Na Mwandishi Wetu
MUFTI na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir Bin Ally ametoa rai dhidi ya vitendo vya kueneza chuki za kidini kupitia mitandao ya kijamii, akiwataka waumini wa dini ya Kiislamu na Watanzania kwa ujumla kupuuza watu wanaochochea migogoro ya kidini.
Ametoa rai hiyo wakati akitoa tamko la maazimio ya kikao cha Baraza la Ulamaa kilichoketi Machi 4, 2026 katika Makao Makuu ya BAKWATA, Dar es Salaam.
Amesema baadhi ya watu wamekuwa wakitumia mitandao ya kijamii kuchapisha ujumbe wa kumtukana Mtume Muhammad (S.A.W), kuukashifu Uislamu na kuibeza dini hiyo, huku akisisitiza kuwa Waislamu wasichokozeke na watu hao.
“Tunaamini wanaofanya hayo si Wakristo wala watu wa dini nyingine, bali ni watu wenye nia ovu ya kutuchonganisha ili tugombane na kutia mtafaruku kati yetu na dini nyingine na jamii kwa ujumla. Niwasihi Waislamu wasiingie kujibizana kwa sababu watu hao wanataka kueneza chuki na fitna dhidi ya dini nyingine,” amesema Sheikh Mkuu.
Aidha, Mufti wa Tanzania amewataka Waislamu wote nchini wakiwemo Masheikh, wanazuoni, maustadh, maimamu na waalimu wa dini kuendelea kuishi kwa upendo, kuvumiliana na kulinda umoja wa kitaifa uliodumu kwa muda mrefu.
Amesisitiza kuwa mafundisho ya Mtume Muhammad (S.A.W) yanahimiza kuishi kwa wema na watu wa dini nyingine.
Katika hatua nyingine Mufti Zubeir amewataka waislamu na watanzania kwa ujumla kuendelea kuchukua tahadhari kufuatia maelekezo ya serikali juu ya magonjwa ya Uviko-19, homa ya ini, dengue na kipindupindu, akiwatakia muendeleo wa mfungo mwema waumini wote wa dini ya Kiislamu wanaoendelea na mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan.


