Na Tatu Mohamed
SHIRIKA la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limesema litaendelea kuimarisha huduma za mawasiliano nchini kwa kutumia Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, kupanua huduma za kidijitali na kuwekeza katika teknolojia za kisasa ili kuongeza mchango wake katika maendeleo ya uchumi wa kidijitali nchini.
Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Moremi Marwa, amesema hatua hiyo imechangiwa na maboresho ya kiutendaji na kibiashara yaliyofanyika ndani ya shirika, ambayo yamewezesha TTCL kuendelea kupata faida na kuboresha huduma kwa wananchi.
Akizungumza na waandishi wa habari Julai 4, 2026, katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), Marwa amesema TTCL inatumia maonesho hayo kuonesha huduma na teknolojia mbalimbali zinazochochea ukuaji wa uchumi wa kidijitali kupitia Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano.

Amebainisha kuwa huduma hizo ni intaneti ya kasi ya juu ya Supersonic Speed, kituo cha FTTX Experience Center, kinachowawezesha wananchi kujionea matumizi ya teknolojia ya nyumba janja (Smart Home), pamoja na huduma za cloud computing kupitia Kituo cha Taifa cha Kuhifadhi Data (National ICT Data Centre – NIDC).
“Kupitia FTTX Experience Center, wananchi wanapata fursa ya kujifunza matumizi ya intaneti katika nyumba janja, ikiwemo mifumo ya usalama, vifaa vya nyumbani vinavyounganishwa na intaneti, michezo ya mtandaoni pamoja na huduma za video na burudani zenye ubora wa juu,” alifafanua.

Aidha, alisema huduma za cloud computing zinazotolewa kupitia National ICT Data Centre zinawawezesha wateja kuhifadhi taarifa zao kwa usalama bila kulazimika kuwekeza gharama kubwa katika miundombinu ya kuhifadhi data.
Akizungumzia utendaji wa shirika hilo, Marwa alisema TTCL ilipata faida ya takribani Sh bilioni 23 katika mwaka wa fedha 2024/2025, huku matokeo ya awali ya mwaka wa fedha 2025/2026 yakionyesha ongezeko la mapato, faida na idadi ya wateja.
“Mafanikio hayo yametokana na maboresho ya kimkakati yaliyofanywa ndani ya shirika kufuatia maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha TTCL linaendeshwa kwa misingi ya kibiashara, kuongeza mapato na kuondokana na utegemezi wa hasara” alisema.

Alisisitiza kuwa TTCL itaendelea kuboresha huduma zake, kupanua wigo wa huduma na kuwekeza katika teknolojia za kisasa ili kuhakikisha Watanzania wanapata huduma za mawasiliano zenye ubora, kasi na gharama nafuu, sambamba na kuharakisha safari ya nchi kuelekea uchumi wa kidijitali.


