📌Aomba ushirikiano ili kuhakikisha wananchi wanaendelea kunufaika na umeme wa uhakika.
📌Aahidi Kuendeleza Mazuri yaliyofanyika TANESCO
Na Mwandishi Wetu
MKURUGENZI Mtendaji mpya wa TANESCO, Lazaro Twange ameahidi kuendeleza mazuri yaliyofanywa ndani ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na kuwaomba ushirikiano viongozi na wafanyakazi wa Shirika hilo ili kutimiza azma ya Serikali ya kuhakikisha Watanzania wanapata huduma ya umeme wa uhakika.

Bwana Twange ameyasema hayo Mei 9, 2025 alipowasili rasmi katika ofisi za TANESCO zilizopo Ubungo, jijini Dar es Salaam ambapo alipokelewa Menejimenti ya TANESCO ikiongozwa na Naibu Mkurugenzi Mtendaji (Utafiti, Mipango na Uwekezaji) CPA. Renata
Ndege.

‘’TANESCO imefanya mambo makubwa kwa kipindi cha miaka hii minne. Nawapongeza sana kwa jitihada hizo, nimekuja kuungana nanyi na mimi ni mtumishi mwenzenu. Wananchi wanategemea sana huduma inayotolewa na Shirika hili na nina imani tutashirikiana kuyaendeleza mazuri yaliyofanyika na kuboresha maeneo mbalimbali ili watanzania waendelee kupata umeme’’, amesema Bw. Twange.

Akiongea Kwa niaba ya Menejimenti Naibu Mkurugenzi Mtendaji (Utafiti, Mipango na Uwekezaji) CPA. Renata Ndege amemkaribisha MD Twange na kumuelezea kwa ufupi mikakati mbalimbali inayoendelea kufanywa ndani ya Shirika na kumuahidi kumpatia ushirikiano kutoka kwa Menejimenti na wafanyakazi wote ili kufikia malengo ya Shirika.

Mkurugenzi Mtendaji Twange aliteuliwa kushika nafasi hiyo Mei 6 mwaka huu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kufuatia kifo cha aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo Mha. Gissima Nyamo-Hanga aliyefariki kwenye ajali ya gari na dereva wake Tarehe 13/4/2025.
