Jaji Mkuu Masaju amepita mlemle

JAJI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, George Mcheche Masaju amemaliza mwezi mmoja ofisini baada ya kuteuliwa kukalia kiti hicho, Juni 13, mwaka huu. Katika kipindi hiki kifupi cha nafasi hii kubwa ya kuongoza Muhimili wa Mahakama, Jaji Mkuu Masaju Alhamisi ya Julai 10, mwaka huu, zikiwa ni siku tatu tu zimesalia atimize muda wa mwezi mmoja ofisini, alifanya ziara katika gereza la Isanga mkoani Dodoma.

Katika ziara hiyo ya kwanza kwake akiwa na wadhifa wa Jaji Mkuu wa Tanzania, alifuatana na viongozi wengine waandamizi wa Mahakama akiwamo Jaji Kiongozi Mustapha Siyani. Akiwa gerezani hapo, Jaji Masaju alisema kuwa mahabusu nyingi zinajaa kwa sababu ya kurundikwa watu wenye tuhuma za makosa ambayo yana dhamana. Alitoa maelekezo kwamba kesi za jinai ambazo zinasikilizwa katika ngazi ya mahakama za Mwanzo nchini kote, watuhumiwa wapewe dhamana.

Alifafanua kuwa mahakimu wa mahakama za Mwanzo wana uwezo na mamlaka ya kutoa dhamana hizo kwa kutoa maelekezo kwa washitakiwa, aidha alisema hata kama mshitakiwa akiruka dhamana, hilo halizuii kesi kuendelea kusikilizwa na kutolewa hukumu. Katika mazingira hayo, mtuhumiwa aliyekimbia na kutiwa hatiani na kuhumumiwa, atatafutwa ili atumikie kifungo chake. Jaji Masaju anatoa maelekezo hayo akitambua kuwa magereza mengi nchini yana msongamano mkubwa wa mahabusu na wafungwa.

Jaji Masaju aliwaagiza majaji wafawidhi nchini kote kutoa mwongozo wa kuzingatiwa katika uendeshaji wa kesi katika suala la dhamana. Alisema kuwa kumekuwa na malalamiko mengi dhidi ya polisi kwamba wanatumia nguvu kupita kiasi katika kuwakamata na kuwahoji watuhumiwa wa kesi mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwashikilia katika vituo vya polisi kwa muda mrefu kinyume cha sheria na taratibu.

Katika ziara hiyo, Jaji Masaju alikumbusha kwamba Tume ya Haki Jinai iliyoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan na kuongozwa na Jaji Mkuu Mstaafu Othman Chande, ilipendekeza: “Itungwe sheria mahususi ya dhamana (Bail Act) itakayoainisha mfumo, mamlaka na utaratibu wote wa dhamana ili kuliweka suala la dhamana kwenye sheria moja na kupunguza mamlaka zinazoshughulikia dhamana.” Tume hii iliundwa na Rais SSH Januari 31, 2023 na ilikabidhi ripoti yake kwa Rais Julai 2023 ikiwa imechambua mambo mengi yanayokwaza utekelezaji wa masuala ya haki jinai nchini.

Ni bahati njema kwamba Jaji Masaju anakumbuka kwamba kuna mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai ya Jaji Chande. Pia ni bahati kwamba Jaji Masaju anaifahamu vema serikali katika kupokea mapendekezo ya ama kufanyika kwa marekebisho ya sheria au kutungwa kwa sheria mpya kulingana na uhitaji wa umma kwa nyakati husika. Ninasema hivyo kwa sababu Jaji Masaju amekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Anaifahamu serikali na kasi yake ya kutenda kazi.

Sasa hivi tupo Julai 2025, yaani miaka miwili kamili tangu Tume ya Haki Jinai ya Jaji Chande ilipowasilisha mapendekezo yake kwa Rais. Hii ilikuwa ni Tume ya Rais, aliiunda mwenyewe ili imsaidie katika uwanda huo wa haki jinai nchini. Ni kwa kiwango gani mawazo na mapendekezo ya Tume yamefanyiwa kazi ni vigumu kueleza. Ila, ni dhahiri yapo mengi ambayo hayajaguswa. Miongoni mwake ni haya ya haki ya dhamana kwa watuhumiwa wa makosa mbalimbali.

Ni kweli kwamba bado nchi yetu inatumia njia ya kuweka watu mahabusu kama adhabu, kukomoana na kuonyeshana ukubwa. Haishangazi kwa mfano raia kukamatwa siku ya Ijumaa na kusota kituo cha polisi, tena nyakati nyingine bila kuandika hata maelezo hadi Jumatatu. Mahabusu imekuwa ni fimbo inayotumiwa na Jeshi la Polisi kutisha na kunyanyasa raia.

Utaratibu huu ndio unasukuma nia ovu ya kuwanyima dhamana watuhumiwa hata wa makosa yanayodhaminika. Hali hii inakwaza pakubwa utoaji wa haki kwa raia. Ni jambo la bahati mbaya kwa mfano, katika mapendekezo ya Tume ya Haki jinai, suala la kuwapo kwa sheria moja kubwa ya kushughulikia dhamana halijafanyiwa kazi kubwa ili walau sasa taifa liwe na sheria ambayo itakuwa ndiyo rejea ya kushughulika na masuala ya dhamana kwa watuhumiwa wa makosa yote.

Unapozungumza upatikanaji wa haki nchini, ni vigumu sana kulikwepa jeshi la polisi. Ni vigumu kwa sababu ndilo lenye wajibu wa kisheria kusimamia utekelezaji wa sheria, upelelezi wa makosa ya jinai, ukamataji wa watuhumiwa na hatimaye kuwasilisha taarifa za upelelezi kwa mamlaka za kufungua mashitaka mahakamani. Kwa mantiki hii, kama kuna sehemu ya kuanzia kusafisha ili masuala ya haki jinai nchini yakae sawa, Jeshi la Polisi ndiko kunakotakiwa kila kitu kianzie katika kusafisha, kurekebisha na kuunda upya chombo hicho ili kifanane na dhima ya kuundwa kwake.

Jeshi la Polisi Tanzania Juni mwaka huu, lilipata sifa kemkem kutoka kwa Amiri Jeshi Mkuu, Rais SSH. Mara ya kwanza ilikuwa ni Juni 9, 2025 alipohudhuria mahafali ya maofisa wa Polisi, Kurasini Dar es Salaam, na mara ya pili ilikuwa ni Juni 27, mwaka huu siku Rais anahutubia Bunge ikiwa ni hotuba ya kuvunja Bunge la 12 jijini Dodoma. Sina nongwa na sifa za rais kwa Jeshi hilo. Pamoja na sifa ambazo zilimiminwa kwa polisi, malalamiko yanayoibuka kila wakati dhidi ya utendaji wao, yanazidi kuhuisha mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai kwa Rais juu ya mwenendo wa chombo hiki chenye dhamana ya kulinda uhai na mali za raia.

Kwa mfano, Tume kuhusu Jeshi la Polisi pamoja na mambo mengine ilisema kwamba lifanyiwe tathmini ya kina itakayowezesha Jeshi hilo kufanyiwa maboresho makubwa na kuundwa upya ili kuondoa kasoro za kiutendaji zilizopo; libadilishwe kisheria, kimuundo na kifikra na kuwa Polisi Tanzania (National Police Service ili kutoa taswira kuwa Jeshi la Polisi ni chombo cha kuwahudumia wananchi; Kubadilisha mitaala ya mafunzo na mtazamo wa askari wa Jeshi la Polisi ili kutoka katika dhana ya ujeshi (police force) kwenda dhana ya kuhudumia wananchi (police service); liboreshe mfumo wa ndani wa kushughulikia malalamiko ya wananchi; na liimarishe huduma za Intelijensia ya jinai na Polisi Jamii na kuanzisha programu za kuisogeza zaidi kwenye jamii.

Haya ni mambo makubwa ambayo ukimsikiliza kwa makini Jaji Mkuu Masaju ni kama anakumbusha kwamba ipo kazi, kipo kiporo mahali fulani cha kufanyiwa kazi kwa haraka kama taifa letu linataka kushughulika na utoaji wa haki kwa raia wake, hususan watu wanaotuhumiwa kwa makosa mbalimbali. Pengine ni bahati mbaya mapendekezo makubwa na muhimu ya kubadili hali ya mambo iliyozoeleka nchini huchukuwa muda mrefu sana. Jaribu kujiuliza juu la lile pendekezo la Wizara ya Sheria na Katiba la kutoa kwanza elimu ya katiba kwa miaka mitatu, kabla ya kuanza tena kwa mchakato wa katiba mpya. Ni hakika, hadi leo kwa vigezo vya Wizara hiyo, pendekezo hilo lilitolewa Agosti 2023, miaka miwili sasa, elimu hiyo bado haijaanza kutolewa. Ndiyo maana ni sahihi kusema kwamba bado tuna safari ndefu katika uwanja wa kutoa haki kwa raia.

spot_img

Latest articles

Arajiga kuchezesha CHAN

Na Mwandishi Wetu Mwamuzi  wa Tanzania  ,Ahmed Arajiga  ni miongoni  mwa waamuzi wa  wameteuliwa  kuchezesha michuano ya  CHAN yanayotarajiwa kuanza kutimua vumbi...

Rais Samia atoa  wito utekelezaji Dira ya Taifa 2050, asema Dk. Mpango hatapumzika

Na Mwandishi Wetu Rais Samia Suluhu Hassan, amezindua rasmi Dira ya Taifa ya Maendeleo ya...

Rostam: Hatuwezi kufanikiwa kwa kuwatenga wafanyabiashara wa ndani na kutegemea wageni

Na Mwandishi Wetu MFANYABIASHARA maarufu na mwakilishi wa sekta binafsi, Rostam Azizi, amesema kuwa...

Ally Kamwe akiri kuvutiwa na Tshabalala

Na Mwandishi Wetu Ofisa Habari wa klabu  ya Yanga Ally  Kamwe amesema licha ya kuwa yupo upande...

More like this

Arajiga kuchezesha CHAN

Na Mwandishi Wetu Mwamuzi  wa Tanzania  ,Ahmed Arajiga  ni miongoni  mwa waamuzi wa  wameteuliwa  kuchezesha michuano ya  CHAN yanayotarajiwa kuanza kutimua vumbi...

Rais Samia atoa  wito utekelezaji Dira ya Taifa 2050, asema Dk. Mpango hatapumzika

Na Mwandishi Wetu Rais Samia Suluhu Hassan, amezindua rasmi Dira ya Taifa ya Maendeleo ya...

Rostam: Hatuwezi kufanikiwa kwa kuwatenga wafanyabiashara wa ndani na kutegemea wageni

Na Mwandishi Wetu MFANYABIASHARA maarufu na mwakilishi wa sekta binafsi, Rostam Azizi, amesema kuwa...