Na Mwandishi Wetu
Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, amewaambia wasuasi na viongozi wa chama hicho kuwa wajiandae kwani akitoka ni mchakamchaka.
Lissu amezungumza hayo leo Julai 1, 2025 wakati alipokuwa anawasalimia wafuasi na viongozi hao waliofika katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kufuatilia kesi ya uhaini inayomkabili kiongozi huyo.
“Jiandaeni hii biashara tunaimaliza siku hizi hizi, nikitoka ni mchakamchaka, nikitoka tuko barabarani, hayo ya yule Jaji mwingine tutajuana nayo,” amesema Lissu muda mchache baada ya kesi yake kuahirishwa, huku akiwatania wafuasi hao kwa kusema “Jamani mie mfungwa,”

Awali akiwa mahakamani hapo, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Franko Kiswaga, Lissu aliomba mahakama hiyo kuwa kama upelelezi ama ushahidi haujakamilika basi aachiwe huru kwa sababu mara ya mwisho waliambiwa upelelezi umekamilika na jalada lipo wa DPP.
Amesema kuwa anaiomba mahakama hiyo isiahirishe kesi kwa sababu hakuna sababu ya msingi, kwani mara ya mwisho waliambiwa upelelezi umekamilika na wangepewa taarifa ya uamuzi.

Lissu alihoji kwamba inamchukua muda gani DPP kusoma faili la kesi hiyo hali ya kuwa yeye ni msomi wa sheria na kama upelelezi ama ushahidi haujakamilika basi aachiwe.
Akizungumzia maisha yake ya Gerezani kwa sasa mambo yamekaa vizuri, anapata huduma za kiroho na pia anakutana na mawakili wake na anafanya mazoezi.
”Baada ya ku-demand hapa kesho yake Mkuu wa Gereza aliniita akaniambia utakaje, Jumapili inayofuata nilipata Padri kwenye selo yangu nikapata huduma ya kiroho.Bwana jela akasema kingine, nikamwambia nataka nifanye mazoezi mahali salama, akasema na hilo limepita kwa sasa nafanya mazoezi uwanjani napata hewa halisi.
“Na mawakili wangu kwa sasa tunakutana kwenye kachumba kamoja hivi, mambo yamekaa vizuri kabisa, lakini sisemi naenda vizuri ili niendelee kukaa mule gerezani, hapana gerezani sio pazuri,” amesema Lissu.
Kwa upande wa Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga amesema kuwa kutokana na shauri hilo kuwa na maslahi kwa umma ndio maana wameomba ahirisho ili waje kusema kwamba jalada limefikia hatua gani.Pia DPP amefanya jitihada za kutosha kuhusu hiyo licha ya kuwa na majukumu mengi.
Kutokana na mvutano huo kwa kisheria, Hakimu Kiswaga ameahirisha kesi hiyo hadi Julai 15, 2025.