Na Mwandishi Wetu
MFANYABIASHARA na mwekezaji wa Tanzania, Rostam Azizi, ametangaza uwekezaji mkubwa wa kimkakati ndani ya Kampuni ya Nation Media Group (NMG), hatua inayoanzisha zama mpya za Mwafrika kumiliki kiasi kikubwa cha hisa katika moja ya taasisi kubwa zaidi za habari Afrika Mashariki.
Kupitia kampuni yake ya Taarifa Limited, kampuni tanzu ya Taifa Group, Rostam amenunua hisa asilimia 54.08 zilizokuwa zinamilikiwa na Aga Khan Fund for Economic Development kupitia kampuni ya NPRT Holdings Africa Limited. Kampuni hiyo ndiyo ilikuwa inamiliki hisa nyingi katika Nation Media Group.
Baada ya kukamilika kwa makubaliano hayo, Taarifa Limited itadhibiti jumla ya hisa za kawaida 92,618,177, sawa na asilimia 54.08 ya mtaji wa hisa ndani ya NMG, jambo litakalomfanya Rostam kuwa mbia mkuu wa kampuni hiyo.
Akizungumza na wanahabari na wadau wa sekta ya habari jijini Nairobi, Rostam alisema uwekezaji huo unatokana na imani yake ya muda mrefu kuhusu umuhimu wa taasisi imara za vyombo vya habari katika kuimarisha demokrasia, maendeleo ya kiuchumi na ushirikiano wa kikanda katika eneo la Afrika Mashariki.
Alimpongeza Aga Khan IV pamoja na Aga Khan Development Network kwa mchango wao wa miongo kadhaa katika kujenga na kuimarisha vyombo huru vya habari katika Afrika Mashariki, huku akisema NMG ni moja ya taasisi za uandishi wa habari zinazoheshimika zaidi barani Afrika.
Amesisitiza kuwa misingi ya taaluma ya uandishi, uhuru wa uhariri na utumishi kwa umma iliyoasisiwa chini ya uongozi wa Aga Khan itaendelea kuwa nguzo muhimu ya mustakabali wa taasisi hiyo.

“Maadili yaliyoongoza taasisi hii yanastahili kutambuliwa na kuheshimiwa,” alisema Rostam na kuongeza: “Ushirikiano huu unaheshimu urithi huo huku ukiimarisha taasisi kwa ajili ya fursa za enzi mpya ya kidijitali.”
Kadhalika, mwekezaji huyo alibainisha kuwa uhusiano wake na sekta ya vyombo vya habari unachukua zaidi ya miongo miwili kwani alikuwa miongoni mwa wawekezaji waanzilishi wa Mwananchi Communications Limited (MCL) nchini Tanzania, ambayo tangu wakati huo imekua kuwa moja ya taasisi zenye ushawishi mkubwa katika vyombo vya habari nchini.
Mwaka 2003, Rostam alimwalika Aga Khan kuwekeza katika kampuni hiyo, ushirikiano uliolenga kuimarisha uandishi wa habari huru nchini Tanzania wakati ambapo Afrika ilikuwa inapitia kipindi cha mabadiliko makubwa ya kiuchumi na kisiasa.
Baadaye aliuza hisa zake katika Mwananchi Communications mwaka 2006 ili kuruhusu taasisi hiyo kuendelea kupanuka chini ya uongozi wa Aga Khan.
“Tangazo la leo lina maana ya kukamilika kwa mzunguko fulani wa safari yetu,” alisema Rostam. “Zaidi ya miongo miwili iliyopita tulifanya kazi pamoja kujenga taasisi imara za vyombo vya habari Afrika Mashariki. Leo tunaendelea na safari hiyo.”
Alisema uwekezaji wake katika Nation Media Group unaongozwa na misingi mitatu mikuu ambayo ni kuimarisha uandishi wa habari barani Afrika, kuunga mkono ushrikiano wa kikanda na kuimarisha taaluma ya habari (uhuru wa uhariri).
Alisisitiza kuwa vyombo vya habari duniani vinapitia mabadiliko makubwa yanayoendeshwa na teknolojia ya kidijitali, na kwamba taasisi za habari za Afrika zinapaswa kujibadilisha huku zikidumisha uaminifu na uhuru wake. “Jamii inayowekeza katika uandishi imara wa habari inawekeza katika uwezo wake wa kujitambua na kuunda mustakabali wake,” alisema.
Kadhalika alisisitiza umuhimu wa umiliki na uwekezaji wa Waafrika katika taasisi za vyombo vya habari, akieleza kuwa sura inayofuata ya sekta ya habari barani Afrika itaendelea kuundwa na wafanyabiashara na wawekezaji wa Afrika.
Uwekezaji huo pia unaakisi kuongezeka kwa ushirikiano wa kiuchumi na kitaasisi ndani ya ukanda wa Afrika Mashariki kwani NMG inaendesha shughuli zake katika nchi kadhaa za Afrika Mashariki, zikiwemo Kenya, Tanzania, Uganda na Rwanda, na ina nafasi muhimu katika mijadala ya umma katika eneo hilo.
Rostam alisema uwekezaji kama huo unaendana na maono mapana ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), ambayo inalenga kuimarisha zaidi ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kati ya nchi wanachama.
“Afrika Mashariki ni moja ya maeneo yenye nguvu na kasi ya maendeleo duniani,” alisema. “Uchumi wetu unazidi kuunganishwa, tamaduni zetu zinaingiliana na jamii zetu zinaunganishwa na matarajio ya pamoja ya maendeleo,” alisema.
Kuhusu wafanyakazi, Rostam alisema wanahabari na wafanyakazi wa Nation Media Group uwekezaji huo unalenga kuimarisha taasisi hiyo huku ukihifadhi uhuru wa uhariri na viwango vya taaluma.
“Wajibu wetu ni kuhakikisha taasisi imara zinaendelea kulitumikia taifa na maslahi ya umma,” alisema. Aliongeza kuwa ushirikiano huo unaashiria mwanzo wa sura mpya kwa taasisi hiyo na kwa uandishi wa habari katika Afrika Mashariki.
“Simulizi ya Nation Media Group imefungamana kwa kina na historia ya Afrika Mashariki yenyewe,” alisema Rostam na kuongeza:“Leo tunafungua sura mpya katika simulizi hiyo.”
Mbali na sekta ya habari, Rostam pia ni mwekezaji katika sekta mbalimbali za kiuchumi barani Afrika. Alikuwa miongoni mwa wawekezaji wa awali wa Kampuni ya Vodacom Tanzania mwaka 2000 wakati wa mchakato wa kukuza mawasiliano ya simu za mkononi.
Baada ya kujitoa katika uwekezaji huo mwaka 2019, ameendelea kushiriki katika sekta ya mawasiliano ya kidijitali kupitia uwekezaji kwenye muungano wa kampuni zinazoogozwa na Axian Telecom, uliyonunua MIC Tanzania, na kuunganisha mitandao ya zamani ya Tigo na Zantel ambayo sasa inafanya kazi chini ya jina la Yas Tanzania.
Katika sekta ya nishati, kampuni yake ya Taifa Gas imepanua usambazaji wa gesi katika masoko kadhaa ya Afrika ikiwemo Kenya, Zambia na Rwanda.


