Nani anazuia wahariri kufikiri, kuamua kwa uhuru?

WIKI iliyopita nimejikuta kwenye mashambulizi ambayo sikuyatarajia. Haya yalitoka kwa watu wanaonifahamu kama mwandishi wa habari. Wengi waliniita majina mabaya. Kwamba siku hizi waandishi tumenunuliwa; mwingine akanishutumu kwamba sote sasa tunasubiri tu fursa za uteuzi, ndiyo maana hatuitendei haki kazi ya uandishi wa habari. Kwa kifupi, wote waliozungumza nami, ama ana kwa ana au kwa simu, walikuwa na ujumbe mmoja, waandishi wa habari hatuitendei haki jamii ambayo inastahili kuhabarishwa juu ya mambo yote yanayotokea katika nchi yao, na hata ulimwenguni kote kwa ujumla.

Kisa cha mashambulizi haya yote ni kile alichofanya Balozi Humphrey Polepole. Wiki iliyopita Balozi Polepole alifanya tukio lililoelezwa ni mkutano na waandishi wa habari. Mkutano huu haukuwa wa ana kwa ana na mwandishi yeyote. Wala haukuweza kuelezwa alikuwa yuko wapi, ila tu kupitia mitandao ya kijamii alionekana akizungumza mambo mbalimbali kuhusu Tanzania. Mkutano huu aliufanya baada ya wiki moja kabla kuwa barua yake ya kujiuzulu nafasi ya ubalozi wa Tanzania nchini Cuba na nchi za Karibe (Caribbean), Amerika ya Kati na nchi za Colombia, Venezuela na Guyana, imesambaa katika mitandao ya kijamii. Balozi Polepole alinukuliwa na vyombo vya habari akikiri kuandika barua hiyo.

Hata hivyo, hakukuwa na kauli yoyote kutoka kwa mamlaka za serikali zinazohusiana na uteuzi wake au wasemaji wa serikali, siyo wa ngazi ya wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wala Msemaji Mkuu wa Serikali.

Kwa usuli huo, walionituhumu kwamba waandishi wa habari hawakutimiza wajibu wao, walikuwa wanasumbuliwa na kiwango kidogo cha kuandikwa kwa mkutano wa waandishi wa habari wa Balozi Polepole. Waliamini kwamba mkutano huo haukuandikwa ipasavyo na vyombo vikubwa vya habari nchini.

Tuhuma hizi za ujumla dhidi yetu waandishi wa habari zimenisumbua. Zimenisumbua kwa sababu tunalaumiwa kwa kutokuwajibika kwa mujibu wa taaluma ya uandishi wa habari. Kwamba sasa tumefikia kiwango cha juu kabisa cha kufunika habari. Kwa kimombo huitwa blackout. Yaani sasa tunatuhumiwa kwamba badala ya kusaidia umma upate habari, na ukiwa ni wajibu wetu namba moja wa kiuandishi na kiuhariri, tumeingia kwenye mtego wa kufunika, kuzuia au kuficha habari zisiwafikie wananchi.

Inawezekana hawa wanaotulaumu habari walizopata hazikukidhi kiu yao ya kupata taarifa hizi za mkutano wa Balozi Polepole ambao hata hivyo, haijulikani kwa hakika aliufanyia wapi na alikuwa na nani. Kwa sababu mawasiliano yote yalikuwa kwa mfumo wa mtandao wa intaneti tena kupitia mtandao wa WhatsApp. Maswali yote aliyoulizwa Balozi Polepole ni ama kwa kupiga simu au ujumbe vyote kupitia mtandao wa WhatsApp. Namba ambayo Balozi Polepole aliitaja na kutaka watu waitumie kuwasiliana naye, ilianza na kikoo cha +1.

Nimetafakari sana lawama hizi na ambavyo zinaelekezwa kwetu waandishi wa habari kwa ujumla wetu. Kwamba ni kweli tumeikosea jamii (umma) tunayopaswa kuitumikia kwa kutokuwajibika sawasawa? Je, ni nani hasa wa kupima utendaji wetu kama waandishi wa habari? Je, tunajipima wenyewe au tunapimwa na wengine?

Katika mazungumzo yangu na watu mbalimbali, inaonekana kwamba wanajua alichosema Balozi Polepole. Wanafahamu kwamba Balozi huyu alifanya mkutano na waandishi wa habari, ingawa kwa hali fulani walitarajia kuwaona hao waandishi waliohudhuria mkutano huo. Wanaamini kwamba mkutano na waandishi wa habari kwa njia ya mtandao ulipunguza ladha ya tukio lenyewe. Hawa wanaamini kwamba pamoja na maendeleo ya kidijitali, bado kuwapo kwa waandishi mahususi katika eneo ambalo Balozi Polepole alifanyia mkutano kungesaidia zaidi kupata undani wa yale aliyozumgumza labda kutokana na maswali ya ana kwa ana ambayo angeulizwa.

Tafakari yangu inanisukuma kuamini kwamba kuna uwezekano mkubwa kwamba waandishi wa habari na wahariri wao waliamua kujizuia (self-censorship) katika kufuatilia, kuchakata na hatimaye kuchapisha kwa kina habari za mkutano wa Balozi Polepole. Ninafikia hitimisho hili kwa sababu, katika hali ya kawaida, ni jambo la kushangaza kidogo kama taarifa hizo zimejaa kwenye mitandao ya kijamii itokee mtu mmoja, au taasisi moja nchini iseme kwamba habari hiyo isiandikwe.

Ukimsikia Balozi Polepole anavyozungumza anaelekeza mashambulizi yake ndani ya serikali na chama tawala, CCM. Ni kama anashambulia watendaji fulani fulani, ni kama anawabebesha lawama kwa yote aliyosema na kwa kifupi kwamba ni kama vile utendaji wao ndiyo umemsukuma kujiengua kwenye nafasi ya ubalozi.

Sasa kama kuna lawama kama hizi, je, siyo fursa njema kwa wanaotuhumiwa kuulizwa na kutoa ufafanuzi ili kuandika habari yenye mzania? Kwa mfano, kama yuko mwenye nguvu au mamlaka ya kuzuia kuandikwa kwa habari hizi ambazo zitakuwa zimebeba pia ufafanuzi wa kina kutoka kwa wasemaji wa serikali, kwa kufanya hivyo anakuwa ameisaidia serikali au amezidi kuiumiza?

Ninasema kuiumiza kwa sababu taarifa hizi zimejaa katika mitandao ya kijamii. Kilichochafuliwa ni serikali na Chama tawala. Waliomsikia Balozi Polepole wataendelea kusadiki aliyosema kama hakuna mtu wa ndani ya serikali au upande wa serikali atakayejitokeza na kuweka mambo sawa.

Kama yuko mwandishi wa habari au mhariri miguu yake imeingia ubaridi au ganzi na sasa anafikiri njia ya kuendelea kubaki salama ni kuficha chini ya zulia taarifa mbalimbali zinazotokea katika jamii, ni vema akajua dhahiri kwamba anachokifanya ni kujichimbia kaburi lake la kitaaluma mwenyewe. Ni hakika hatakuwa na manufaa yoyote kwa jamii yake, kwa maana hiyo atakuwa amejiondoa kwenye wajibu wa waandishi wa habari.

Ukisikiliza malalamiko yetu waandishi wa habari na wahariri wetu, tunalia na kulalamika kwamba vyombo vya habari vinakabiliwa na hali ngumu sana ya kiuchumi. Kwa maana hiyo, kama uchumi wa vyombo vya habari ni mbaya, nasi waandishi wa habari uchumi wetu nao unazidi kuwa mbaya siku baada ya siku. Wengi tumegeuka kuwa ombaomba. Ni fedheha kubwa sana!

Kwa bahati mbaya, hatufanyi tafakari ya kina kujua tumefika vipi hapa tulipo leo? Hatufanyi tathmini na kutambua katika hali hii duni, mbaya yenye dhiki kubwa ya kiuchumi, sisi tumechangia kwa kiasi gani? Kwa nini jamii imetutupa mkono? Je, kuna mahali tumepotoka na kusahau wajibu wetu?

Ninataka kuamini hata kama kuna msukumo kutoka sehemu fulani wa kutaka kuzuia habari isiandikwe, kwa mwandishi anayeijua taaluma yake vema na mhariri mwenye kuipenda kazi yake, bado kuna njia na mbinu za kufanya ili umma upate habari za kukidhi kiu yao. Kama hatutaamka na kubadilika, tuhuma kama hizi ambazo safari hii zimenielemea kutokana na kisa cha Balozi Polepole, siyo tu zitaongezeka bali kazi yetu kama waandishi wa habari itafika mwisho. Hakuna mtu atasumbuka tena kufuatilia, kusikiliza, kuangalia au kusoma haya tunayoandika. Tujue sasa tunaandika tanzia ya taaluma yetu kwa mikono yetu wenyewe.

spot_img

Latest articles

Rais Samia: Kituo cha EACLC kitaimarisha uchumi wa Taifa

Na Tatu Mohamed RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema...

Vyombo vya habari vyatakiwa kuripoti habari za Uchaguzi Mkuu kwa usahihi

Na Tatu Mohamed VYOMBO vya habari nchini vimetakiwa kuwa makini katika kuripoti taarifa zinazohusu...

Tamasha la Singeli Agosti 2 wasanii kutoa burudani ya Kimataifa

Na Winfrida Mtoi Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa,...

Maandalizi ya Mkutano Mkuu Maalum UVCCM yamekamilika

Pichani ni Viongozi wa sekretarieti ya Umoja wa Vijana CCM wakikabidhi vifaa mbalimbali wezeshi...

More like this

Rais Samia: Kituo cha EACLC kitaimarisha uchumi wa Taifa

Na Tatu Mohamed RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema...

Vyombo vya habari vyatakiwa kuripoti habari za Uchaguzi Mkuu kwa usahihi

Na Tatu Mohamed VYOMBO vya habari nchini vimetakiwa kuwa makini katika kuripoti taarifa zinazohusu...

Tamasha la Singeli Agosti 2 wasanii kutoa burudani ya Kimataifa

Na Winfrida Mtoi Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa,...