Na Mwandishi Wetu
Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuzindua rasmi Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050, Julai 17, 2025 kwenye Ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma.
Taarifa hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo wakati akizungumza na wahariri na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam na kueleza kuwa uzinduzi wa Dira 2050 unafuatia hatua muhimu ya Baraza la Mawaziri kuidhinisha dira hiyo pamoja na kuridhiwa kwa Dira 2050 na Bunge la Tanzania.
Amesema Dira 2050 imejengwa kutokana na maoni ya wananchi waliokusanywa kupitia vikao vya wadau kutoka sekta zote ikiwemo vyama vya siasa, mashirika ya kiraia, wanataaluma, waandishi wa habari na makundi ya kijamii, ili kuleta maono ya pamoja kuhusu mustakabali wa taifa.

“Dira hii siyo ya chama chochote, ni dira ya watanzania wote. Vyama vya siasa vinaelewa kwamba ilani zao zinapaswa kuakisi dira hii. Hatutarajii kuona chama chochote kikitunga ilani inayokwenda kinyume na Dira ya Taifa,” amesema Prof. Mkumbo.
Amefafanu kuwa Dira hiyo itaongoza maendeleo ya nchi kwa zaidi ya miongo miwili ijayo, chini ya usimamizi wa marais watakaoingia madarakani hadi mwaka 2050.

“Lengo letu ni kuhakikisha mjadala wa kisiasa unajikita katika namna ya kufika kwenye malengo ya maendeleo, na si kuhusu kwenda wapi kwa sababu tumeshaamua, kama taifa, tunataka kwenda wapi,” ameeleza.
Amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha pato la Taifa linafikia la Dola za Kimarekani trilioni moja, huku mtu mmoja mmoja kuwa na wastani wa kipato cha sh. 1,500,000 kwa mwezi, ikiwa ni sehemu ya mwelekeo mpya wa taifa kuelekea uchumi wa kati wa juu unaojikita katika matumizi bora ya rasilimali, teknolojia na maarifa.


Prof. Mkumbo ameeleza kuwa Tanzania imejifunza mengi kutoka kwa nchi mbalimbali ikiwamo Botswana, hasa namna ilivyofanikiwa kunufaika na sekta ya madini kwa maendeleo ya kitaifa.
Amebainisha kuwa Botswana imeweza kufikia hatua ya pato kubwa la mtu mmoja mmoja kwa sababu ya usimamizi mzuri wa rasilimali, jambo ambalo Tanzania imelichukua kama funzo muhimu katika utekelezaji wa Dira 2050.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile amesisitiza umuhimu wa vyama vya siasa nchini kuwa na ilani za uchaguzi zinazokidhi malengo na mipango ya Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025/50 ili kuleta mtazamo wa pamoja kwa Tanzania.

“Tumejipanga kutangaza habari zinazohusu Dira ya Taifa ya mwaka 2025/50 na siyo kwa chama chochote cha siasa pekee, maana baadhi ya watu wanaweza wakachanganya kuwa Dira ni ya CCM. Vyama vyote vinavyotaka kuandika ilani zao vinapaswa kuakisi dira hii na sisi hatutasita kuandika habari zao,” amesema Balile.
Pia, Balile amesema kuna haja ya Idara ya Habari ya Tume ya Taifa ya Mipango kuwa na bajeti ya kutosha katika kuwezesha utoaji wa elimu na uelewa kwa wananchi kuhusu Dira 2050, ili kuhakikisha jamii inaelewa malengo ya Taifa kufikia mwaka 2050.