“Kama taifa letu lilipata kuwa na bahati ni kuwa na Rais aliyechukia rushwa kama Julius Kambarage Nyerere. Nyerere aliikataa rushwa kwa maneno na vitendo. Kwa maneno na vitendo. Anapokuambia anaichukia rushwa alimaanisha kwamba anaichukia rushwa. Lakini vile vile taifa letu lilipata bahati ya kipekee tulimpata mtu aliyepinga kwa maneno na vitendo matumizi mabaya ya madaraka. Kosa kubwa ambalo viongozi wengi tunalolifanya ni kutumia vibaya imani tunayoipata kutoka kwa wananchi wetu. Ukiaminiwa na wananchi maana yake wanakutarajia utumie madaraka waliyokupa kwa maslahi ya wananchi siyo kwa maslahi yako.”
Hii hapo juu ni nukuu ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Emmanuel Nchimbi wakati wa Kongamano la kuadhimisha miaka 104 ya kuzaliwa kwa Mwalimu Julius Nyerere lililofanyika Dodoma Aprili 11, 2026. Ilikuwa ni siku ya kuzaliwa kwa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Nukuu hiyo ilisambaa kwa kasi katika mitandao ya kijamii kuanzia Jumamosi iliyopita, yaani Aprili 11, 2026. Watu wengi waliijadili. Yalisemwa mengi. Kwa ujumla wake ni kauli ambayo ilivutia hisia za watu wengi wakionyesha kwamba bado ingalipo sauti ya kusemea na kukemea kile kinachowasumbua watu wengi.
Kwamba bado kungalipo na watu wanaothubutu kusema ukweli. Ukweli katika uwazi wake. Ukweli ambao yamkini unaweza kuponya watu majeraha yao. Majeraha ya kukata tamaa, majeraha ya kuumizwa kimwili na kisaikolojia na majeraha ya kupuuzwa kwa kuwa hawana nguvu ya kuzuia madhila ambayo katika miaka ya hivi karibuni yamekuwa ni haki ya raia – karma ya wanadamu. Kuonewa na kupuuzwa.
Katika mijadala kwenye mitandao ya kijamii, baada ya kauli ya Makamu wa Rais Nchimbi kuonekana kuwa ni rejea muhimu ya kukumbusha wenye viti vya mamlaka katika ngazi mbalimbali nini cha kujifunza kutoka kwa muasisi wa taifa hili, ikaibuka taarifa nyingine nzito. Kwamba mojawapo ya chombo cha habari cha umma, kimeondoa maudhui hayo kwenye mitandao yake ya kijamii.
Kwa mwandishi wa habari anayetambua maadili ya kazi yake, habari inaweza kuondolewa kwenye jukwaa husika, au habari inaweza kufutwa, au inaweza kukanushwa na kuomba radhi kama itakuwa imekiuka maadili. Kama haikuzingatia misingi na maadili ya uandishi wa habari. Kufanya hivyo, ni wito wa kitaaluma, kisheria na kiungwana katika kufanya kazi ya uandishi wa habari.
Hata hivyo, habari ya aina ya hotuba ya Makamu wa Rais inapoondoshwa kwenye jukwaa kimyakimya, bila kuelezwa sababu za kufanya hivyo, umma unabaki na maswali mengi, kuna nini?
Katika miaka ya hivi karibuni, kumekuwa na amri nyingi kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa vyombo vya habari juu ya kushusha maudhui ya aina fulani ambayo kwa mtazamo wao yanakiuka sheria na kanuni ya Maudhui ya Mtandaoni.
Ni hakika, akili ya kawaida kabisa haiwezi kukuelekeza kuwaza na kuhitimisha kwamba rejea ya Makamu wa Rais Dk. Nchimbi juu ya haiba ya Mwalimu Nyerere katika utawala, ni jambo linaloweza kufikirika kuwa eti ni ukiukaji wa maadili. Aidha, tafakari yoyote ya kina juu ya alichokisema Makamu wa Rais, hakiwezi kuchukuliwa ni kitu kibaya hata kwa watawala waovu kupindukia. Watawala waovu kupindukia katika dunia hii, hupenda sana kujinasabisha na mambo mema hata kama hawatendi kama hao watu wema. Hii huitwa funika kombe mwanaharamu apite!
Kikubwa zaidi, ujasiri wa kuelekeza au kuamrisha chombo cha habari kifute, kizuie au kisichapishe habari inayofanya rejea ya uadilifu na haiba isiyotiliwa shaka ya Mwalimu Nyerere ni kufuru inatostahili kulaaniwa na kila mwenye kuitakia nchi yetu mema.
Mwalimu Nyerere alikuwa binadamu, tena kama binadamu mwingine. Alikuwa anatambua hilo wakati wote, ndiyo maana kila wakati alikuwa anatafuta wasaa wa kutengeneza mambo yake na Mola wake. Alikwenda kusali kanisani, na hakutaka kusali kwake, au imani ya dini yake, iwe ndiyo imani ya serikali yake au taifa. Alitambua kuwa yeye ni binadamu kama walivyo Watanzania wengine, na kwamba kila mmoja kwa utashi wake afuate imani yake, na dola iheshimu uhuru wa kuabudu wa kila raia.
Pamoja na kutambua ubinadamu wa Mwalimu Nyerere, kizazi chake na hata vilivyofuata katika tawala za nchi hii, vimejifunza na kukumbushana kwa kina msingi wa maadili mema ya kitaifa na kiuongozi ambayo Mwalimu aliyasimamia. Mwalimu Nyerere amekuwa ni rejea, ya kiutawala, kitaaluma na kimaadili katika nyanja zote. Nyerere ni kiongozi aliyepata kukiri hadharani kwamba chini ya utawala wake walifanya makosa. Alikiri kwamba wao walikuwa ni binadamu, kukosea kwa binadamu ni jambo la kawaida.
Mwalimu alitambua kuwa nyakati hubadilika, na mbinu za utawala – hasa kuhusu sera za uchumi nazo hubadilika, lakini aliamini maadili ya utawala, juu ya haki, kupiga vita rushwa, kukataa umasikini, magonjwa na kila aina ya dhuluma dhidi ya raia, kuheshimu ofisi ya umma kuwa mahala patakatifu na taifa kujitegemea ni mambo yasiyoweza kuwekwa rehani hata kama mfumo wa uchumi umegeuka kutoka wa kijamaa kwenda wa kibepari – unyama. Taifa lisilojitegemea litarejeshwa utumwani; taifa lisilokemea rushwa na matumizi mabaya ya ofisi za umma kwa dhati ya kweli kabisa, litatawaliwa na wanyang’anyi wa haki za raia na watu wasiojali ustawi wa jamii na kila mmoja katika nchi.
Tunapofikishana mahali pa kuanza kuogopa rejea ya haiba ya Mwalimu Nyerere kama njia ya kutaka kuturejesha kwenye mstari kama taifa, tunaanza kuulizana maswali magumu, nini kimelipata taifa letu?
Kama kweli taarifa hizi ni za kweli, kwamba chombo cha habari kimeamrishwa kuondoa maudhui yanayomrejea Makamu wa Rais akilenga kuwakumbusha Watanzania hazina ya kimaadili aliyotuachia Mwalimu Nyerere na kwa maana hiyo, tuitumie, basi hali yetu ni ya mashaka kuliko tunavyoweza kufikiri.
Kama sasa taifa limefikishwa hatua ya kuanza kuzuia Mwalimu Nyerere kama rejea ya utawala uliojali watu, uliopinga rushwa, uliokataa matumizi mabaya ya madaraka, uliokataa watu kuonewa siyo kwa Tanzania tu bali ulimwenguni kote, huenda tumekwisha kutumbukizwa kwenye shimo la maangamizi mabaya. Hakuna njia ya kutoka huko, bali ni kukataa kwa nguvu zote tabia hii ya ovyo. Kukubali kupelekwa huko, ni kukubali kunyweshwa sumu inayofisha.


