Na Mwandishi Wetu
RAIS Mstaafu wa awamu ya nne Jakaya Mrisho Kikkwete anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Kongamano la Kitaifa la Sheria la Chama cha Mawakili wa Serikali (PBA) kesho jijini Dar es Salaam katika ukumbi wa kitaifa wa Mikutano wa Mwalimu Nyerere na kuhudhuriwa na Mawakili wa Serikali kutoka maeneo mbalimbali nchini.
Katika Kongamano hilo kutaendeshwa mada mbalimbali ambazo zitawasaidia mawakili kutoa elimu za kisheria kwa wananchi na watanzania kwa ujumla.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam na waandishi wa habari juu ya Kongamano hilo, Rais wa PBA, Bavoo Junus amesema kuanzishwa kwa Chama cha Mawakili wa Serikali ni kuunganisha mawakili wa Serikali kwa pamoja kutokana na kuwepo katika maeneo mbalimbali ya nchi.

“Kwa mujibu wa ibara ya 151 ya Katiba inasema Serikali maana yake ni Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ,Halmashauri na Serikali za Mitaa pamoja na mtu yoyote anayetekeleza mamlaka kwa niaba ya Serikali.
“Mawakili wa Serikali wametapakaa hadi ngazi ya chini, hivyo lengo letu ni kuwaunganisha Mawakili hawa ambao wanatoka maeneo mbalimbali na taasisi mbalimbali kuwaleta pamoja kujadili masuala yetu,”amesema.
Amefafanua kuwa, lengo la Chama chao ni kuwa Jukwaa la Kutoa elimu na mafunzo kwa wananchi kwa sababu Serikali inawajibika kwa wananchi.

“Sisi ni Mawakili wa Serikali lakini sisi ni Mawakili wa Umma, Chama chetu kinajukumu la kuhakikisha elimu katika masuala mbalimbali ya kisheria hususan yanayogusa maslahi mapana ya Taifa,” amesema.
Amesema Chama kinajukumu la kutoa elimu hususan katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu Oktoba mwaka huu hivyo kimejipanga kutoa elimu kuhusu mambo mbalimbali yanayohusu uchaguzi Mkuu.

“Tunaelekea katika uchaguzi mkuu,chama kimeona ni busara kuandaa Kongamano hili ambalo lengo kubwa ni kutoa elimu kwa wananchi na watanzania kuhusu mambo mbalimbali yanayohusu uchaguzi Mkuu.
“Tanzania ndio Baba na ndio Mama,kuna maisha baada ya Uchaguzi ipo haja ya wadau wote na wananchi kwa ujumla kuweza kutambua hivyo ndio maana tumeamua kuweka mada mbalimbali ikiwemo hiyo ya elimu ili mwisho wa siku uchaguzi ufanyike kwa amani,” amesema.
Amesema tofauti mbalimbali za watu zisisababishe uvunjifu wa amani ya nchi kwani mambo yanayowaunganisha ni mengi ambayo ni makubwa na mengi kuliko yale yanayowatofautisha.

“Tutofautiane katika itikadi za Kisiasa ,Dini lakini sio kwa mambo ya amani,Mimi nimeona Mume yupo chama hiki na mke yupo chama kingine ila maisha yanaendelea au huyu Dini hii na yule dini hii na maisha yanaendelea.
“Haya ni mambo madogo kuliko mambo yanayotuunganisha ni makubwa na mazito kuliko yanayotutofautisha,” amesema.
Kongamano hilo litakalobeba kaulimbiu “Demokrasia kwa vitendo: Sheria, Wajibikaji na Uchaguzi Mkuu 2025”, linalenga kuwajengea wananchi uwezo wa kuelewa sheria zinazoongoza chaguzi pamoja na kuwahamasisha kushiriki katika utunzaji wa amani na mshikamano wa kitaifa kuelekea uchaguzi mkuu.