Trump katukumbusha tena, sisi siyo watu

KAMA kuna jambo la kujifunza juu ya Uafrika na Afrika ni uamuzi wa juzi wa Rais wa Marekani, Donald Trump, kuamua kuwapa hifadhi wanaodaiwa kuwa wakulima wa Kiafrikana wa Afrika Kusini kwa kile kinachodaiwa kwamba wanabaguliwa nchini mwao.

Jumla ya Waafrikana 59 walipokewa nchini Marekani Jumatatu wiki hii kama wakimbizi baada ya Rais Trump kuwapa shufaa hiyo akidai kwamba wamekuwa wakionewa sana nchini kwao kwa kuwa ni kundi la walio wachache.

Hatua hizi za Trump zinafanana na nyingine za namna hiyo ambazo zimepata kuchukuliwa na marais wengine wa nchini hiyo. Hata hivyo, tofauti iliyopo sasa ni kwamba shufaa hii inatolewa katikati ya kipindi ambacho utawala wa Rais huyo umekuwa na sera katili dhidi ya wahamiaji wengine, hasa weusi, ambao wameondoshwa kwa maelfu katika nchini hii baada ya kuzingirwa na wanausalama kama vile wawindaji wawindavyo digidigi mbungani.

Juzi Trump akiongea huku anaonyesha sura ya huruma dhidi ya Waafrikana hao, alisema wamebaguliwa sana na kuporwa mashamba yao na utawala wa Afrika Kusini. Katika sura hiyo, Trump alionyesha ni kiongozi mwenye huruma na anayependa haki kwa watu wanaonyanyaswa kokote duniani.

Ingawa ni jambo jema kunyoosha mkono kuwatia moyo wanadamu wowote wanaoonewa kokote duniani, ni vema unyooshaji mkono huo usiwe wa kibaguzi. Pengine ni vema kukumbusha kwa kifupi sana Waafrikana ni nani hasa. Hili ni kundi la watu weupe kutoka Ulaya hasa nchi za Udachi, Ufaransa na Ujerumani ambao waliingia Afrika Kusini katika karne ya 17 na 18 na kuweka makazi yao eneo la sasa la Cape, nchini Afrika Kusini. Hawa baadaye walikuja kuongoza Afrika Kusini chini ya sera za ubaguzi wa rangi mkali kwa miongo mingi, tangu mwaka 1948.

Wakiwa ndiyo waasisi wa ubaguzi wa rangi, pia walijitwalia kila kitu katika ardhi ya Afrika Kusini, waliendesha uchumi wote, kama madini na viwanda. Miliki ya ardhi yote kiasi cha zaidi ya asilimia 72  inayofaa kwa kilimo imo mikononi mwa watu hao huku wakiwa ni asilimia saba tu ya wananchi wote wa Afrika Kusini. Kwa wastani weusi ambao ni wengi nchini humo wanamiliki si zaidi ya asilimia 10 ya ardhi yote ya nchi hiyo.

Utawala wa kibaguzi wa Afrika Kusini chini ya Waafrikana ambao kimsingi ndiyo hasa Makaburu, walipojitangazia Jamhuri mwaka 1961, waliendesha sera za kibaguzi dhidi ya weusi wengi kwa kiwango ambacho hakijawahi kutokea chini ya jua. Walitenda vitendo vingi vya kinyama ambavyo makala hii moja hatoshi kueleza. Kwa kifupi watu hawa ambao Trump anawalilia leo, hawajawahi kulipa uovu, unyama, ufedhuli na kila aina ya ubaya waliowatenda watu weusi katika nchi yao.

Uhuru wa waliowengi uliopatikana mwaka 1994 baada ya kufikia ukomo wa utawala wa ubaguzi wa rangi na Nelson Mandela kuchaguliwa kuwa Rais wa kwanza wa Afrika Kusini ya wote, weusi, wa rangi, weupe, ulifungua milango ya maisha mapya kwa kila raia wa Afrika Kusini, wakiwamo hawa Waafrikana ambao mpaka sasa bado wanaamini katika siasa za kibaguzi. Wengi wameendelea kulilia mfumo wa kibaguzi, wakiamini kwamba wanapaswa kuishi kivyao katika Afrika Kusini mpya na kuachiwa kuendelea kumiliki kila kitu kama hapo zamani wakati wa sera za ubaguzi wa rangi.

Ni bahati mbaya sana kwamba kwa madhila yote waliotendwa watu weusi Afrika Kusini na Waafrikana hawa, watu aina ya Trump siyo tu nyakati zile hawakufungua mdomo kulaani, bali walilala kitanda kimoja na watesi hawa. Walibariki unyama wote na kuendelea kushirikiana nao, kana kwamba matendo yao maovu dhidi ya binadamu wengine hayakuwahuzunisha.

Tangu Afrika Kusini iingie chini ya utawala wa wengi ikiongozwa na chama cha African National Congress (ANC) imeweka mikakati ya kurekebisha mgawanyo wa rasilimali za nchi. Ardhi ni mojawapo ili kugawanywa kwa wote. Sera hii haijakubalika na Waafrikana ambao wamejitwalia kuwa na haki ya kumiliki ardhi yote ya Afrika Kusini peke yao. Wanatamani Waafrika Kusini wengi, hasa weusi, waendelee kuwa manamba. Hawataki kabisa kusikia sera yoyote ya kugawana ardhi, hata kama ni pamoja na kulipwa fidia. Mgawanyo wa ardhi kwao ni unyanyasaji, ni kubaguliwa, ni kuonewa, ni jambo lisilokubalika.

Watu wa aina ya Trump wanatuonyesha kwa mara nyingine tena jinsi mtu mweusi asivyostahili heshima, utu, kumiliki uchumi wake hata katika ardhi yake asilia ya kuzaliwa. Anawalilia hawa wachache wa Afrika Kusini tena katikati ya sekeseke lake la kuwasaka wahamiaji walioko Marekani, hasa weusi, ambao wameshiriki kujenga uchumi wa nchi hiyo, wakifanya kazi zote za ovyo ambazo weupe wanabeua mdomo na kuzipa mgongo, huku zikiwa na umuhimu wa kipekee kwa ustawi wa uchumi wa nchi hiyo.

Ni Weusi hawa wamekuwa nguzo kubwa ya nguvu kazi katika kazi za mashambani, kazi za kwenye mahoteli na migahawa ambazo weupe hawataki hata kuzigusa, ijapokuwa zinachangia pakubwa uchumi wa taifa hilo.

Ni bahati mbaya kwamba Weusi hawa hawajajitakia kukaa Marekani bila kuwa na vibali rasmi, wamejikuta kuwa mateka wa mfumo mgumu na wa kibaguzi wa kutambua mchango wao katika kujenga uchumi wa taifa hilo. Kwa wastani inamchukuwa hadi miaka 25 kufanikiwa kupata vibali rasmi vya kuishi kihalali nchini humo. Hii haijalishi unafanya kazi kama punda, Januari hadi Desemba. Haijalishi kwamba rekodi yako ya kuishi nchini humo ni ya kutukuka isiyokuwa na waa lolote, kwa kosa lolote hata la kutukana mtu. Wapo weusi wengi wametaabika mpaka kuingia uzeeni bila kufanikiwa kupata vibali hivi ambavyo hakika vimekuwa ni fimbo chungu dhidi ya weusi.

Katika mazingira ya namna hii hatua ya Trump ya kuwakaribisha Waafrikana hao kwa mbwembwe zote hizi, kwa kishindo hiki chote, kwa ‘machozi yote ya mamba’ aliyotoa akiwahurumia, ni fursa nyingine kwa Waafrika kujiuliza maswali magumu, kwamba kuwa mtu mweusi ni kosa ukiwa Marekani hata ukiwa Afrika? Ni wakati wa Waafrika kutambua kwamba kupuuzwa kwao kila wanakokwenda hata pale wanapokuwa wanastahili heshima na kuthaminiwa kwa utu wao, sasa iwe ni kichocheo cha kukataa udhalili na kujisimamia wenyewe.

Mpaka sasa bara la Afrika ndilo bado limesheheni rasilimali asilia nyingi kuliko bara lolote. Ni bara ambalo watu wake wakiongozwa na viongozi wake wakiamua kusimama na kukataa ‘ugonjwa’ wa kutembeza bakuli kwa mataifa yaliyopiga hatua ili kupatiwa ‘kitu kidogo’ kwa jina la misaada ya maendeleo, linaweza kujikwamua kwenye udhalili huu. Kwa mara nyingine tena Trump ametuonyesha wazi, kwamba sisi siyo kitu cha maana sana, tusipoamka sasa kama Waafrika, basi tutakuwa tumepoteza fursa ya kupiga teke udhalili wetu.

spot_img

Latest articles

Luhemeja ashuhudia zoezi la usafirishaji Ziwa Victoria

KATIBU Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mha. Cyprian Luhemeja akifuatilia...

Mfalme Zumaridi ashikiliwa na Polisi

Na Mwandishi Wetu Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limesema linamshikilia na kumhoji Diana Bundala...

Msajili hazina aongoza mazungumzo ya uwekezaji na kampuni ya Uswisi

Na Mwandishi Wetu, Abidjan MSAJILI wa Hazina, Nehemiah Mchechu, Mei 14, 2025, ameongoza mazungumzo ya...

More like this

Luhemeja ashuhudia zoezi la usafirishaji Ziwa Victoria

KATIBU Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mha. Cyprian Luhemeja akifuatilia...

Mfalme Zumaridi ashikiliwa na Polisi

Na Mwandishi Wetu Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limesema linamshikilia na kumhoji Diana Bundala...