Na Mwandishi Wetu
CHUO Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kimesema Tanzania ina fursa kubwa ya kuongeza kipato cha wananchi na kuchochea uchumi kupitia ufugaji wa nyuki wasiodunga, baada ya tafiti zake kubaini aina 12 za nyuki hao wenye uwezo wa kuzalisha asali yenye thamani kubwa katika soko la ndani na kimataifa.
Akizungumza katika Maonesho ya Kitaifa ya Wakulima ‘Nanenane’ yanayoendelea jijini Dodoma, Mwanasayansi wa Nyuki kutoka Idara ya Mazao na Teknolojia ya Ufugaji Nyuki katika Ndaki ya Sayansi ya Kilimo na Teknolojia ya Chakula ya UDSM, Gabriel Mwambogela, amesema tafiti za chuo hicho zimebaini kuwa nyuki wasiodunga si tu wanachangia uzalishaji wa mazao kupitia uchavushaji, bali pia ni fursa kubwa ya biashara kutokana na thamani ya asali yao.
“Lita moja ya asali ya nyuki wasiodunga huuzwa kati ya Sh50,000 na Sh70,000, wakati asali ya nyuki wa kawaida mara nyingi huuzwa kati ya Sh10,000 na Sh20,000. Hii inaonesha kuwa ufugaji wa nyuki hawa unaweza kuwa chanzo kikubwa cha kipato kwa wananchi,” amesema Mwambogela.
Amebainisha kuwa, UDSM imefanya tafiti za kina zilizowezesha kubaini aina mbalimbali za nyuki wasiodunga wanaopatikana katika kanda tofauti za Tanzania pamoja na mazingira yanayowafaa kufugwa kwa njia endelevu.

Mwambogela amesema tafiti hizo pia zimezaa ubunifu wa mizinga maalumu inayorahisisha ufugaji wa nyuki hao, ambao unaweza kufanyika nyumbani, mashambani au hata mashuleni kwa kuwa hawadungi na hawahitaji vifaa maalumu vya kujikinga.
“Nyuki hawa ni rafiki kwa binadamu. Wanaweza kufugwa na wanawake, vijana na hata watoto bila hofu ya kudungwa, jambo linalofungua fursa kwa makundi mengi kushiriki katika shughuli hii ya kiuchumi,” amesema.
Mbali na thamani ya asali yake, amesema nyuki wasiodunga wana mchango mkubwa katika kuongeza uzalishaji wa mazao kwa kuchavusha zaidi ya asilimia 75 ya mimea ya chakula.
“Tukiwatunza nyuki hawa vizuri tutakuwa tumelinda siyo tu biashara ya asali, bali pia uzalishaji wa mazao ya kilimo na usalama wa chakula nchini,” amesisitiza.
Ameongeza kuwa tafiti za maabara zimeonyesha asali ya nyuki wasiodunga ina uwezo mkubwa wa kupambana na bakteria na fangasi, jambo linaloongeza thamani yake katika matumizi ya afya.
Wakati huo huo, mwanafunzi wa mwaka wa tatu wa Ndaki ya Kilimo na Teknolojia na Chakula ya UDSM, Theresia Anthony amesema wanafunzi wa chuo hicho wamefanikiwa kuongeza thamani ya mazao ya nyuki kwa kutengeneza bidhaa mbalimbali za ubunifu.
“Tumetengeneza dawa ya asili ya kikohozi kwa kutumia asali ya nyuki wasiodunga pamoja na viambato vya asili. Pia tuna sabuni za kuogea, sabuni za kunawa mikono na dawa ya kung’arisha viatu zinazotokana na mazao ya nyuki,” amesema Telkia.
Amefafanua kuwa, ubunifu huo unaonesha kuwa mazao ya nyuki yanaweza kutumika kuzalisha bidhaa nyingi zenye thamani ya kibiashara, hatua inayoweza kuongeza ajira kwa vijana na kuinua kipato cha wafugaji wa nyuki.
UDSM imetumia Maonesho ya Nanenane kuhamasisha wananchi kuwekeza katika ufugaji wa nyuki wasiodunga, ikieleza kuwa ni sekta inayohitaji mtaji mdogo, ni rahisi kuifanya na ina soko lenye thamani kubwa ndani na nje ya nchi.


