Tanzania, Angola zataka kuongeza biashara na uwekezaji

Na Mwandishi Wetu

TANZANIA na Angola zimeahidi kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kwa kuongeza biashara na uwekezaji kati ya nchi hizo mbili, huku zikisisitiza umuhimu wa kutumia fursa zilizopo kuchochea ukuaji wa uchumi na uzalishaji wa viwanda.

Kauli hiyo ilitolewa wakati wa maadhimisho ya Siku ya Angola yaliyofanyika katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (DITF), maarufu kama Sabasaba, ambapo Mamlaka ya Uwekezaji na Kanda Maalum za Kiuchumi Tanzania (TISEZA) iliendelea kunadi fursa za uwekezaji zilizopo nchini.

Akizungumza katika maadhimisho hayo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar, Said Seif Mzee, alisema Tanzania na Angola zimejenga historia ndefu ya ushirikiano wa kisiasa tangu enzi za harakati za ukombozi, lakini sasa ni wakati wa kuimarisha zaidi ushirikiano wa biashara na uwekezaji.

“Ni mara ya kwanza kuwa na Siku ya Angola katika maonesho ya Sabasaba. Angola wametuonesha fursa walizonazo nchini kwao na sisi tumewaonesha fursa zilizopo Tanzania. Sasa ni wakati wa wafanyabiashara na wawekezaji wa pande zote kuzitumia fursa hizo kuongeza biashara na uwekezaji,” alisema.

Alibainisha kuwa kiwango cha biashara kati ya nchi hizo bado hakijafikia matarajio, akieleza kuwa Tanzania inauza bidhaa nyingi zaidi kwenda Angola kuliko inazoagiza kutoka nchini humo.

Kwa upande wake, Balozi wa Angola nchini Tanzania, Domingos De Almeida Da Silva Coelho, alisema urafiki wa muda mrefu kati ya nchi hizo unapaswa sasa kuzaa matokeo ya kiuchumi kupitia biashara, uwekezaji na uanzishaji wa viwanda.

“Angola na Tanzania zina historia ya ushirikiano wa muda mrefu, lakini sasa tunahitaji kuugeuza urafiki huo kuwa fursa za biashara, uwekezaji, ajira na maendeleo ya wananchi wetu,” alisema.

Aliongeza kuwa maonesho ya Sabasaba yameendelea kuwa jukwaa muhimu la kuwaunganisha wawekezaji na wafanyabiashara kutoka mataifa mbalimbali na kufungua masoko mapya.

Katika maadhimisho hayo, TISEZA ilinadi fursa za uwekezaji katika Kanda Maalum za Kiuchumi na Maeneo Maalum ya Uzalishaji kwa ajili ya Mauzo Nje, ikiwahamasisha wawekezaji wa Angola kutumia mazingira rafiki ya uwekezaji yaliyowekwa na Serikali ya Tanzania.

Ofisa Mwandamizi wa Uwekezaji wa TISEZA, Vedasto Kagombora, alisema Serikali imeendelea kuboresha sera na mifumo ya uwekezaji ili kuongeza uwazi, kupunguza urasimu na kufanya Tanzania kuwa kitovu cha uwekezaji katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Alisema wawekezaji wanaowekeza kupitia maeneo maalum ya kiuchumi wanapata mazingira bora ya uzalishaji, miundombinu na fursa za kufikia masoko ya kikanda na kimataifa.

Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya Afritrack, Sebena Yohannes, alisema Maonesho ya Sabasaba yameendelea kuwa jukwaa muhimu la kuwakutanisha wafanyabiashara, wawekezaji na wazalishaji kutoka mataifa mbalimbali, hatua inayochochea ukuaji wa biashara na ushirikiano wa kiuchumi barani Afrika.

Washiriki wa mkutano huo walieleza kuwa sekta za kilimo, viwanda, nishati na usafirishaji zina nafasi kubwa ya kuimarisha ushirikiano wa Tanzania na Angola na kuongeza kiwango cha biashara kati ya nchi hizo mbili.

spot_img

Latest articles

STAMICO YAONGEZA MAPATO HADI SH BILIONI 147.8

Na Tatu Mohamed SHIRIKA la Madini la Taifa (STAMICO) limeongeza mapato yake ya ndani kutoka...

SERIKALI KUANZA UTAFITI WA MADINI ENEO KUBWA LA NCHI KWA KUTUMIA FEDHA ZA NDANI

Ni kupitia mfuko wa utafiti wa Madini ▪️Rais Samia apongezwa kwa dhamira ya kukuza sekta...

NDEJEMBI ARIDHISHWA NA MAENDELEO YA UJENZI WA KITUO CHA UMEME IGANJO, MBEYA

📌 Ujenzi wa kituo hicho umefikia asilimia 93 ya utekelezaji 📌 Aeleza manufaa ya mradi...

WAZIRI MKUU ASISITIZA AFRIKA KUIMARISHA USHIRIKIANO WA USAFIRI WA MAJINI

Na Tatu Mohamed WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema nchi za Afrika zinapaswa kuimarisha ushirikiano...

More like this

STAMICO YAONGEZA MAPATO HADI SH BILIONI 147.8

Na Tatu Mohamed SHIRIKA la Madini la Taifa (STAMICO) limeongeza mapato yake ya ndani kutoka...

SERIKALI KUANZA UTAFITI WA MADINI ENEO KUBWA LA NCHI KWA KUTUMIA FEDHA ZA NDANI

Ni kupitia mfuko wa utafiti wa Madini ▪️Rais Samia apongezwa kwa dhamira ya kukuza sekta...

NDEJEMBI ARIDHISHWA NA MAENDELEO YA UJENZI WA KITUO CHA UMEME IGANJO, MBEYA

📌 Ujenzi wa kituo hicho umefikia asilimia 93 ya utekelezaji 📌 Aeleza manufaa ya mradi...