KATIKA siku za hivi karibuni kumekuwa na matamko ya operesheni mbalimbali za kurejesha uzingatiaji wa sheria, kanuni na taratibu katika matumizi ya barabara kwenye Jiji la Dar es Salaam.
Awali lilianza Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam kuwataka waendesha bodaboda wote na bajaji pamoja na madereva wa magari, kuacha kutumia barabara za Mwendokasi.
Kufuatia tangazo hilo, askari polisi walijaa katika barabara zenye mtandao wa barabara za Mwendokasi – kama Morogoro, Kawawa na Kilwa. Walionekana kwa wingi zaidi katika barabara ya Morogoro ambayo kwa ukweli kuna ukiukaji mkubwa wa matumizi yake. Madereva wa bodaboda na bajaji ambao mimi huwaita ‘mashujaa’ kwa kuwa wana ujasili usiomithilika, wamejitangazia jamhuri yao kwa jinsi wanavyoendesha vyombo vyao vya moto. Utii wa sheria za usalama barabarani ni sifuri kabisa!
Operesheni hii ya polisi ilishuhudiwa wakikamata bodaboda na kuzipakia katika magari ya polisi kupeleka vituoni.
Wiki moja baadaye, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ilitoa tangazo kwa wakazi wa Jiji hilo juu ya uzingatiaji wa matumizi ya barabara katika maeneo ya mjini. Tangazo hilo lilihusu wenye maduka ambao wameamua kupanga bidhaa zao kwenye baraza ambazo ni mahususi kwa ajili ya waenda kwa miguu; walitakiwa kuondoa bidhaa hizo.
Tangazo hilo liliwataka madereva wa bajaji, pikipiki, maguta na magari wanaoegesha vyombo vyao vya moto katika maeneo ambayo hayaruhusiwi, kuviondoa mara moja.
Aidha, tangazo hili liliwagusa ‘watoto pendwa wa wanasiasa’ – wamachinga. Hawa walitakiwa kuondoa vibanda na meza zao za biashara vitu ambavyo vimejengwa kwenye maeneo ya waenda kwa miguu, juu ya mitaro ya maji machafu na maeneo mengine ambayo hawaruhusiwi.
Kwa ujumla operesheni hizi, ya Jeshi la Polisi na ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, ni hatua ya kutaka kurejesha udhabiti wa matumizi ya barabara katika Jiji la Dar es Salaam.
Kwa hali fulani ukisikia matangazo haya unaweza kushawishika kuamini kwamba wenye dhima ya kusimamia matumizi sahihi ya barabara na wanaohusika na usimamizi wa upangaji wa miji, wameamka na sasa wameamua kufanya kazi yao.
Hata hivyo, yafaa kujiuliza kama ni lini Jeshi la Polisi lilipata kwenda likizo, kiasi cha kuachia ‘mashujaa’ wetu kujitangazia jamhuri yao kwa jinsi wanavyoendesha bodaboda na bajaji barabarani? Ni lini kwa mfano askari wa usalama barabarani – trafiki- walipata kukosekana barabarani?
Ni kwa nini kila uchao ‘mashujaa’ wanapita kwenye taa nyekundu mbele ya trafiki na hawafanywi lolote? Ni kwa nini bodaboda hawatii sheria yoyote ya usalama barabarani na hawafanywi lolote na trafiki? Ni kwa nini hawavai kofia ngumu, hawavai viatu, hawavai majaketi ya kuwafanya waonekane (reflectors), na ya kuwakinga dhidi ya upepo, lakini trafiki hawasumbuki nao? Nani amewapa kiburi hiki cha kutokutii sheria na kuona ni sawa tu na kwamba inakubalika?
Wakati Halmashauri ya Jiji ikitangaza operesheni hiyo ya kutaka kushughulika na ‘watoto pendwa wa wanasiasa’ yafaa kukumbushana jambo moja hapa. Kwamba pamoja na kutambua ukweli kwamba umachinga ni shughuli halali ya kujitafutia kipato, upo udhaifu mkubwa wa kitaifa umeachwa mpaka sasa umachinga umekuwa ni janga la kitaifa.
Vivyo hivyo, shughuli ya uendeshaji bodaboda na bajaji pamoja na uhalali wake, uholela wa kutokudhibitiwa kwake umegeuka shughuli hii ya usafirishaji kuwa janga la taifa pia.
Kwa jiji la Dar es Salaam, hakuna hata Halmashauri moja imesalimika na majanga haya. Barabara zote zimevamiwa na wamachinga. Kila uchao barabara nzuri zinazojengwa kwa gharama kubwa ili kurahisisha shughuli za wakazi wa mijini, zinamegwa na kugeuzwa maeneo ya kusimika vibanda vichafu, vilivyochakaa na kusababisha adha kubwa siyo kwa magari tu, bali hata kwa waenda kwa miguu.
Foleni nyingi za Jiji la Dar es Salaam zinasababishwa na uvamizi wa maeneo ya barabara. Mitaro ya maji machafu imefunikwa, vibada vimejengwa juu yake, taka zinajazwa humo kutokana na shughuli za umachinga. Uvunjaji huu wa sheria na taratibu za kuendesha shughuli mijini, haujaanza sasa, umeota mizizi miaka mingi sasa.
Wasimamizi wa jiji na barabara wanaona hali hii kila uchao ikiongezeka kuwa mbaya. Hawafanyi lolote. Hawajisumbui, bila shaka kwa kile kinachoaminiwa kuwa hao ni ‘watoto pendwa wa wanasiasa’ eti ni hazina ya kura, hawaguswi – hivyo wanaweza kufanya lolote.
Wakati hali hii ni sura ya miji yote mikubwa ya nchi hii. Halmashauri zote ama za wilaya, miji, manispaa au majiji, zina uongozi kamili. Wapo wakurugenzi wa halmashauri hizo na maofisa wake; yapo mabaraza ya madiwani yakiwa na wajibu wa kusimamia maeneo yao, lakini hali imeachwa mpaka imegeuka kuwa maafa. Hakuna anayejali.
Inashangaza sana kwamba yanaweza kujengwa masoko au majengo ya wamachinga, lakini wanagoma kwenda huko. Wanabaki pembezoni mwa barabara, mwisho wanavamia barabara, hali inayosababisha usumbufu mkubwa kwa watumiaji wa barabara- magari na waenda kwa miguu. Uvamizi huu ni chanzo kikubwa za msongamano wa magari.
Pamoja na sababu nyingi zinazoweza kutolewa kuhusu kadhia ya wamachinga na bodaboda inayoonekana sasa katika miji mikubwa ya nchi hii, suala la kutokuwajibika ipasavyo kwa wenye mamlaka ya kusimamia mipango miji na matumizi sahihi ya barabara, haliwezi kupuuzwa.
Upuuzwaji huu umejificha kwenye kivuli cha kula rushwa. Trafiki wanakula sana rushwa ndogo ndogo. Sana. Wasimamizi wa shughuli za kibiashara mijini- jinsi wamachinga wanapaswa kukaa, nao wanakula sana rushwa. Hakuna maelezo mengine yoyote yanayoweza kuhalalisha kwa mfano, mkorogano ulioko pale Kariakoo na mitaa yake yote, au Mwenge na mitaa yake yote, au Mbezi Mwisho na mitaa yake yote, kama kweli kungelikuwa na umakini wa kusimamia sheria na taratibu za wamachinga kufanya shughuli zao.
Ofisi ya Waziri Mkuu ndiyo yenye dhima ya kusimamia halmashauri zote za nchi hii, hapo kabla kwa takribani miaka 10 ikiwa ni jukumu la Ofisi ya Rais. Kote huko, Ofisi ya Rais na hata sasa Ofisi ya Waziri Mkuu ni dhahiri hakuna msukumo wowote wa maana wa kutaka kusafisha uchafu huu ambao ni aibu kwa taifa.
Najua wapo wahafidhina watakaosema kwamba haiwezekani kurekebisha hali hii. Hawa ninawakumbusha kurudi nyuma mpaka mwaka 1996 wakati Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ilipovunjwa na kuundwa kwa Tume ya Jiji chini ya Mwenyekiti wake, Charles Keenja. Tujiulize wote, je, Dar es Salaam ilipangwa au la? Je, ilisafishwa au la? Je, wamachinga hawakufanya shughuli zao kwa mpangilio uliokubalika kisheria na kitaratibu. Haikubaliki, hali hii ya Dar es Salaam inachefua.


