na Mwandishi Wetu MAKAMU Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Rehema Sombi Omary (MNEC), amepokelewa kwa...

DAWASA YAPELEKA TABASAMU KUNDI MAALUM WIKI YA HUDUMA KWA WATEJA

Na Mwandishi Wetu MAMLAKA ya Majisafi na Usafi wa Mazingira (DAWASA) imehitimisha wiki ya...

TANESCO YANG’ARA TUZO ZA UMAHIRI WA MAWASILIANO KWA UMMA

📌 Yanyakua tuzo nne katika vipengele mbalimbali 📌 Yatambuliwa kwa ubora katika mawasiliano ya kimkakati,...

BRELA YAFUNGUA FURSA YA URASIMISHAJI KWA WADAU WA UCHUMI WA UBUNIFU ARUSHA

Na Mwandishi Wetu WAKALA wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) imeweka kambi ya...

More like this

MAKAMU MWENYEKITI UVCCM REHEMA SOMBI (MNEC) APOKELEWA NKASI, AHIMIZA VIJANA KUUNGANISHA SIASA NA UCHUMI

Na Mwandishi Wetu MAKAMU Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Rehema Sombi Omary (MNEC), amepokelewa kwa...

DAWASA YAPELEKA TABASAMU KUNDI MAALUM WIKI YA HUDUMA KWA WATEJA

Na Mwandishi Wetu MAMLAKA ya Majisafi na Usafi wa Mazingira (DAWASA) imehitimisha wiki ya...

TANESCO YANG’ARA TUZO ZA UMAHIRI WA MAWASILIANO KWA UMMA

📌 Yanyakua tuzo nne katika vipengele mbalimbali 📌 Yatambuliwa kwa ubora katika mawasiliano ya kimkakati,...