Na Mwandishi wetu
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imekamata basi la abiria aina ya Yutong linalomilikiwa na kampuni ya Abood, likiwa linasafirisha kilogramu 101.2 za dawa za kulevya aina ya mirungi katika eneo la Tegeta Kibo, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, amesema basi hilo lenye namba za usajili T 181 EMJ lilikuwa likifanya safari kati ya Mombasa, Kenya na Dar es Salaam, ambapo dawa hizo zilikuwa zimefichwa kwa ustadi ndani ya mfumo wa hewa (AC) wa gari hilo.
Amefafanua kuwa katika tukio hilo, watuhumiwa watano walikamatwa akiwemo dereva wa basi, Ramadhan Mohamed (52), pamoja na kondakta wake, Salma Sanga (26).

Aidha amesema katika operesheni nyingine, DCEA imemkamata Semvua Sangi (31), msimamizi wa hosteli ya wanafunzi iliyopo mtaa wa Nyasa, Kijitonyama, jijini Dar es Salaam, akiwa na pakiti 144 za bangi aina ya skanka zilizopatikana ndani ya chumba chake.
“Mtuhumiwa huyo alikutwa na kifaa maalum cha kuchanganya na kufungasha bangi kwa ajili ya usambazaji,” amesema.
Kamishina Lyimo ameeleza kuwa takwimu zinaonyesha ongezeko la ukamataji wa mirungi, ambapo kwa mwezi Machi 2026 pekee, jumla ya kilogramu 1,267.12 zilikamatwa, sawa na asilimia 64 ya dawa zote zilizokamatwa katika kipindi hicho.
Aliongeza kuwa, katika operesheni zilizofanyika mwezi huo ziliwezesha kukamatwa kwa kilogramu 1,983.31 za dawa za kulevya, sambamba na watuhumiwa 77.

“Katika maeneo mbalimbali nchini, matukio ya ukamataji yaliendelea kushuhudiwa. Mkoa wa Pwani ulikamata kilogramu 419.09 za mirungi zilizokuwa zikielekea Dar es Salaam, huku mkoani Mwanza, kilo 52 zilikamatwa zikiwa zimefichwa kwenye gari aina ya fuso.
“Mkoani Tanga, kilogramu 32.95 za mirungi zilikamatwa zikiwa zimefichwa ndani ya maembe, ambapo mtuhumiwa Seif Omar (38) alikamatwa. Aidha, katika wilaya ya Longido mkoani Arusha, kilo 106.25 zilikamatwa kutoka kwa watuhumiwa waliokuwa wakitumia gari aina ya Toyota Wish,” amesema.
Kwa upande wa mikoa mingine, Kilimanjaro iliripoti kukamatwa kwa kilo 68.3 za mirungi kutoka kwa watuhumiwa wawili, huku mkoa wa Songwe ukikamata kilo 8.2 za bangi aina ya skanka.
Mbali na hilo, DCEA ilikamata pia kemikali bashirifu zenye uzito wa kilogramu 3,012.5 na lita 17,960, ambazo hutumika katika utengenezaji wa dawa za kulevya. Vilevile, vidonge 286 na chupa 1,001 za dawa tiba zenye asili ya kulevya zilikamatwa, zikiwemo aina za alprazolam, midazolam na fentanyl.
“Katika operesheni hizo, vyombo vya usafiri vilivyokamatwa ni pamoja na magari tisa, pikipiki 12 na bajaji moja.
“Mafanikio hayo yametokana na mkakati wetu wa kuelekeza nguvu katika operesheni za mashambani na kudhibiti mitandao ya usafirishaji, pamoja na ukaguzi wa makampuni yanayohusika na kemikali,” amesema.
Hata hivyo, mamlaka hiyo imetoa wito kwa jamii kushirikiana na vyombo vya dola, hasa kwa wamiliki na wasimamizi wa makazi ya wanafunzi, ili kuhakikisha maeneo hayo yanabaki salama na hayageuki kuwa vituo vya biashara haramu ya dawa za kulevya.
Kamishina Lyimo amesisitiza kuwa DCEA itaendelea kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na wananchi ili kuhakikisha wahalifu wote wanachukuliwa hatua kali za kisheria bila kujali hadhi zao.


