Na Mwandishi Wetu
MKURUGENZI Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Lazaro Twange, amesema Shirika hilo linaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati ikiwemo kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, kuimarisha miundombinu ya kusafirisha umeme kwenda Zanzibar na kuanzisha teknolojia mpya zitakazowarahisishia wateja kufuatilia matumizi ya umeme.
Akizungumza baada ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, kutembelea banda la TANESCO katika Maonyesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), Twange alisema walipata fursa ya kumueleza rais hatua mbalimbali zinazochukuliwa na shirika hilo katika kuboresha huduma za umeme nchini.
“Kwa heshima kubwa namshukuru Mheshimiwa Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi kwa kupata muda wa kutembelea banda letu. Tumempa taarifa ya baadhi ya miradi mikubwa tunayotekeleza na hatua tulizofikia katika utekelezaji wake,” alisema.

Alifafanua kuwa, TANESCO inaendelea kutekeleza mkakati wa Serikali wa matumizi ya nishati safi ya kupikia kupitia mpango wa Bill Financing, unaowezesha wateja wapya na waliopo kukopeshwa majiko ya umeme na kulipa gharama zake taratibu kupitia ununuzi wa umeme.
“Mpango huu umepata makubwa. Hii inaonyesha wananchi wameupokea vizuri na tayari tumeshasaini mikataba na sekta binafsi ili kuongeza kasi ya kuwafikishia wananchi majiko haya,” alisema.
Aliwahimiza wananchi kuondokana na hofu ya kutumia umeme kwa shughuli za kupikia, akieleza kuwa teknolojia za sasa zimeboresha majiko ya umeme na kuyafanya kuwa ya gharama nafuu na yenye ufanisi mkubwa kuliko nishati nyingine.

Twange alisema kupitia mradi unaofadhiliwa kwa dola za Marekani milioni 282, TANESCO imetenga dola milioni sita kwa ajili ya kuendeleza matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa kutumia umeme, huku ikishirikiana na Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) katika utekelezaji wa mpango huo.
Aidha, alisema walimueleza Rais Dkt. Mwinyi kuhusu maendeleo ya mradi mkubwa wa kujenga njia mpya za kusafirisha umeme kutoka Tanzania Bara kwenda Zanzibar.
“Tutakuwa na njia tatu mpya za kusafirisha umeme chini ya bahari; moja kutoka Dar es Salaam kwenda Unguja, nyingine kutoka Tanga kwenda Pemba na ya tatu kutoka Kisigino kwenda Mafia. Tunatarajia kumpata mshauri mwezi Agosti na mkandarasi mwezi Januari, huku utekelezaji wa mradi ukitarajiwa kuchukua miezi 20 hadi 22,” alisema.

Alieleza kuwa mradi huo utasaidia kuongeza uwezo wa kupeleka umeme wa uhakika Zanzibar, ambako mahitaji yameongezeka kutokana na ukuaji wa sekta za utalii, viwanda pamoja na ujenzi wa miundombinu ya kijamii.
Katika hatua nyingine, Twange alisema TANESCO inaandaa teknolojia mpya ya Smart House, itakayowawezesha wateja kufuatilia matumizi ya umeme majumbani kupitia simu za mkononi.
“Mteja ataweza kuona kifaa gani kinatumia umeme mwingi na hata kukizima akiwa popote alipo duniani kupitia simu yake. Hii ni teknolojia mpya inayolenga kupunguza malalamiko ya matumizi makubwa ya umeme na kuongeza ufanisi kwa wateja wetu,” alisema.

Pia alisema shirika hilo linaendelea kuhamasisha matumizi ya magari, pikipiki na bajaji zinazotumia umeme sambamba na kuendelea kujenga vituo vya kuchaji magari hayo katika maeneo mbalimbali nchini.
“Sasa tunasema ‘Pika na Uendeshe kwa Umeme’. Baada ya uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali katika uzalishaji wa umeme, ikiwemo mradi wa Julius Nyerere Hydropower, ni wakati wa wananchi kutumia umeme katika shughuli nyingi zaidi za kiuchumi na kijamii,” alisema.
Twange aliwashukuru wananchi wote waliotembelea banda la TANESCO katika maonyesho hayo, akisema maoni na changamoto walizowasilisha zitafanyiwa kazi ili kuendelea kuboresha huduma zinazotolewa na shirika hilo.


