Tumeepuka balaa jingine, uadilifu uongoze tiba machungu ya MO29

JUMANNE wiki hii Watanzania walisherehekea siku ya uhuru wa Tanganyika wengi wakiwa majumbani kwao. Waliitikia wito wa kuwataka kusherehekea siku hiyo ya kukumbuka kuondoka kwa utawala wa kikoloni wa Mwingereza Desemba 9, 1961, wakiwa nyumbani bila shaka ili kusaidia kuepusha kile kilichokuwa kinaelezwa kuwa kungekuwa na maandamano yaliyopewa jina la Maandamano ya Desemba 9 (MD9).

Maandamano hayo ambayo yalikuwa yanahamasishwa kwenye mitandao ya kijamii, yanatajwa kuwa ni mwendelezo wa madai ya maandamano mengine yaliyofanyika Oktoba 29 na Oktoba 30, 2025 na kusababisha maafa makubwa nchini. Kama yalivyokuwa maandamano ya Oktoba 29 maarufu kwa jina la MO29, ambayo yalihamasishwa pia kwa njia ya mitandao ya kijamii, haya ya MD9 yalipitia humo humo.

Hata hivyo, miito mbalimbali kutoka kwa watu wa kada mbalimbali- viongozi wa kisiasa na kiroho, ikihamasisha Watanzania kutokuandamana tena, hasa walengwa wakitajwa kama kundi la vijana wa Gen Z (waliozaliwa 1996 hadi 2012); pia kauli za vyombo vya ulinzi na usalama na kutanda kwa vikosi vya ulinzi na usalama katika mitaa mingi ya miji kunaweza kutajwa kuwa vimesaidia kuepusha maandamano hayo. Lakini, kiini cha kutaka maandamano hakijaguswa.

Ni jambo la kumshukuru Mungu kwamba maandamano hayo hayakufanyika tena safari hii. Hii inatokana na ukweli kwamba taifa lingali kwenye msiba, bado halijaanua matanga. Bado watu wanawalilia wapendwa wao. Wapo waliopata walau fursa ya kuwazika wapendwa wao kwa maana walipata miili na kukamilisha taratibu za kiutu ya kusitiri maiti kwa kuwafanyia ibada na kuwazika; wapo waliozika nguo; wapo walioaga picha tu; zipo familia nyingi ambazo itawachukua muda mrefu sana kama siyo maisha yao yote kusahau machungu ya kupoteza wapendwa wao bila hata faraja ya kuona miili yao.

Katika kadhia hii ya Oktoba 29 na 30, 2025 wapo waliopata vilema vya kudumu. Kwa kifupi maisha ya wote walioguswa kwa njia moja au nyingine na maandamano hayo, maisha yao hayatakuwa kama awali tena. Maisha yao yamebadilika moja kwa moja. Wote katika makundi haya wapo kwenye majonzi, wangali wanaomboleza na wataomboleza kwa muda mrefu ujao.

Katika hali kama hii, hakika ingelikuwa ni muhali tu watu wa aina hii kwa ujumla wao kuitikia wito wa maandamano mengine katika kipindi cha muda mfupi sana. Katika kipindi ambacho hata wale waliopata fursa ya kuwazika wapendwa wao, maua kwenye makaburi hayajakauka, au wenye majeraha yao, yangali ‘mabichi’, walioachwa upweke wangali wanatafakari maisha baada ya ama kupoteza watoto, wazazi, walezi au ndugu. Kwa kifupi, taifa bado liko msibani, hata kama watu wamerejea katika maisha yao ya kawaida.

Tunapotafakari hali hii sote tumeshuhudia jinsi ambavyo nia ovu zimetumika kama propaganda ya kupandikiza mgawanyiko mkubwa wa kiimani katika jamii. Tumesikia na kushuhudia kauli zinazotaka kusadikisha umma kwamba maandamano yaliyotokea ni mpango na msukumo wa watu wa imani fulani. Isivyo bahati, kauli za mamna hiyo ama zimepata mwitikio mkubwa kwa wale ambao hakika walipaswa kuzikana, kuzilaani na kuzikaripia kwa kiwango kinachostahili.

Katika baadhi ya hotuba za Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere za kuasa na kuwajengea Watanzania umoja wa kitaifa, alipata kueleza mambo mawili makubwa ambayo ni rahisi sana kutumika kulisambaratisha taifa. Alitaja UDINI na UKABILA. Matukio ya Oktoba 29 na 30, 2025 kwa mara nyingine yametufundisha na kutukumbusha jinsi ambavyo ni rahisi sana kutumbukia katika mparaganyiko kama taifa kama waliopewa dhima ya kutuongoza watajiruhusu kutoa majawabu mepesi katika maswali magumu yanayohusu taifa letu.

Anga ya Tanzania ilisikia mwangwi wa juhudi kubwa za kutaka kugawa taifa hili kwa imani za kidini. Wapo waliofanya bidii kubwa iwe ni kwa kijituma wenyewe au kutumwa, kutuelekeza katika mparaganyiko wa kiimani. Hawa wameachwa wakapanda mbegu mbaya ya udini na mparaganyiko kwa Watanzania. Waliokuwa wanafanya hivyo, waliamini wanasaidia wenye dhima ya kuongoza taifa hili kujiokoa na mtihani ulioko mbele yao wa kutupa uongozi shupavu wa kutuvusha katika msukosuko ambao taifa linapitia.

Isivyo bahati, utetezi huu wa udini badala ya kusaidia umezidi kulizamisha taifa katika mgawanyiko na mtanziko mkubwa. Utetezi huo mwepesi, umekwepa kugusa ama kitovu au kiini cha hali ya kisiasa na kiusalama inayotukabili kama taifa kwa sasa. Utetezi huu umezidi kuharibu. Ni muhimu watawala wetu wakajifunza kwamba utetezi wa udini hauwezi kumsaidia yeyote katika taifa letu. Hauwezi. Anayedhani atamsaidia au kumvusha yeyote kwa utetezi wa kiimani, anamchimbia shimo refu la maangamizi. Kutoka huko itakuwa ni kazi ngumu zaidi. 

Matukio ya kati ya Oktoba 29 hadi Novemba 3, 2025 yalikuwa ni mtihani mkubwa wa taifa letu. Hakuna ubishi kwamba yametuacha pagumu. Yameacha simanzi na makovu makubwa ambayo hata mataifa rafiki wametuasa kwamba yafaa kuyafanyia kazi yaliyotokea ili kujenga taifa imara lenye umoja na mshikamano. Kazi iliyoko mbele ni kubwa na ngumu. Kwa vyovyote haitasaidiwa na udini!

Kutokuwapo kwa MD9 ni faraja kwamba damu nyingine haikumwagika. Kwamba orodha ya vifo (ingawa haijaelezwa hadi sasa waliokufa ni wangapi kwa matukio ya Oktoba 29 na 30, 2025) haikuongezeka. Hata hivyo, ni vema ikaeleweka kwamba kutokuwako kwa maandamano ya D9 siyo kwamba taifa limepona. Hapana. Taifa lingali na machungu, lingali na msiba mkubwa. Machungu bado yapo.

Kutokuwako kwa MD9 kumepunguza kiwango cha mzigo ulioko mabegani mwa watawala wetu juu ya hali ngumu ya kisiasa na kijamii ilivyo nchini ambayo kwa muda mrefu sana ilihitaji utatuzi wa uhakika. Kwamba matukio yaliyotokana na MO29 ni matokeo ya hali hii ambayo imedumu kwa muda wa takribani muongo mmoja sasa. Kujaribu kufumba macho na kujipa matumani hewa kwamba matatizo haya hayapo, haitasaidia kitu.

Kama Watanzania kwa umoja wao waliishi na kujitambua kuwa wao ni ndugu, taifa lao ni la amani na utulivu, basi kama kwa miaka yote hii ya uhuru wao wa miaka 64 sasa hakuna aliyefanikiwa kuwatikisa, swali linalopaswa kuumiza vichwa vya watawala wetu ni hili, ‘Ni nini kipya kimetokea sasa kiasi cha kufanikisha kuwabadili Watanzania?’ Tukiendelea kujipa matumaini ya kufikirika kwamba mchawi wetu anatoka nje, na kwamba sisi siyo chanzo cha kadhia yote hii, tumechagua kubaki kama tulivyo. Na ni hakika kesho yetu ni ya mashaka makubwa zaidi kuliko MO29.

spot_img

Latest articles

Aweso aridhishwa na wingi wa maji Ruvu Juu, aipa Dawasa jukumu

Na Mwandishi Wetu WAZIRI wa maji, Jumaa Aweso amekagua na kujiridhisha na wingi wa...

Prof. Mkenda: Serikali imeendelea kufanya mageuzi makubwa katika sekta ya Elimu

Na Tatu Mohamed WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amesema Serikali...

Jeshi la Polisi latoa onyo wanaondelea kuhamasisha maandamano

Na Mwandishi Wetu JESHI la Polisi nchini limesema  kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi...

Watanzania waaswa kudumisha amani, Umoja na mshikamano

Na Mwandishi Wetu KATIKA kuadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Tanganyika, Watanzania wametakiwa kukumbuka...

More like this

Aweso aridhishwa na wingi wa maji Ruvu Juu, aipa Dawasa jukumu

Na Mwandishi Wetu WAZIRI wa maji, Jumaa Aweso amekagua na kujiridhisha na wingi wa...

Prof. Mkenda: Serikali imeendelea kufanya mageuzi makubwa katika sekta ya Elimu

Na Tatu Mohamed WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amesema Serikali...

Jeshi la Polisi latoa onyo wanaondelea kuhamasisha maandamano

Na Mwandishi Wetu JESHI la Polisi nchini limesema  kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi...