Na Tatu Mohamed
BARAZA la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura CCC) limesema kuwa wananchi wana haki ya kudai fidia wanapocheleweshewa kuunganishiwa maji kwa siku saba za kazi baada ya kulipia.
Hayo yamebainishwa jana jijini Dar es Salaam na Mjumbe wa Kamati ya Watumiaji kutoka Wilaya ya Ubungo, Jane Joseph, katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba).

“Kwa mujibu wa Kanuni ya 34(3) ya Kanuni za Ubora wa Huduma za Majisafi na Usafi wa Mazingira za mwaka 2020, mteja ana haki ya kulipwa Sh15,000 endapo hatapata huduma ndani ya siku saba za kazi baada ya malipo. Na kila siku ya ziada, atapaswa kulipwa Sh5,000,” alisema.

Aidha aliwahamasisha wananchi kufika katika banda la Ewura CCC ndani ya Sabasaba ili kujifunza zaidi kuhusu haki zao, namna ya kufuatilia fidia, na kujiepusha na matumizi ya huduma zisizo na ubora unaotakiwa.

Naye Afisa Uelimishaji na Uhamasishaji wa Ewura CCC, Lugiko Lugiko, alibainisha kuwa wananchi wengi hawafahamu haki zao, na hivyo kukosa fidia zinazostahili.
Alisisitiza kuwa mteja anapaswa kuchukua hatua kwa kuandika barua rasmi kwa mtoa huduma akitaja tarehe ya malipo, changamoto iliyojitokeza, pamoja na kuambatanisha ushahidi kama risiti.

“Watu wengi hudhani fidia italetwa bila kuchukua hatua. Tunasisitiza kuwa haki huambatana na wajibu. Lazima ufuate utaratibu wa kisheria ili kulindwa,” aliongeza Lugiko.
Kwa mujibu wa Sheria ya Ewura Sura ya 414, kifungu cha 30, Ewura CCC imepewa mamlaka ya kuwalinda na kuwatetea watumiaji wa huduma, kusambaza taarifa muhimu na kutoa elimu kwa umma ili kuwajengea uwezo wa kudai haki zao.