WIKI iliyopita haikuwa ya habari njema kwa Taifa la Tanzania huko duniani. Pamoja na kile kilichotokea Zanzibar kwa vyama vya ACT Wazalendo na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kusaini Tamko la Pamoja la Maridhiano ya Kisiasa Zanzibar na Ajenda ya Utekelezaji wake, Jumuiya ya Madola nayo imetoka na tamko lake kuhusu Tanzania, ikiiweka katika darubini kali zaidi.
Zanzibar, utiliwaji saini ulifanyika Jumatano Julai 9, 2026 ikulu na hafla hiyo ilishuhudiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Ali Mwinyi, pamoja na marais wastaafu wa Zanzibar, Dk. Amani Abeid Karume na Dk. Ali Mohamed Shein, ambao walikuwa wasuluhishi wa mazungumzo yaliyodumu takribani miezi minane.
Tamko hilo linalenga kuanzisha sura mpya ya maridhiano ya kisiasa Zanzibar na yanajumuisha mambo makuu yafuatayo: Kurejesha na kuimarisha Serikali ya Umoja wa Kitaifa (GNU) kama msingi wa utulivu wa kisiasa; Kufanya marekebisho ya mfumo wa uchaguzi ili kuongeza uaminifu na ushirikishwaji katika uchaguzi; na kufanya mapitio ya Katiba na sheria mbalimbali zinazohusu utawala na siasa.
Mengine ni kuimarisha uhuru na uwajibikaji wa taasisi za umma, ikiwemo mfumo wa haki; kuweka utaratibu wa kudumu wa mazungumzo kati ya vyama vya siasa ili kutatua migogoro kwa njia ya mazungumzo badala ya migongano; Kuimarisha amani, mshikamano wa kitaifa, uvumilivu wa kisiasa na maendeleo ya Zanzibar; na kuweka ajenda ya utekelezaji yenye hatua na utaratibu wa kufuatilia makubaliano hayo.
Kwa mujibu wa viongozi wa pande zote mbili, makubaliano hayo hayakuwa tu tamko la kisiasa bali pia yalikuwa na ajenda ya utekelezaji inayolenga kuhakikisha yaliyokubaliwa yanatekelezwa kwa hatua na kwa ushirikiano wa taasisi husika.
Wakati Zanzibar ikionyesha juhudi za kusaka maridhiano baada ya madhila ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, Kundi la Mawaziri wa Jumuiya ya Madola Linaloshughulikia Hatua za Utekelezaji (Commonwealth Ministerial Action Group – CMAG) katika mkutano wake wa 73 uliofanyika Julai 10, 2026 umetoa tamko kuhusu Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tamko hilo linaikumbusha serikali juu ya utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa yakitokana na matukio ya uchaguzi mkuu wa mwaka jana, hasa matukio ya Oktoba 29, 2025 ambayo yalishuhudia mauaji yasiyoelezeka yaliyofanywa na vyombo vya dola. Mauaji ambayo hayajawahi kushuhudiwa tangu uhuru.
Baadhi ya makubaliano ambayo Jumuiya ya Madola inasukuma yatekelezwe ni pamoja na kuondolewa kwa vikwazo vinavyozuia uhuru wa kukusanyika na kujieleza, pamoja na vikwazo dhidi ya asasi za kiraia na vyombo vya habari; Kufanyika kwa mashauriano kati ya vyama vya siasa ili kufikia makubaliano kuhusu mfumo wa pamoja wa kuelekea uchaguzi ujao; Utekelezaji wa taratibu za kisheria na kiutawala zilizo wazi na zenye uwazi ili kuwawajibisha wahusika wa vitendo vya vurugu na athari zake, pamoja na kutoa fidia kwa waathirika, pale inapofaa.
Mawaziri hao kulingana na taarifa yao iliyotolewa kwa umma, walipokea na kuzingatia mapendekezo ya Mjumbe Maalum (Rais wa Zamani wa Malawi, Profesa Lazarus Chakwera) kuhusu hatua mahsusi zenye muda wa utekelezaji. Mlolongo wa utekelezaji huo ni: Ndani ya siku 30: Kutatua suala la kuwekwa kizuizini kwa Tundu Lissu (Mwenyekiti wa Chadema) kupitia mchakato wa kisiasa na kisheria, na kuwaachia huru wengine wote wanaoshikiliwa kwa sababu tu ya kutumia haki zao za msingi kwa njia ya amani.
Ndani ya siku 60: Kurejesha kikamilifu upatikanaji wa majukwaa ya mitandao ya kijamii na kusitisha vitisho dhidi ya vyombo vya habari na watetezi wa uhuru wa kujieleza; Ndani ya siku 90: Kuitisha jukwaa la kuaminika na shirikishi la vyama vya siasa, likiwa na usuluhishi usioegemea upande wowote, lenye mamlaka ya kujadili mageuzi ya mfumo wa uchaguzi, ushindani wa kisiasa, suala la wafungwa na wanaozuiwa, pamoja na uwajibikaji; na kuanza, bila kuchelewa, uchunguzi huru wa jinai uliopendekezwa na Tume ya Uchunguzi (Tume ya Jaji Chande), ukiwemo uchunguzi wa masuala kama vile fidia kwa waathirika, kwa kuweka vigezo stahiki, vyanzo vya fedha na ratiba za utekelezaji.
Kundi hilo limekubaliana kukutana tena katika kikao maalum Septemba 2026 na limeiomba Serikali yaTanzania kuwasilisha taarifa ya maendeleo kabla ya kikao hicho. Na kwamba katika mkutano wake wa Novemba 2026, CMAG itazingatia kuchukua hatua zaidi endapo maendeleo yanayotarajiwa hayatakuwa yamepatikana.
Masuala haya ni kama maumivu yaliyoganda shingoni mwa mtu. Kwamba Tanzania taifa lililotambulika kama nchi masikini, lakini jeuri kwelikweli katika kutetea haki za wanyonge katika dunia hii, leo hii inashikiliwa bango na jumuiya ya kimataifa kwa sababu ya kuruhusu mambo ya kifedhuli kutendwa na vyombo vya mabavu vya dola dhidi ya raia wake.
Tanzania iliyosifika duniani kote kusimama hadharani bila kupepesa macho, kukataa, kukemea, kutoa rasiliali zake -watu, ardhi, fedha- kuhakikisha kokote uonevu unapokuwapo unakomeshwa, leo hii inajitafuta na kuchutama kwa kuruhusu ufedhuli dhidi ya raia wake. Kibaya zaidi, hata baada ya ufedhuli huo, inashindwa kutekeleza makubaliano ambayo iliafikiana na jumuiya za kimataifa kama Jumuiya ya Madola.
Ni dhahiri ukisikiliza kauli za baadhi ya viongozi wa serikali, tena wenye dhamana kubwa kubwa, ni kama hawajali kwamba sura, hadhi na nafasi ya taifa letu imeshuka mno mbele ya umma na jumuiya ya kimataifa kwa sababu ya matendo ambayo yaliruhusiwa yakatokea Oktoba mwaka jana. Hadi sasa tafakari yoyote ya kina haionyeshi kwamba kuna anayejali kwa dhati ya moyo wake. Bado ubabe na kiburi kisichopimika vimekuwa ni staili ya utendaji wa viongozi wetu. Sura inayojijenga ni kama hakuna anayeonyesha majuto ya kweli.
Picha kubwa inayojitokeza hata bila hao viongozi kutarajia, ni kutokujali na ulevi uliopindukia kwa kujiegemeza kwenye vyombo vya mabavu kuzuia madai na haki za raia.
Yaani wakati CMAG wakikaa kikao Julai 10, mwaka huu kutafakari njia ya Tanzania kutafuta tiba ya matatizo yake, ili kurejesha heshima na hadhi yake inayotambuliwa kama masikini jeuri aliyetikisa dunia katika kupigania haki za wote wanaoonewa na kubezwa katika dunia hii, baadhi ya viongozi wakubwa wenye dhamana ndani ya serikali kwa kauli na matendo yao wanadhihirisha kuwa wao siyo sehemu ya makubaliano hayo. Na kwa maana hiyo hayatatokea.
Kwa mfano, maridhiano hayo yanaweza kutokea vipi, wakati ulevi wa madaraka tu umemtuma Waziri wa Mambo ya Ndani, Patrobas Katambi, kumtaka Inspekta Jenerali wa Polisi, Camillus Wambura kuharamisha mikutano ya kisiasa nchini? Au inapatikana vipi wakati wapo mawaziri wamegeuka kuwa wapelelezi wa jinai, kwa kila mara kueleza umma kwamba wamekamata watuhumiwa wa kutengeneza mabomu, wanunuzi wa petroli, wahamasishaji wa maadamano, walipa fedha za maadamano na mambo kama hayo. Tutaipata wapi tena Tanzania yetu katika mazingira na kwa watu kama hawa?


