Na Mwandishi Wetu, Dodoma
MAMLAKA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imekuja na mashine ya kisasa ya kupiga mpunga inayoweza kupunguza kwa zaidi ya nusu nguvu kazi inayohitajika katika kazi hiyo, hatua inayotarajiwa kuongeza tija na kupunguza gharama za uzalishaji kwa wakulima.
Mashine hiyo inaonyeshwa katika Maonesho ya Kitaifa ya Wakulima (Nanenane) yanayoendelea katika Viwanja vya Nzuguni, jijini Dodoma, ambapo imevutia wadau wa sekta ya kilimo kutokana na uwezo wake wa kufanya kazi iliyokuwa ikihitaji watu 10 kwa kutumia watu wanne pekee.

Akizungumza katika maonesho hayo, Mkufunzi Mwandamizi wa VETA Arusha, Franklin Mazala, alisema mashine hiyo inaendeshwa na injini ndogo ya petroli na hutumia takribani lita moja ya mafuta kupiga zaidi ya magunia 10 ya mpunga.
Alisema teknolojia hiyo imelenga kurahisisha kazi za wakulima, kupunguza muda wa uchakataji wa mpunga na kuongeza ufanisi katika uzalishaji.
Mazala aliongeza kuwa mashine hiyo inaweza kuunganishwa na mashine nyingine ya kupepeta mpunga, hatua inayorahisisha zaidi uchakataji wa zao hilo kuliko kutumia njia za kawaida.

Mbali na mashine hiyo, VETA imeonyesha majembe madogo yanayowawezesha wakulima wa bustani kulainisha udongo kwa urahisi, kuruhusu maji na hewa kupenya na hivyo kuongeza uzalishaji.
Aidha, alisema chuo hicho kinaendelea kutekeleza programu ya kuwawezesha vijana inayofadhiliwa na AGRA kupitia mafunzo ya utengenezaji wa zana za kilimo, umwagiliaji wa matone na usindikaji wa mazao baada ya kuvuna ili kuongeza thamani ya mazao.
Mazala alisema wanafunzi wa VETA pia huzalisha bidhaa mbalimbali, zikiwemo siagi zinazotengenezwa kutokana na matunda kama nanasi, machungwa na ndizi, hatua inayowapa ujuzi wa kujiajiri na kuongeza kipato.
Aliwahimiza wakulima na vijana kutembelea banda la VETA katika Maonesho ya Nanenane ili kujionea teknolojia hizo na kupata taarifa kuhusu mafunzo mbalimbali yanayotolewa na chuo hicho.


